Header Ads

Responsive Ads Here

Mkurugenzi Kituo cha Huruma ahimiza watoto wenye ulemavu kupewa fursa

Judith Ferdinand, Mwanza
Wazazi wenye watoto wenye ulemavu mbalimbali wametakiwa kuwapa kipaumbele watoto hao katika fursa mbalimbali ikiwemo elimu kama ilivyo kwa watoto wasio na ulemavu.
Mkurugenzi wa Kituo watoto wenye ulemavu Huruma kilichopo Jijini Mwanza, Boniventura Toto ametoa rai hiyo wakati akizungumza na BMG ofisini kwake na kuongeza kubainisha wazazi wengi wenye watoto wenye ulemavu hudhani watoto hao hawawezi kufanya chochote na kwamba ni mzigo kwao jambo ambalo si sahihi.
Toto alisema wazazi wanapaswa kutambua kuwa watoto hao ni kama walivyo wengine na wanauwezo wa kufanya mambo mbalimbali, tofauti yao ni kuzaliwa na changamoto ya ulemavu ambao unaweza kumpata hata mtu mzima.
Alisema ni wajibu wa wazazi hao kuwatimizia mahitaji yao ikiwemo kuwapeleka shule ili waweze kupatiwa elimu itakayowasaidia kujitambua na kuweza kujitegemea wenyewe.
Pia alisema watoto hao wanauwezo wa kufanya jambo lolote kama walivyo wengine,hivyo aliwaomba wazazi kuacha kuwafungia ndani,na kuwatelekeza kwa bibi zao vijijini sambamba na kuachana na mila potofu za kudhani  ni laana au mikosi.
Hata hivyo aliiomba serikali inapotenga bajeti kwa ajili ya watoto iwape kipaumbele zaidi watoto wenye ulemavu ili waweze kupata elimu itakayowasaidia kujiajiri wenyewe na kuacha kuwa tegemezi hali itakayosaidia kupunguza umaskini na taifa tegemezi.
Aidha alisema wajibu na mkazo wa serikali  ambao wanauweka kwa watoto wa kawaida uwekwe na kuongezwa kwa watoto wenye uhitaji maalum na wazazi wale ambao wanawafungia ndani na kuacha kuwapeleka shule wachukuliwe hatua kali kama ilivyo kwa wengine.
Vilevile alisema katika kuonyesha kuwa watoto hao wanaweza wanatarajia kuanzisha darasa kwa ajili ya kuwafundisha stadi  za maisha ambapo watawajengea uwezo wa kutengeneza vitu mbalimbali.
Baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu katika Kituo cha Huruma Jijini Mwanza wakifanya usafi wa mazingira kituoni hapo.

No comments