Header Ads

Responsive Ads Here

Kampuni ya Acacia yazidi kuwajengea uwezo wafanyakazi wazalendo

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Acacia nchini Tanzania, Asa Mwaipopo (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa program hiyo.
Na Dickson Masindi
Kampuni ya madini ya Acacia Tanzania imetangaza adhma yake ya kuwaendeleza na kutambua wafanyakazi wenye vipaji vya uongozi ndani ya kampuni hiyo na kuwajengea uwezo zaidi ili kuja kushika nyadhifa za juu za uongozi katika kampuni hiyo.
Adhma hiyo ilitangazwa mwishoni mwa wiki Jijini Mwanza na Mkurugenzi Mtendaji wa Acacia Tanzania, Asa Mwaipopo wakati akizungumza kwenye mahafali ya kuwatunuku vyeti wafanyakazi 105 wa kampuni hiyo waliohitimu mafunzo maalum ya uongozi yalioandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao.
“Dhamira ya Acacia Tanzania ya kuendeleza ujuzi wa wafanyakazi wetu inaendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 na awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo wa Serikali ambao unalenga kutoa mafunzo na ujuzi katika sekta ya madini ili kusaidia ukuaji wa uchumi na viwanda nchini Tanzania,’’ Alisema.
Kwa mujinu wa Mwaipopo tangu kuazishwa kwake, programu hiyo maalumu ijulikanayo kama ‘Rainbow Leadership Development Programme’ imewezesha kampuni hiyo kupunguza utegemezi wa wafanyakazi wa kigeni kwa asilimia 85% ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Hadi kufikia mwaka 2017, asilimia 96.2% ya wafanyakazi wa Acacia ni raia wa Tanzania.’’ Alibainisha huku akiongeza kuwa kupitia programu hiyo, Acacia imetoa mafunzo kwa viongozi katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na madini, uhandisi (mitambo, umeme, kiraia), metalojia, jiolojia, na mazingira.
Mahafali hayo yametimiza awamu ya nne ya programu hiyo toka kuanzishwa kwake mwaka 2016.
“Nawapongeza wahitimu wote kwa mafanikio haya makubwa. Mbali na kujiwekea msingi mzuri wa kupata nafasi za juu zaidi za uongozi ndani ya Acacia, mmejiweka katika nafasi nzuri ya kusimama na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kusaidia mapunduzi ya viwanda nchini,” alisema.
Mafunzo ya programu hiyo hutolewa kupitia mfululizo wa madarasa, mitihani na kazi (workplace assignments).
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miezi sita, wahitimu wamemaliza kozi nane tofauti za uongozi zikiwemo ufanisi katika mawasiliano, utamaduni wa uongozi, kanuni za tahadhari za Kampuni na malalamiko, ustawi mahali pa kazi, kusimamia mahusiano ya kibinafsi, kujenga imani na kutumia mifumo ya ndani.
Alisema kuwa ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita, jumla ya wafanyakazi 204 katika migodi mitatu ya Acacia – North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi – wamehitimu programu hiyo.
Tangu kuanzishwa kwa programu hiyo, kampuni imeanza kuona matokeo chanya, ikishuhudia ongezeko la kiwango cha uzalishaji na usalama katika migodi yake yote mwaka 2017, kwa mujibu wa Mwaipopo.
“Mtazamo wa Acacia umejikita katika kuimarisha nguzo zetu kuu tatu ambazo ni; biashara yetu, watu wetu na mahusiano yetu, wakati tukiendelea kuwekeza kufikia maono yetu ya kujenga kampuni inayoongoza Afrika.’’ Alitaja.
Meneja kampuni ya madini ya Acacia anayeshughulikia ukuaji wa biashara, Rodney Burges (kushoto) akimkabidhi cheti mfanyakazi wa Mgodi wa madini wa Buzwagi, Morice Ndagija wakati wa mahafali ya kuwatunuku vyeti wafanyakazi 105 wa Acacia waliohitimu mafunzo maalum ya uongozi yalioandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Acacia Mining Plc, Peter Geleta (kushoto) akimvalisha koti Godfrey Kihumbe (katikati)kutoka Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi wakati wa mahafali ya kuwatunuku vyeti wafanyakazi 105 wa Acacia waliohitimu mafunzo maalum ya uongozi yalioandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao. Anaeshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Acacia Tanzania, Asa Mwaipopo.

No comments