Header Ads

Responsive Ads Here

DIAMOND SOMA NILOCHOANDIKA KUHUSU WEWE NA ZARI, NAMUOMBA MUNGU ASIKURUDISHE ULIKOANZIA


Na said Mwishehe,Globu ya Jamii

NI ngumu kuzungumzia mahusoano ya kimapenzi ya watu wengine lakini kuna wakati unaamua kufumba macho na kuziba masikio useme japo kidogo.

Nikiri mahusiano ya kimapenzi wakati mwingine hukumbwa nachangmoto nyingi.Mungu nisaidie nifikishe ujumbe kwa ufasaha.Hata hivyo siri ya mtungi aijue kata.Wengine huwa ni wa kupata taarifa...bwana umesikia jamaa ameacha mpenzi au mke.

Wakati mwingine unaweza kuambiwa ndugu yangu yule mshikaji wako kaachwa na mkewe au mpenzi wake.Ni mambo ya kawaida kusikia waliokuwa na mapenzi moto na pengine kuwa ya mfano wa kuigwa yamefika tamati.Hata hivyo swali la msingi huwa watu wanataka kujua kwanini waliokuwa wanapendana wameachana.Hivyo sababu ndio huibua mjadala kwenye jamii.

Tena usiombe walioachana wakiwa ni watu maarufu na wenye kukubalika na kupendwa zaidi.Nikiri kwenye maisha yangu ya uandishi yaliyoanza rasmi mwaka 2001,sikuwahi kabisa kuandika chambuzi au maoni inayozungumzia wapenzi kuachana.

Sikuwa na sababu ya kufanya hivyo kwani ni maisha binafsi ya watu wawili walioamua kupenda na kukaa pamoja na hatimaye wakaamua kuachana.Kwa mazingira ya aina hiyo unatoa maoni au kuandika uchambuzi il iweje?Hivyo huwa napotezea na ndio maana hata hili la juzi la Mkuu wa Wilaya fulani(jina kapuni) kutumia mitandao ya kijamii kumpongeza mumewe kuongeza mke wa pili kichwani kwangu halikunisumbua maana halina uhusiano na maendeleo ya Watanzania.

Ingawa aliyesema ni kiongozi wa umma na matendo yake wakati mwingine yana nafasi ya kuigwa na wengine hasa yale matendo mema.Nikiri kabla kuvunja mwiko huu wa kutoandika habari za uhusiano wa kimapenzi,niliamua kufanya mawasiliano ya kutosha na halmashauri ya ubungo wangu mwisho wa siku moyo,mwili na akili vikakubaliana si dhambi kuelezea walau kidogo.

Naomba niombe radhi kwa nitakaowakwaza kwa namna yoyote ile kwani kwenye maisha yetu haya lile ambalo wewe unaliona haliko sawa kwa mwingine anaona zuri na kulipa maksi za juu.Ndio maisha ya binadamu yalivyo.Hivyo niombe msamaha kwa yule ambaye kwa namna moja au nyingine nitamkwaza.

Naomba nianze kwa kuelezea masikitiko yangu makubwa baada ya kusikia taarifa za Nasibu Abdull maarufu Diamond kuachana na mpenzi wake ambaye ni mama wa watoto wake wawili Zarinah Hassan a.k.a The Boss Lady.Sitaki kusema kama Diamond kaachwa au kaacha lakini kwa lugha nyepesi ni kwamba wawili hao penzi limefika mwisho.

Yaani kama nitatumia moja ya wimbo za Diamond niseme penzi la Diamond na Zar sasa Zilipendwa.Inasikitisha sana lakini ndio hivyo.Kwanini wameachana? Ni swali gumu kulijibu ila fahamu tu hakuna mapenzi tena kwa sasa kati yao.Taarifa za wawili hao kuamua kuachana zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kama utani.Si unajua tena mambo ya wasanii wetu kuna wakati unaweza kuumiza kichwa kumbe wenzio wanatafuta kiki.

Hata hivyo nikaanza kumtafakari Diamond,alikotoka,alipo na hatua ambayo amefikia kwenye muziki huo. Nikaanza kujiuliza ni kweli taarifa za kuachwa ni kitafuta kiki?Kichwa changu hakikukubali kirahisi.Nikasema ngoja nikae kimya maana unaweza kuzungumzia jambo hewa na kibaya zaidi huwa sina utaratibu wa kuzungumzia mapenzi ya watu.

Nikawa nasubiri maana nikiri tu binfasi ni miongoni kwa mashabiki wa muziki wa Diamond ,imefikia hatua kuishi na bango lenye nembo ya WCB kwangu ni jambo la kawaida.Basi bwana kama unavyojua msanii unayempenda lazima utafuatilia na maisha yake. Na kazi yangu hii ya kuandika andika imenifanya nifuatilie maisha ya wasanii mbalimbali maana wanafanya kazi nzuri na naifurahia.

