Header Ads

Responsive Ads Here

WANANDOA WASHIKILIWA KWA WIZI WA MTOTO WA SIKU MOJA WODINIShangwe na vilio vimetawala katika Kata ya Iganzo jijini Mbeya baada ya mtoto wa kike wa siku moja aliyeibwa katika wodi ya wazazi kupatikana akiwa hai.

Wanandoa Happy Charles (24) na Chiluba Peter ambaye ni dereva wa teksi anayeegesha eneo la Hospitali ya Mkoa wa Mbeya wanashikiliwa na Polisi wakituhumiwa kuhusika na wizi huo.

Februari Mosi, 2018 mwanamke aliyejifanya muuguzi wa Hospitali hiyo aliingia katika wodi ya wazazi na kumchukua mtoto wa Sarah Mwasanga (40) kwa madai ya kwenda kumpatia chanjo.

Akizungumzia tukio hilo jana  Februari 3, 2018 Kaimu Mganga Mkuu wa Hosptali hiyo, Yahaya Msuya amesema mara baada ya tukio hilo mama wa mtoto huyo alitoa taarifa kwa uongozi wa hospitali.

Amesema baada ya kupata taarifa hizo, uongozi wa hosptali kwa kushirikiana na polisi na wananchi waliweka mitego katika maeneo mbalimbali iliyowezesha kukamatwa watuhumiwa.

Msuya amesema mtuhumiwa alifika hospitali ya mkoa akiwa katika pikipiki huku akiwa amebeba kitu mfano wa mtoto na alipohojiwa na walinzi aliwaeleza kuwa ana mgonjwa aliyeandikiwa sindano za masaa.

Amesema hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri na yupo katika uangalizi wa madaktari kutokana na mazingira waliyomkuta baada ya kuibwa.

Mama wa mtoto huyo amesema, “Siamini kilichotokea, nilitambua mwanagu amechukuliwa kimazingira na mwanamke aliyefika katika wodi ya wazazi akiwa kama muuguzi kwa kweli yote namwachia Mungu.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mpaka sasa wanawashikiliwa wanandoa hao.

Amesema bado wanaendelea na taratibu za kisheria za kuwahoji na watafikishwa mahakamani wakati wowote mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Na Hawa Mathias, Mwananchi 

No comments