Header Ads

Responsive Ads Here

SERIKALI INA MTAZAMO WA KUIFANYA SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI KUWA SEKTA YA UZALISHAJI -ULEGA


Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdalah Hamis Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ameiambia kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji kuwa, Serikali ina mpango wa kuifanya sekta ya Mifugo na Uvuvi kuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa. 

Naibu Waziri HamisUlega ameyasema hayo leo Mkoani Kigoma mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji, ilipokuwa katika ziara ya kutembelea chuo cha wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kampasi ya kigoma jana.

Mhe. Ulega amesema Wizara yake ina Mkakati wa kulinda rasilimali za Mifugo na Uvuvi, kwa kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na kuitoa sekta hiyo kwenye kuchangia kiasi na shilingi Bilioni 19 kwa mwaka katika pato la taifa hadi kufikia kuchangia zaidi ya shilingi Bilioni 50 kwa mwaka.

“Tunaweza kufikia malengo haya kwanza kwa kuimarisha uvuvi wa Bahari kuu kwa kuhakikisha kwanza tasisi yetu ya kusimamia uvuvi wa bahari kuu inakuwa na nguvu kwa kuweka vizuri sheria na kanuni zetu za uvuvi ikiwa ni pamoja na kufufua shirika letu la TAFICO, Alisema Ulega.”

Sambamba na hilo, Ulega alisema Serikali ina mkakati wa kuwa na Meli ambayo itakuwa na uwezo wa kwenda kuvua na kuchakata mazao ya samaki, jambo ambalo litakwenda sambamba na ufunguaji wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya uvuvi.

Naibu Waziri Ulega pia alisema serikali ina lengo la kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya Uvuvi kupitia mafunzo, utafitu na elimu ya ugani kupitia vyuo vya Feta , ili kuweza kuwa na wataalam wa kutosha pamoja na kuipa nguvu wakala hiyo ili kuweza kutoa wataalam kwani mpaka sasa sekta ya uvuvi ina uhaba wa wataalam na kuongeza kwa kusema kuwa kwa upande wa utafiti serikalii ina mkakati mkubwa wa kuweza kuiwezesha TAFIRI kwa kuipa kazi maalum za tafiti akitolea mfano wa uelewa mdogo wa baadhi ya wavuvi kuhusiana na zana halali za uvuvi.

Akizungumzia suala la kuingiza samaki aina ya vibua na sato kutoka nje ya nchi, Ulega alisema, “Ukiangalia kwa makini sioni sababu ya kwanini tutoe mathalani kiasi cha shilingi Bilioni 50 kwa mwaka tuwapelekee wavuvi wengine na tuingize tani elfu 20 na zaidi kuleta hapa ndani za samaki ambao sisi wenyewe tunao.” Alisisitiza Ulega.

“ Ipo Mikakati kwa serikali ya kuwatengenezea wafanya biashara ya samaki mazingira mazuri ili pesa hiyo iwekezwe hapa nchini.” Alisema.

Awali akitolea mfano wa ulinzi wa rasilimali za uvuvi Ulega alisema “Tumefanya ulinzi wa rasilimali za uvuvi katika ziwa Victoria kwa muda mfupi tu ikiwa ni pamoja na ulinzi wa utoroshwaji wa Mazao ya Uvuvi nje ya nchi na tumeingiza kiasi kikubwa cha fedha.” Alisema.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Sekta ya Uvuvi Dkt. Yohana Budeba alisema kuwa njia ya ufugaji wa samaki wa kisasa kupitia chuo cha FETA kitatengeneza wataalam na kuongeza ajira na kupatikana samaki wengi na kupelekea mchango mkubwa wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa taifa hili.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Hamis Ulega (Mb) kulia akiongea na Wabunge wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji ilipotembelea chuo cha wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kampasi ya Kigoma jana, wabunge wa kamati hiyo wameambata na maafisa mbali mbali kutoka serikalini.
Kushoto Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Hamis Ulega (Mb) akizunguma katika kikao na Wabunge wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji katika chuo cha wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kampasi ya Kigoma jana, kati kati ni mwenyekiti wa kamati Hiyo Mhe. Mahmoud Hassan Mgimwa (Mb.) Kalenga na kulia ni Makamu Mwenyekiti Mhe. Christine Gabriel Ishengoma (Mb).
Pichani Mbele ni baadhi wa wabunge wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji wakifuatilia mazungumzo katika kikao wakati wa ziara yao katika chuo cha wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kampasi ya Kigoma jana,wengine ni watumishi wa serikali.

No comments