Header Ads

Responsive Ads Here

TANZANIA,HISPANIA WAANDAA KONGAMANO LA BIASHARA NA UWEKEZAJI MJINI MADRID

Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa ambao pia unawakilisha Tanzania katika nchi ya Hispania kwa kushirikiana na Shirikisho la wafanyabiashara la Madrid (Madrid chamber of commerce – CAMARA) pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) uliandaa kongamano la kwanza la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Hispania tarehe 12/03/2018 mjini Madrid. 

Kongamano hilo liliudhuriwa na watendaji wakuu wa makampuni makubwa Madrid nchini Hispania yapatayo 60. Kongamano hilo lilifunguliwa na Bw. Augusto de Castaneda, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Wafanyabiashara la Madrid. Katika kongamano hilo, Mhe. Samwel Shelukindo, Balozi wa Tanzania nchini Hispania, mwenye makazi nchini Ufaransa, aliyashawishi makampuni hayo kuja kuwekeza nchini Tanzania. 

Balozi Shelukindo alieleza juhudi mbalimbali alizozichukua Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamuhri ya muumngano wa Tanzania katika kupambana na rushwa jambo ambalo limetengeza mazingira bora ya kufanya biashara na kuwekeza nchini. Balozi Shelukindo alieleza kwamba hali ya utulivu na usalama ambayo imeendelea kuwepo nchini Tanzania imekuwa ni kivutio kikubwa cha uwekezaji kutoka nje. 

Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambaye alishiriki katika kongamano hilo aliezea mazingira bora ya uwekezaji nchini pamoja na fursa mbalimbali zinazoweza kupatikana Tanzania. 

Pia aliendelea kuelezea jinsi Kituo cha Uwekezaji kilivyojiandaa kuwapokea wawekezaji kutoka Hispania kuja kuwekeza nchini kwa kuwasaidia kujua taratibu na sheria mbalimbali zinazohusu uwekezaji nchini. Aidha Bw. Mwambe alielezea fursa za kipaumbele ambazo ni viwanda, kilimo, miundombinu pamoja na nisharti. 

Bi. Devota Mdachi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) alitoa mada kuhusu vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini Tanzania na kuyakaribisha makampuni ya Hispania kuja kuwekeza katika sekta hiyo muhimu katika uchumi wa Tanzania.

 Bw. Gilead Teri Mkurugenzi wa Sera kutoka Taasisi ya sekta binafsi Tanzania (TPSF) alielezea mchango wa sekta binafsi katika uchumi wa Tanzania na namna Taasisi hiyo itakavyoshirikiana na wawekezaji kutoka Hispania. 

Baada ya kongamano hilo Makamu wa Rais wa Shirikisho la Wafanyabiashara la Madrid Bw. Augusto de Castaneda aliahidi kwamba wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Hispania watafanya ziara nchini Tanzania hivi karibuni kuchangamkia fursa hizo.
Mheshimiwa, Samwel Shelukindo Balozi wa Tanzania nchini Hispania mwenye makazi Ufaransa , Makamu wa Rais wa Madrid Chamber of Commerce Bw. Augusto de Castaneda Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania na Bi. Devota Mdachi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) wakiwa kwenye meza kuu wakati wa kongamano hilo.

Baadhi ya wawakilishi wa makampuni ya Kihiispania walioshiriki kwenye kongamano hilo.

No comments