Maana maisha tunayoishi nayo yametawaliwa na changamoto nyingi za kimaisha,hivyo nyimbo za wasanii zimekuwa sehemu ya tulizo la moyo.Juzi sasa nikapata jibu, kweli Zari na Diamond wameachana.Ujue kwanini ?Nimemsikia Zari kwa masikio yangu akielezea kufika mwisho kwa penzi lao.Ameeleza sababu kadhaa na zote kwangu lawama nazielekeza kwa Diamond. Amevuruga penzi kwa mikono yake.

Wakati naandika nikaanza kukumbuka mashairi ya wimbo wa Nandy unaosema Kivuruge.Kuna sehemu anaomba "Umekuwa kivuruge unavuruga sana". Yale maneno ya wimbo huo yafanye sasa ndio anaimba Zari.Acha niendelee Diamond amesahau alikotoka,maisha ambayo amepitia kwenye masuala ya mahusiano.Kabla ya kukutana na Zari Diamond amepita kwenye msururu wa warembo.

Ama kweli mwenye asili haachi asili.Ukijumlisha umaarufu ,fedha ,kipaji na mafaniko akajisahau ndugu yangu Boy from Tandale kwani ameanza kurudi kule kule.Leo Zari ameshindwa kuvumilia.Zari anasema wakati anahojiwa na BBC kuwa amevumilia ameshindwa.Diamond amekuwa akifanya mambo ya kumvunjia heshima.Ile stori ya kuzaa na binti mwenye uzuri wake Hamisa Mobeto ilimuumiza sana The Boss Lady.Ndivyo anavyosema.

Akajipa moyo kuwa huenda Diamond atajifunza na kuacha kumbe wapi.Zari anasema wakati akiendelea kufikiria aina ya maisha ya mzazi mwenzake kwenye mambo ya mahusiano ghafla anaona zile picha akiwa amekumbatiana na Wema Sepetu.

Usiniulize kwanini?Kwani hujui kama Diamond kabla ya kuwa na Zari ameishi sana na Wema.Basi tena Diamond akiwa na Wema hapa juzi kati ameeleza mengi na kuwaambia mashabiki wake yeye na Wema hawana matatizo tena na ni marafiki wakubwa.Kumbe Zari anamsikia .Unajua kilichoafuata? Moyo wa Zari ukasema sasa basi.Cha kwanza akaamua kudhibiti mawasiliano ya Diamond yasimfikie.Kwa kifupi amekata mawasiliano.Hataki tena kuwasiliana na Diamond.Pata picha nini kinaendelea.Itoshe kusema nimemsikia Zari akizungumzia kumuacha Diamond na kwamba sasa atajikita kwenye shughuli zake binafsi.

Kauli hiyo kimsingi ndio imenisukuma kivunja mwiko wa kuandika habari za mahusiano ya mapenzi ya watu na baada ya leo sitaandika tena.Iko hivi nayaangalia maisha ya Diamond baada ya kuachana na Zari.Nakumbuka historia yake Diamond kwenye mambo ya mapenzi anapokuwa na binti wa Kitanzania haikuwa vizuri.

Diamond aliyekuwa na Wema sawa alikuwa tayari maarufu lakini baada ya kuingia kwenye mikono ya Zari ,Diamond akaanza kuonekana msanii anayejua nini anachokifanya kwenye muziki.Akapiga hatua kiasi cha kumshangaza kila mmoja wetu.Diamond wakati akiwa na Wema alitambata na nyimbo kadhaa kikiwamo kibao chake cha Mbagala ambacho ndicho kilimtambulisha rasmi.

Alipokuwa na Zari ,Diamond akaanza kuwa msanii mkubwa na wa kimataifa.Dunia leo hii inamjua Diamond.Ametambulika kila mahali kutokana na kipaji chake kwenye muziki wa kizazi kipya.Kama ukitaka ushahidi wa uwezo wa Diamond usiniulize mimi Said Mwishehe,nenda kawaulize akina DJ Khalifa,Chris Brown ,Neyo na hata wale akina Morgan Heritage waliomba naye wimbo wa Halleluya.

Huku wengine tukianza kubishana kuhusu uwezo wa Diamond tunapoteza muda maana wenye muziki wao wanamjua.Ila ndio hivyo tena amefanikiwa kupenya kwenye muziki lakini ameshindwa kupenya kulinda penzi lake kwa Zari.Unaweza kujiuliza Diamond nini kimemtokea,ni utoto? Hapa kwani ni mtu mzima.

