Header Ads

Responsive Ads Here

Mambo 5 ya kuyafahamu kuhusu Eid Al-Adha au ‘Sikukuu ya Kuchinja’Na Jumia Tanzania

Katika ya dini ya Kiislamu, Eid Al-Adha au ‘Sikukuu ya kuchinja’ ni sikukuu kubwa inayofanyika baada ya kuisha kwa Hija. Sikukuu hii huashiria kuisha kwa ibada ya Hija eneo la Mina, nchini Saudi Arabia, lakini huadhimishwa na Waislamu duniani kote kama ishara ya kumbukumbu ya imani aliyoionyesha Ibrahimu.
Eid Al-Adha huanza siku ya kumi ya Dhu’l-Hijja, mwezi wa mwisho kwenye kalenda ya Kiislamu, na hudumu kwa muda wa siku nne. Huanza baada ya siku ambayo Waislamu kumali Hija wakishuka kutoka Mlima Arafat.

Sikukuu hii husherehekewa na Waislamu duniani kote, kama zilivyo tamaduni za imani ya dini nyingine. Lakini Eid Al-Adha ni nini? Yafuatayo ni mambo matano ambayo Jumia ingependa uyafahamu kuhusiana na sikukuu hii.   

Historia ya Eid. Eid Al-Adha, ni sikukuu ya Kiislamu inayoadhimishwa kukumbuka tukio la Nabii Ibrahimu kuwa tayari kumtoa sadaka mwanaye wa pekee kwa kuchinja kama alivyoagizwa na Mungu. Ingawa alikuwa ni mtu mwema na aliyempenda mwanawe; imani yake na kujitoa kwa Mungu vilikuwa na nguvu zaidi kiasi ambacho angeweza kufanya chochote alichoagizwa. Kitendo cha utayari wa Ibrahimu kumtoa sadaka mwanaye wa pekee kwa Mungu kilipelekea Mungu kutoruhusu kuchinjwa kwa mtoto yule na badala yake akampatia mwanakondoo kuwa mbadala.

Kitendo cha kuchinja mnyama. Kwa wengi walio nje ya imani ya Kiislamu wamekuwa wakilitafsiri hili tukio tofauti. Kinyume chake, Waislamu huwachinja wanyama wao kwa kutanguliza sala kwanza na kuwachinja kwa jina la Mungu, ambaye amewapa mamlaka juu ya wanyama hao na haki ya kuwala. Hata hivyo, Wailsamu wanapolitaja jina la Mwenyezi Mungu wakati wa kuchinja, ni kutukumbusha kwamba uhai ni kitu kitakatifu. Kwa hiyo kiuhalisia, hukifanya kitendo hiko kwa kumbariki mnyama na kumshukuru Mungu, pamoja na kutambua utakatifu wa maisha ya mnyama.

Nyama hugawiwa kwa familia, jamaa na maskini. Eid Al-Adha pia hujulikana kama ‘Sikukuu ya Kuchinja.’ Kondoo, ng’ombe, mbuzi, au ngamia ni sadaka kwa jina la Mwenyezi Mungu. Nyama itokanayo na sadaka hugawanywa katika mafungu matatu: theluthi moja kwa ajili ya familia, theluthi nyingine kwa marafiki na majirani, na theluthi inayobakia hugawiwa kwa maskini. Sehemu ya nyama ya mnyama aliyetolewa sadaka siyo kwa ajili ya matumizi binafsi pekee, bali kuwasaidia watu maskini pia. Kitendo hiki ni ishara ya utayari wetu kutoa vitu ambavyo tunavithamini, ili kufuata maagizo ya Mungu. Pia huashiria utayari wa kutoa fadhila ili kuimarisha urafiki na kuwasaidia wale wanaohitaji msaada.  

Huashiria kuisha kwa Hija. Hija ni ibada katika dini ya Kiislamu na ni nguzo ya tano ya imani. Eid Al-Adha ni sikukuu ambayo huashiria kuisha kwa Hija kila mwaka, ambapo Waislamu wenye uwezo wa kiafya na kifedha wanatakiwa kufanya angalau mara moja katika maisha yao ikiwa ni sehemu ya imani. Kila mwaka, takribani Waislamu milioni mbili huenda Maka (Mecca) kwa ajili ya Hija.

Inavyosherehekewa. Asubuhi ya kwanza ya Eid Al-Adha, Waislamu duniani kote huhudhuria ibada kwenye misikiti iliyo karibu nao. Inasemekana kuwa baada ya kumaliza ibada ni vema kubadili njia uliyoenda nayo msikitini saa ya kurudi nyumbani. Kubadili njia saa ya kurudi itakupatia fursa ya kusambaza salamu za Eid kwa watu wengi zaidi.

Ni desturi kwa Waislamu katika kipindi hiki cha sikukuu kusherehekea kwa kutoa zawadi, kuvaa nguo mpya, pamoja na kuwatembelea marafiki na jamaa. Kwa kawaida, watu wazima huwapatia watoto pesa kwa ajili ya kutumia kipindi cha Eid Al-Adha. Eid Mubarak! Kwa wote

No comments