Header Ads

Responsive Ads Here

Shirika la HAKIZETU lawapiga msasa wasaidizi wa kisheria wilayani Magu


Judith Ferdinand, BGM
Jumla ya wasaidizi 30 wa kisheria ngazi ya jamii (Para Legal) kutoka  vijiji vitatu katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, wamepewa mafunzo ya siku tatu kujengewa uwezo wa kutoa msaada na ushauri wa kisheria kwa wananchi.
Mafunzo hayo yametolewa na shirika la kutetea haki za watoto na wanawake Hakizetu kupitia mradi wake wa Vitendo Vidogo Vidogo Vinaleta Mabadiliko (Aactions Brings Changes), unaofadhiliwa na shirika la Freedom House la nchini Marekani.
Akizungumza juzi kwenye uzinduzi wa mradi huo, Meneja Miradi shirika la Hakizetu Gervas Evodius alisema lengo ni kusaidia maeneo ya Vijijini kupata msaada wa kisheria ili kupunguza vitendo vya kikatili katika jamii.
Alisema mradi huo ambao ni wa majaribio utadumu kwa kipindi cha miezi mitatu na kufanya kazi katika Vijiji vitatu wilayani Magu ambavyo ni Sese na Ighushi vilivyopo Kata ya Bujashi pamoja na Kijiji cha Langi kilichopo Kata ya Lutali.
Alibainisha kwamba mradi huo pia utawafikia viongozi mbalimbali wakiwemo Wenyeviti wa Vijiji, Maafisa Kata, Viongozi wa Dini na Kimila ili kuwaelimisha na kutambua haki zao ikiwemo kutambua namna ya kuwaelimisha watu ambao wanahitaji msaada wa kisheria na kuwaelekeza sehemu ambayo anapaswa kwenda kupata msaada huo.
“Tumetoa mafunzo haya katika Kata ya Bujashi na Lutali ambapo tumechagua Vijiji  vitatu  ambavyo ni Sese, Langi na Ihushi ambapo tunatarajia kuwafikia viongozi 30 wa Serikali za Vijiji, Kata, Dini na Kimila kwa sababu ni watu ambao wako karibu na wananchi na pia tutaendelea kutoa elimu kupitia midahalo ya wazi kwa jamii yote ili  iweze kutambua haki zao na kujua ni kinga gani za kisheria walizo nazo, sehemu gani wanaweza kupata msaada wa kisheria pindi watakapohitaji”. Alisema Gervas.
Wakili wa kujitegemea Paul Bomani alisema wameamua kutoa  mafunzo hayo Vijijini kwa sababu kuna uhitaji wa kisheria na hakuna wanasheria wala mawakili ambao wanaweza kuwasaidia wananchi pindi wanapohitaji msaada wa kisheria ikizingatiwa huko ndiko kuna vitendo vya ukatili kwa wingi.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Sese, Simon Anacret alisema baada  ya kukaa muda mrefu ndani ya uongozi nakuona vitendo vya unyanyasaji kwa watoto wadogo chini ya umri wa miaka 17 wakifanyiwa na wazazi wao, ndipo alishawishika kuliita shirika hilo ili liweze kutoa elimu kwa wananchi na kutambua aina za ukatili kwani wapo ambao hufanya vitendo hivyo bila kutambua kuwa ni kosa kisheria.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walilishukuru shirika la Hakizetu kwa  kuwapatia  elimu hiyo kwani mwanzo walikua gizani na hawakujua cha kufanya hivyo elimu hiyo itawasaidia kupunguza na kumaliza vitendo vya ukatili katika jamii.
“Nalinganisha wasaidizi wa kisheria na mwanga, wanakijiji wenzetu wako gizani na sisi ni mwanga hivyo tutaenda kumulika na kuleta nuru kwa wale wanaoingia katika ukinzani wa kisheria” Alisema Rhoda Amos. Bonyeza HAPA kusoma zaidi.

No comments