Unaweza kujiuliza ni ulimbukeni wa mapenzi?Hapana kwani Diamond si limbukeni.Unaweza kujiuliza amepitiwa na shetani?Hapana kwani nani amemuona Shetani.Unaweza kujiuliza ameharibu penzi kwa sababu ya uzuri wa Wema na Hamisa?Akili yangu inakataa kabisa maana kwa Zari anakila kitu.Ni mrembo,anavutia, ana akili na kubwa zaidi ana sifa zote za kuwa mke.

Diamond amekosea sana kumvunjia heshima Zari kwa kurudi kwenye kupiga picha za kukumbatiana na watu alipokuwa ana mahusiano nao huko nyuma.Tangu Zari awe na Diamond aamekuwa makini sana kuilinda nyumba yake.Amejitahidi kutunza heshima ya Diamond, amejitahidi kuwathibitisha Watanzania yeye ni mwanamke sahihi kwa Diamond.

Kwa bahati mbaya aliyepewa heshima zote hakuona.Sijui ni upofu? Hapana. Diamond ni msanii anayejua nini anachokifanya na kwenye hili huenda anajua anachokifanya.Lakini ukweli amekosea sana tena sana,Diamond kuachana na Zari umefanya kosa kubwa.Kibaya zaidi ni kwa sababu za kitoto kabisa.Ulishindwa nini kufanya mambo yako kwa siri.Kuna wanaume wangapi wana nyumba ndogo na bado wanaheshimu nyumba zao.

Sawa Diamond moja ya nyimbo yake amesema "Sikomi" tena ukaongeza licha ya mateso haya.Brother umemkosea sana kuachana na Zari.Leo huenda hata Tiffah na Nillan waliokuwa wamezoea kukuona kila wanapofumbua macho sasa wanaanza kuona tofauti.Ndio maana baba yupo kwake na mama yupo kwake.

Angalia unavyoingiza watoto kwenye shida.Kisa picha za kukumbatiana na aliyekuwa mpenzi wako.Ulishindwa kutafakari?Mbona kwenye nyimbo unatafakari kabla na ndio maana ukatuteka wengi na kuwa upande wako.Umeshindwaje kutafakari unayoyafanya kwa Zari.

Diamond unakumbuka kuna wakati Zari alipost picha kwenye mitandao wake wa kijamii akiwa na mwanaume mwenye bwawa la kuogolea akiwa Afrika Kusini.Nakumbuka ulikuja juu na ukaweka post ukisema ndio maana unakulaga tu.Sijui ulikuwa na maana gani.Zari akaitolea ufafanuzi ile picha kuwa alikuwa ni ndugu yake na picha hiyo ilipigwa na mke wa huyo ndugu.

Ukasemehe na maisha yakaendelea.Sasa pata picha wewe tukio moja tu lilikutesa,je wewe unayoyafanya kwake unamtesa kwa kiasi gani.Naomba unisamehe Diamond,naomba mashabiki wako nao wanisamehe huenda nachokiona mimi ni kibaya kwa wengine kikawa poa na wanakupongeza.

Hata hivyo naangalia maisha yako kimuziki.Nikiri naanza kupata wasiwasi na sikuombei mabaya lakini kama naanza kuona unarudi ulikotokea.Naomba Mungu nachowaza kisiwe maana umeliwakilisha vema taifa kwenye tasnia ya muziki wa kizazi kipya.Tunahitaji kuona ukiendelea kubaki keleleni kwenye muziki. Chondechonde angalia namna ya kuomba radhi kwa Zari.

Na kuomba radhi si kosa au dhambi bali ni njia ya kujisahihisha na kujiimarisha.Kuna hatari ya mipango yako mingi kushindwa kuendelea kama ulivyoipanga.Najua unao mameneja wenye uwezo mkubwa wa kukusimamia lakini nyumba ikiyumba na kazi nayo inayumba.Kumbuka ile kauli kwenye mafanikio ya mwanaume nyuma kuna mwanamke.Hivyo kwenye mafanikio yako nyuma yako yupo Zari.

Tulizoea kila wiki tunasikia nyimbo mpya kutoka kwako lakini sasa wiki imekata.Unajua kwanini?Nyumba haiko sawa.Utajipa moyo kuwa yatapita na wanawake wako wengi sawa.Ila kumbuka hata wakiwa wengi kiasi gani lakini hatakuwa wa aina ya Zari.

Ni salamu zangu kwako Diamond,Simba,Boy from Tandale na majina mengine mengi .Hata lila Chib Dangote.Nihitimishe kwa kueleza tu ni mtazamo tu na nilichoandika si sheria,kanuni wala taratibu.Nikuombe Diamond soma nilichaondika kuhusu wewe na Zari.

Ni mawazo tu yamejikusanya kichwani na kwa ujinga wangu nikaona acha niyaandike yaonekane.Alamsiki.Jumapili iwe njema kwetu sote.

UKITAKA KUWASILIANA 0688534011

No comments