Header Ads

Responsive Ads Here

MTWARA WATAKIWA KUCHANGAMKIA KILIMO CHA MAHINDI


Na Dotto Mwaibale, Mtwara

MKOA wa Mtwara umetakiwa kuchangamkia kilimo cha mahindi kwa ajili ya biashara na chakula badala ya kutegemea zao la korosho pekee.

Mwito huo umetolewa mjini hapa leo na Mratibu wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Philbert Nyinondi wakati akizungumza na Kaimu Katibu Tawala Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Francis Mkuti alipofika ofisi hapo na timu ya watafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na waandishi wa habari waliopo katika ziara ya upandaji wa mbegu bora za mahindi aina ya Wema yanayostahimili ukame katika mashamba darasa mkoani humo.

Alisema wakulima mkoani humo waache kutegemea zao moja la korosho badala yake walime  mahindi ambayo yatawasaidia kwa chakula na biashara.

"Msitegemee zao moja tu la korosho limeni na mahindi ndio maana COSTECH kupitia OFAB tumewaletea mbegu hii inayostahimili ukame ili muweze kunufaika na kilimo cha mahindi" alisema Nyinondi

Nyinondi alisema wamekuwa wakilima kwa wingi zao la korosho na wakishaiuza  nusu ya fedha hizo zimekuwa zikitumika kwenda kununulia chakula lakini kama wakiamua kulima mahindi itawasaidia kwa kuwa na chakula na fedha hizo zinazotumika kununualia chakula zikafanya kazi zingine.

Alisema mbegu hiyo ya mahindi iliyofanyiwa utafiti inavumilia ukame na ndio maana wameona waipeleke mkoani humo ipandwe katika mashamba darasa na matokeo yake yakiwa mazuri itasambazwa katika maeneo mengine ambapo mkoa huo utapatiwa kilo 150. 

Kaimu Katibu Tawala Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Francis Mkuti (pichani) alisema mbegu hiyo ya mahindi itakuwa ni mkombozi kwa wakulima wa wilaya hiyo ambapo alisema jambo la muhimu ni uhamasishaji wa kilimo hicho kwani wakulima wa mkoa huo wamezoea zaidi kilimo cha korosho.

Alisema mkoa huo una mabonde yenye rutuba ambayo yanaweza kuotesha mahindi na mazao mengine kama mpunga na mihogo lakini changamoto ni elimu ya kilimo hicho na ni wakati gani kinatakiwa kufanyika.

Mkuti alitoa angalizo kuwa ili kupata mazao yenye toja kilimo cha mahindi kisifanyike kwenye mashamba ya mikorosho bali kitengewe mashamba yake.

Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Mtwara, Omari Kipanga aliishukuru COSTECH na OFAB kwa kupeleka mbegu hiyo mkoani humo na kuahidi kutoa ushirikiano katika kufanikisha mashamba darasa hayo. 

Baada ya kukamilika kwa zoezi la upandaji wa mbegu hiyo bora ya mahindi katika mashamba darasa mkoani Mtwara zoezi hilo litaendelea katika Mkoa wa Lindi.

No comments