Header Ads

Responsive Ads Here

WALEVI,WAZURURAJI NA WAKAA VIJIWENI WILAYANI CHEMBA WAANDALIWA SHAMBA LA EKARI 30.

Na: Calvin Edward Gwabara
Chemba - Dodoma

Mkuu wa wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma Mhe. Simon Odunga ameagiza kukamatwa wazururaji,wakaa vijiweni na walevi wakati wa kazi na kuwapeleka shambani wakafanye kazi za kilimo kwenye shamba la ekari 30 ambalo amemuagiza Mkurugenzi wa wilaya kuliandaa mara moja ili kuhakikisha watu hao badala ya kufungwa watumike kwenye kuzalisha mali.
Mkuu wa wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma Mhe. Simon Odunga akizungumza mara baada ya kupokea mbegu bora za mahindi na Mbolea kutoka COSTECH


Kauli hiyo aliitoa wakati akipokea mbegu za Mahindi yanayostahimili ukame wa wastani na mbolea kutoka tume ya taifa ya sayansi na teknolojia kwaajili ya kuanzisha mashamba darasa kwenye vijiji vya kata mbalimbali yenye lengo la kuwafundisha wakulima umuhimu wa matumizi ya mbinu bra za kilimo ili kuongeza tija.‘’ Wakati wa kazi ni kazi sitaki kuona watu wanakaa vijiweni,kunywa pombe asubuhi na kuzurura mitaani wakati wengine wapo kazini naomba OCD nikamtie watu wa aina hiyo wooote  niwekee rumande alafu mimi nitakuwa nakuja kuwachukua nawapeleka shambani wakafanye kazi kwa masaa nane baada ya hapo tunawaachia waondoke zao kasha tunakamata wengine” Alisistiza Mhe. Odunga.

‘’Shamba darasa hili lililowekwa hapa shuleni naomba lisihudumiwe na wanafunzi mimi nitaleta watu hawa pia kuja kulihudunia kila siku ili muwaache wanafunzi wetu wasome maana tunao watu wengi wasio na kazi huko mitaani, wale walevi wooote waletwe shambani pombe zao zitawaishia shambani” Aliongeza Odunga.
Dkt. Nicholous Nyange akizungumza na wakulima mbele ya viongozi wa wilaya namna ya kutumia teknolojia ya mbegu,Upandaji wa nafasi na matumizi ya mbolea ili kuongeza uzalishaji wakati wa uzinduzi wa shamba darasa kwenye kijiji cha Kidoka wilayani Chemba


Akipokea mbegu hizo kwaajili ya kupanda kwenye wilaya yake na kuzindua upandaji wa shamba darasa la kwanza Mkuu huyo wa wilaya ameishukuru serikali kupitia COSTECH na Vituo vya utafiti kwa kufanya kazi kubwa ya kuwapelekea mbegu hizo bora za mahindi ambazo zinavumilia ukame na kusema kuwa zimekuja kwenye mkoa husika ambao mvua zake ni kidogo kila mwaka.

Aliongeza kuwa wananchi wa wilaya ya Chemba zao lao kubwa ni mahindi lakini linawaangusha kila mwaka kutokana na uhaba wa mvua lakini kupitia mbegu hizo bora zitasaidia kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo kwa wananchi huku akisisitiza maafisa ugani kusimamia vyema mashamba darasa hayo ili yaweze kuleta tija iliyokusudiwa na kuwafanya wakulima waige mbinu hizo bora za kilimo zinzofundishwa kwenye mashamba hayo.

Akieleza malengo ya zoezi hilo Mtafiti kutoka COSTECH Dkt. Beatrice Lyimo alisema kuwa zoezi hilo ni utekelezaji wa majukumu ya msingi ya COSTECH ya kuhakikisha kuwa teknolojia nzuri zinazotafitiwa na watafiti mbalimbali hapa nchini zinawafikia walengwa katika sekta mbalimbali ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na watu wengine.

Mtafiti kutoka COSTECH Dkt. Beatrice Lyimo (wa kwanza kushoto) akieleza lengo la mashamba darasa hayo

Aliongeza kuwa katika wilaya hiyo wamepeleka teknolojia mbili ambazo ni Matumizi ya mbegu bora za kilimo kwa wakulima kwa kutumia mbegu hizo za WEMA 2109 zinazovumilia ukame wa wastani,Matumizi ya mbolea za kupandia na kukuzia pamoja na upandaji wa mahindi kwa nafasi na kwa kufuata mistari mbinu ambazo wakulima wengi hawazizingatii na hivyo kuchangia kupata mavuno duni kila mwaka.

“Tunaamini mbinu hizi tunazozitumia hapa zitasaidia sana wakulima kuja kujifunza na kuona zinavyofanya kazi na umuhimu wake katika kuzalisha kwa tija hivyo mashamba haya yatumike kujifunza wakulima wote kwenye kila kijiji na hatimae mwishoni wkati wa mavuno wakulima waone mazao yatakayopatikana wakilinganisha nay ale waliyopata kwenye mashamba yao yasiyotumia mbinu hizi” Alisema Dkt. Lyimo.

Kwa upande wake Selemani Muna ambaye ni mkulima katika kijiji cha Kidoka wilayani Chemba aliwashukuru COSTECH na OFAB kwa kuona umuhimu wa kuwaletea mashamba darasa hayo na kusema kuwa wamekuwa wakilima mahindi sana lakini ni vigumu sana kupata magunia matano katika ekari moja kwani mtu analima ekari 30 anapata dunia 10 au 15.

Alisema kuwa wamezoea kulima bila kutumia mbolea,hawatumiii mbegu bora za madukani kila mwaka na huwa hawapandi kwa mistari bali hulifukuza trekta kwa nyuma wakati likilima na wao wanamwaga mbegu na likirudi upande wa pili linafunika mbegu wakati linalima hali ambayo imewafanya watumie mbegu nyingi na kupoteza eneo la shamba.

“Mimi nimekuwa nikilima ekari 25 na Napata magunia ya mahindi 20 lakini kwa sasa nakwenda kulima ekari tano tuu kwa kutumia mbinu hizi badala ya kupoteza nguvu na gharama kuwa kila mwaka na kupata mavuno ambayo ningeyapata kwenye ekari moja tu” Alisema Muna.
Mkuu wa wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma Mhe. Simon Odunga akizindua upandaji wa shamba darasa la kwanza kwenye wilaya yake.


Akizungumza na wakulima hao katika shamba darasa la shule ya msingi Kidoka kata ya Kidoka Mtafiti aliyebobea kwenye tafiti za bioteknolojia na zao la mahindi Dkt. Nicholous Nyange alisema kuwa wakulima wengi wanakosa mavuno ya kutosha kwa kutotumia mbinu bora za kilimo na badala yake wanalima mashamba makubwa na kupoteza nguvu na mali bila mafanikio.

Mbinu hizi zikitumiaka zitasaidia sana kuongeza uzalishaji kwa wakulima kwani kwa sasa makulima wa Dodoma anayelima ekari sita anapata gunia 30 wakati mkulima anayelima kitaalamu kwa kutumia mbegu bora na kufuata kanuni zingine za kilimo anaweza kupata gunia 30 hadi 35 katika ekari moja.

“Tunataka wakulima wetu mbadilike muachane na kilimo cha mazoea na mfuate kilimo cha kisasa ambacho mtalima mashamba madogo na kupata mavuno makubwa badala ya kulima mashamba makubwa ambayo hamuwezi kuyahumia na kupata mavuno kidogo”Alisema Dkt. Nyange.

No comments