Header Ads

Responsive Ads Here

WANANCHI 300 WA KITONGOJI CHA KINACHERE,HANANG WAANZA UJENZI WA KISIMA NA TENKI LA KUHIFADHIA MAJI YA MVUA


Na Jumbe Ismailly -HANANG    


WANANCHI  300 wa Kitongoji cha Kinachere,kata ya Sirop,tarafa ya Simbay,wilayani Hanang,Mkoani Manyara kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Hanang wameanza ujenzi wa kisima na tanki la kuhifadhia maji ya mvua ili waweze kuondokana na adha ya kufuata huduma hiyo  umbali wa zaidi ya mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji hicho,Peter Qwendo alisema mradi huo utakapokamilika unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi milioni 49 na kwamba kati ya kiasi hicho cha fedha nguvu za wananchi ni asilimia kumi ya gharama za mradi huo kwa kufanyakazi ya kukusanya mawe,mchanga,kokoto,kuchota maji na kumwagilia.
Aidha Qwendo ambaye pia ni mmoja wa watu waliokwenda nchini Kenya kupata mafunzo juu ya usimamizi wa shughuli hiyo,alisema wananchi hao wanaoishi katika kaya 107 wamekuwa wakiifuata huduma hiyo katika Kitongoji cha Ghata kilichopo umbali wa takribani kilomita 14 kwenda na kurudi.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mpango wa afya wa Kijiji cha Nangwa,Apolei Wilbrod aliweka bayana kwamba wafadhili wa mradi huo ni Medical Missionary Of Mary Nangwa wanaoendesha huduma za kliniki ya mama na mtoto katika wilaya ya Hanang. 
Kwa mujibu wa Wilbrod mradi huo ulioanza tangu mwaka 2014 kwa miradi ya aina nne,kabla ya kuanza kwa mradi huo wa tano na madhumuni yake yalikuwa kuwasaidia wananchi waliopo kwenye maeneo hayo na kwamba unaotarajiwa kukamilika katika kipindi cha mwezi mmoja na utagharimu jumla ya shilingi milioni 49,700,000/=.
Hata hivyo Msimamizi huyo wa mradi alitumia pia wasaa huo kutoa wito kwa wadau wengine kujenga utamaduni wa kushirikiana wakati wote na jamii kwa kufurahia miradi husika ili iweze kuwasaidia wananchi.
Mbunge wa jimbo la Hanang,Dk.Mary Nagu aliyetembelea mradi huo kwenye ziara yake inayoendelea katika jimbo hilo alibainisha kuwa utaratibu mzuri waliojiwekea ni kwamba wananchi wanalazimika kuchangia asilimia kumi na Halmashauri asilimia kumi.
Hata hivyo mbunge huyo aliunga mkono wananchi hao kwa kuwaahidi kuwapatia malori matano ya mchanga na atawasiliana na Halmashauri ili kufahamu imechangia kitu gani katika mradi huo.
“Mradi umechelewa hela zimekuja zikakaa sasa basi tuonyeshe kwamba na sisi tunataka maji kwani maji ni uhai,hamtaki maji,mmenionyesha mnataka kwa sababu mmejitolea na kazi inaenda kwa kasi sana.”alisisitiza Mbunge huyo wa Jimbo la Hanang.
Ramadhani Hamisi ni fundi wa kujenga kisima na tenki la maji katika mradi huo anaweka bayana kwamba tenki hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kujaza lita laki moja za maji na wanatarajia kukamilisha kujenga katika kipindi cha mwezi mmoja.
ananchi wa Kitongoji cha Kinachere,kata ya Sirop,Tarafa ya Simbay wakifanya kazi za mikono kuhakikisha mradi huo unakamilika katika kipindi cha mwezi mmoja na kuanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama.
bunge wa Jimbo la Hanang,Dk.Mary Nagu akiungana na wananchi wa Kitongoji cha Kinachere kufanyakazi za kukusanya na kusomba mchanga wa kujengea kisima pamoja na tenki la kuhifadhia maji ya mvua na kuahidi kuchangia lori tano za mchanga.
Mbunge wa Jimbo la Hanang,Mkoani Manyara,Dk.Mary Nagu(wa kwanza kutoka kushoto) akikagua ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji ya mvua linalojengwa juu ya mawe.
mafundi wa kujenga kisima wakiendelea na kazi ya kusuka nondo za kisima kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wake katika kipindi cha mwezi mmoja.(Picha zote Na Jumbe Ismailly)
Ni Mbunge wa Jimbo la Hanang,Mkoani Manyara,Dk.Mary Nagu(wa kwanza kutoka kushoto) akipata maelezo mafupi ya mradi wa ujenzi wa kisima na tenki la kuhifadhia maji ya mvua kutoka kwa msimamizi wa mradi huo,Apolei Wilbrod.

No comments