Header Ads

Responsive Ads Here

Shilingi milioni 208 zanufaisha kaya maskini TASAF Kishapu


Na Robert Hokororo, Ofisi ya Mkurugenzi.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kishapu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imetoa sh. milioni 208.5 kwa ajili ya kuwezesha kaya maskini katika kipindi cha Januari hadi Februari.
Mratibu wa TASAF wilaya hiyo, Sospeter Nyamuhanga amebainisha hayo jana ambapo amesema fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya kaya 5959 katika vijiji 78 vilivyopo wilaya humo.Alisema kuwa zoezi hilo limeendelea kupata mafanikio kutokana na walengwa wengi kufanyia kazi elimu wanayopewa kuhusu matumizi sahihi ya fedha hizo wanazowezeshwa.
Nyamuhanga aliongeza kuwa kutokana na ufuatiliaji unaofanyika nyakati tofauti baadhi ya kaya zimeonesha mabadiliko kimaisha ambapo zimetumia fedha hizo kuboresha maisha yao kwa kufanya shughuli mbalimbali za kujipatia kipato.
Alifafanua kuwa katika kaya hizo imebainika kuwa wanufaikaji wameweza kununua mifugo ikiwemo mbuzi, kondoo  na kuku huku wengine wakifanya biashara ndogondogo.Aidha, alisema baadhi ya walengwa tayari wamebadilisha aina za makazi yao kutoka nyumba za tembe na nyasi za awali na kuanza kujenga nyumba za kisasa za bati hali inayoleta matumaini katika miradi kama hii.
“Lengo la mpango wa TASAF siku zote ni kuziwezesha kaya maskini kujikwamua kiuchumi na ndiyo maana mara kwa mara katika mazoezi haya tunatoa elimu ili kuwaelekeza namna bora kutumia fedha wanazowezeshwa,” alisema.
Mratibu huyo alisema pamoja na mambo mengine pia walengwa wanapopata fedha hizi wanawajibika kuwapeleka watoto wao shule na kliniki kama ambavyo masharti yanavyoelekeza.Alisisitiza umuhimu wa elimu kwa watoto wa walengwa kwani wanavyoelimika ndivyo wanaondosha umaskini na kuchangia kujikwamua katika umaskini kwa kaya zao.
Pia aliendelea kuwataka walengwa wanaonufaika na fedha hizo za mpango huo wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kupata matibabu wakati wowote wanapohitaji.   TASAF imekuwa ikitoa ruzuku ya msingi kwa kaya zote maskini zilizoandikishwa kwenye mpango na nyingine ya utimizaji masharti ambayo hutolewa kwa kaya zenye watoto wanaotakiwa kwenda shule na vituo vya kutolea huduma za afya.
Kishapu ni miongoni mwa halmashauri za wilaya 161 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba zinazotekeleza Mpango wa TASAF III ili kuongeza kipato na fursa za kuboresha upatikanaji wa mahitaji muhimu.
 Zoezi la uwezeshaji Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) likiendelea katika kijiji cha Mwigumbi kata ya Mondo ambapo mmoja wa walengwa akiwawezeshwa ruzuku.
 Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Sospeter Nyamuhanga (wa pili kulia waliosimama) akipata maelezo kuhusu zoezi hilo alipofika kufanya ufuatiliaji kijiji cha Wela kata ya Uchunga.
 Sehemu ya walengwa wa TASAF wakiwa katika zoezi la uwezeshaji kwenye kijiji cha Mwigumbi kata ya Mondo.
Zoezi likiendelea katika kijiji cha kijiji cha Wela kata ya Uchunga.

No comments