Header Ads

Responsive Ads Here

WAKULIMA WILAYANI MASASI WAIOMBA COSTECH NA OFAB KUSAIDIA KUKABILIANA NA VIWAVIJESHI

 Mkurugenzi wa Sayansi ya Uhai kutoka COSTECH, Profesa Mohammed Sheikh, akiangalia mahindi yaliyoshambuliwa na viwavjijeshi katika moja ya shamba lililopo Kijiji cha Namajani wilayani Masasi mkoani Mtwara jana.
 Ofisa Mazao kutoka Halmshauri ya Wilaya ya Masasi DC, Basil Mdage, akitoa maelezo kwa wakulima wa Kijiji cha Chingulungulu kilichopo Kata ya Namatutu Tarafa ya Lisekese wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mahindi aina ya Wema WE2109 uliofanyika kijijini hapo jana.
 Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Ali Linjenje, akionesha jinsi ya upandaji wa mahindi hayo kwa wakulima wa Kijiji cha Chingulungulu.
 Mkurugenzi wa Sayansi ya Uhai kutoka COSTECH, Profesa Mohammed Sheikh, akipanda mbegu ya mahindi aina ya Wema wakati akizindua shamba darasa la mbegu hiyo katika Kijiji cha Chingulungulu.
 Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Ali Linjenje, akiwaelezea wakulima wa Kijiji cha Namainga jinsi ya upandaji wa mbegu ya mahindi aina ya Wema.
 Bakari Chabanda,  mkulima wa Kijiji cha Namainga akielezea changamoto ya viwavijeshi.
 Wanakijiji wa Kijiji cha Namainga wakipokea mbegu ya mahindi aina ya Wema na mbolea ya kupandia.
 Mkulima Sarafina Adinani akielezea changamoto ya wadudu wanaoshambulia mahindi. Kulia ni Mwanahabari Calvin Gwabara kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro.
Mkulima Dominich Emmanuel akizungumzia wadudu waharibifu wa mahindi.

Na Dotto Mwaibale, Masasi Mtwara

WAKULIMA wa Vijiji vya Namainga na Namajani katika Wilaya ya Masasi wameiomba Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) kuwaondolea changamoto ya viwavijeshi vinavyo shambulia mahindi yao yaliyopo mashambani.

Ombi hilo walilitoa jana baada ya kuzuia msafara wa watafiti wa kilimo kutoka COSTECH na OFAB wakati wakiwa katika uzinduzi wa mashamba darasa ya mbegu ya mahindi aina ya Wema WE2109 yanayostahimili ukame uliofanyika katika vijiji hivyo.

Akizungumzia changamoto hiyo Bakari Chabanda mkulima wa Kijiji cha Namainga alisema wadudu hao wamekuwa tishio sana katika mashamba yao na walianza kuonekana tangu msimu wa kilimo wa mwaka jana ambapo na mwaka huu wameibuka tena.

"Wadudu hawa ni changamoto kubwa kwetu wakulima kwani wanatafuna majani ya mahindi hivyo kuhufanya mmea ushindwe kukua" alisema Chabanda.

Mkulima wa Kijiji cha Kijiji cha Namajani, Sarafina Adinani alisema wadudu hao wamekuwa wakiwakatisha tamaa kwani wanashambulia mimea hasa nyakati za usiku na kuwa hali hiyo ilianza mwaka jana.

Mkulima Dominick Emanuel wa Kijiji cha Namajani aliomba COSTECH na OFAB kusaidia kupatikana kwa dawa ya kuwaangamiza wadudu hao ili waweze kufanya kilimo chenye tija.

"Tunawaomba wataalamu wa kilimo hasa ninyi watafiti mtusaidie kupata dawa ya uhakika ya kukabiliana na wadudu hawa ambao hata tukipuliza dawa kwenye mahindi yetu wamekuwa hawafi" alisema Emmanuel.

Akizungumza na wakulima hao Mkurugenzi wa Sayansi ya Uhai kutoka COSTECH, Profesa Mohammed Sheikh alisema COSTECH inaifahamu changamoto hiyo na kuna jitihada ambazo zinafanyika za kupata dawa.

"Changamoto hii inafahamika na kunajitihada zinafanyika za kupata dawa ya kukabiliana na wadudu hao kwani hata kwa upande wetu itakuwa haina maana ya kuanzisha mashamba darasa ya mahindi bora alafu yakaishia kushambuliwa na wadudu hao" alisema Sheikh.

Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Ali Linjenje alisema dawa ya kukabiliana na wadudu hao ipo baada ya kufanyiwa utafiti wa kuzichanganya dawa aina tatu lakini kubwa zaidi ni kubaini ni aina gani ya wadudu hao.

"Changamoto hii inafahamika na sisi kama mkoa tunaifanyia kazi tunachofanya hivi sasa ni kubaini aina ya wadudu hao" alisema Linjenje.

COSTECH kupitia OFAB wapo mkoani Mtwara kuanzisha mashamba darasa ya mahindi aina ya Wema yanayostahimili ukame ambapo kwa wilaya ya Mtwara vijiji vya Kilombero na Mnawene vimeanzisha mashamba hayo na sasa yanaendelea kuanzishwa katika Wilaya ya Masasi na baadae mkoani Lindi.

No comments