Header Ads

Responsive Ads Here

MAKONDA AWAOMBA WAUMINI DINI ZOTE KUHESHIMU MFUNGO WA RAMADHAN, AWAGEUZIA KIBAO WAVAA VIMINI, NGUO FUPINa Said Mwishehe,Globu ya jamii

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amewaomba wanawake wenye tabia ya kuvaa sketi fupi maarufu Vimini na nguo za kubana wakati huu wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan wakaacha kuzivaa katika kipindi hiki ili kuhakikisha waumini wa dini ya Kiislamu wanatekeleza funga hiyo vema.

Makonda ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati anapokea msaada wa tende kutoka kwa Mwenyekiti wa Taasisi Darul Irshad Centre Islamic Tanzania Arif Yusuf AbduRahman kwa kushirikiana na taasisi rafiki ya Muraj Islamic Centre Tanzania.Makonda ameagiza tende hizo zipelekwe katika vituo vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Wakati anazungumzia funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhan ambayo waumini wa dini ya Kiislamu wanaendelea nayo amesema ni vema waumini wa dini zote wakashiriki katika kufanikisha waliofunga wanatekeleza moja ya nguzo za dini hiyo vema.Hivyo amewaomba wanawake wenye tabia ya kuvaa vimini na nguo za kubana katika mwezi huu wakaacha kuzivaa ili kutoa nafasi ya waliofunga kutoingia majaribuni kutokana na mavazi hayo.

"Niwaombe akina dada wanaopenda kuvaa nguo za kubana hasa vimini kuacha kuvaa hadi hapo mfungo utakapokwisha.Natambua wananchi wa Mkoa wa Dar es Salam wapo wenye imani tofauti lakini bado tunayo nafasi ya kuheshimi imani ya kila mmoja wetu,"amefafanua Makonda.Pia ametoa ombi kwa wafanyabishara kutopandisha bei ya vyakula katika kipindi ambacho waumini wa dini ya Kiislamu wanaendelea na mfungo wa mwezi wa Ramadhan.

"Wananchi wa Dar es Salaam niendelee kutoa ombi tuwape ushirikiano ndugu zetu walioko kwenye funga na kwa wafanyabiashara msipandishe bei ya vyakula,"amesisitiza.Kuhusu tende ambazo zimetolewa na taasisi hiyo Makonda amesema zitakwenda kugawiwa vituo vya watoto yatima vilivyopo Dar es Salaam na anaamini kwa kugawa tende hizo kwenye vituo hivyo ni sehemu ya kuwakumbuka watoto walioko huko ambao wapo ambao wapo kwenye funga.

Pia ameishukuru Taasisi ya Darul Irshad Centre Islamic Tanzania kutokana na namna inavyotoa misaada ya aina mbalimbali kwa wananchi wa Dar es Salaam na siku za karibuni wametoa msaada wa magodoro 500 pamoja na vyakula kwa ajili ya kuwasaidia waliokumbwa na mafuruko yalitokana na mvua za masika.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Darul Irshad Centre Islamic Tanzania AbduRahman amesema taasisi hiyo imesema lengo kubwa la taasisi hiyo ni kusaidia jamii yenye uhitaji na kufafanua tende hizo ambazo wamekabidhi leo zimetoka kwa wageni ambao wamekuwa wakija nchini kupitia taasisi hiyo na moja ya mambo ambayo wamekuwa wakifanya wanaporudi kwao ni kusaidia jamii yenye uhitaji.

Awali kabla ya kufika kwa Makonda, AbduRahman ameelezea changamoto anayoipata kwenye taasisi yake ambayo imekuwa ikipokea wageni ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu na lengo la kuja kwao nchini mbali ya kuzungumzia dini wanasaidia wananchi.

Hata hivyo amesema pamoja na wageni hao kuwa na vibali vya kuingia nchini lakini bado wamekuwa wakisumbuliwa na baadhi ya maofisa wa uhamiaji na kufafanua ujio wa wageni hao ni wenye nia njema na sehemu kubwa umejikita katika kusaidia zaidi na ni watu wema.
 Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu wa Taasisi ya Darul  Irshad  Centre Islamic Tanzania wakibeba tende kabla kukabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar  es Salaam leo
 Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu wa Taasisi ya Darul  Irshad  Centre Islamic Tanzania wakibeba tende kabla kukabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar  es Salaam leo
Mkuu wa  Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akizungumza na Mwenyekiti wa Taasisi ya  Darul Irshad Centre Islamic Tanzania AbduRahman leo jijini

No comments