Header Ads

Responsive Ads Here

MHADHIRI UDSM ATOA USHAURI KWA SERIKALI KUHUSU WATAALAMU WA MASUALA YA UMEME

Na Mwandishi Wetu

MRATIBU wa Jukwaa la Nishati Tanzania, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Hudson Nkotagu ameishauri serikali kuongeza juhudi ya kuwafundisha wataalam wa masuala yanayohusu umeme kwa kuangalia vyanzo vya umeme husika.

Profesa Nkotagu alisema hayo alipokuwa akizungumza na Habari Leo jijini Dar es Salaam, ambapo alisema nchini Tanzania kuna nishati za aina mbili kubwa, zikiwemo vile ambazo zikitumika hazirudi tena kwa mfano gesi, mafuta, makaa yam awe na urani pamoja na vile vyanzo vyake vinavyojiendeleza vyenyewe kiasili.

Akitolea mfano wa hizo zinazojiendeleza zenyewe kiasili alisema ni nishati ya sola, upepo, maji, mawimbi ya bahari na kuni.

Alisema hivyo serikali itakapowafundisha wataalam hao iangalie vyanzo hivyo vya nishati akitolea mfano eneo la nishati ya urani kwamba huko yamkini hakuna wataalam wengi au waliopo ni wachache.

Kwa upande mwingine alisema ni veme serikali ikawashirikisha wananchi wote kwa kuwapa elimu ya kulipa pale wanapopata huduma hiyo ikiwa ni pamoja na taasisi za serikali kulipa madeni yao ili kuondokana na changamoto ya nishati ya umeme nchini.

“Sioni sababu taasisi za serikali kutokulipa madeni yao wanayodaiwa, kwa kufanya hivyo Tanesco haitaweza kujiendesha vizuri,” alisema.

Profesa huyo alisema katika kuleta ufahamu wa mambo hayo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kwa kushirikiana na vyuo vikuu vingine vinatoa uelewa kwa wananchi wote pamoja na taasisi za serikali kuhusu masuala na changamoto za nishati.

Vile vile kufanya tafiti zinazohusu  nishati ikiwemo kuishauri serikali pale inapobidi kuhusu masuala ya nishati pamoja na kufanya makongamano mbalimbali.

Vyuo hivyo vingine ni Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) pamoja na vyuo vikuu vinne kutoka Uholanzi ambavyo ni Twente, Ultrecht, Hanze na Delft.

No comments