Header Ads

Responsive Ads Here

MTWARA WAIPONGEZA COSTECH NA OFAB KUPELEKA MBEGU BORA YA MAHINDI YA WEMA 2109

  Mkurugenzi wa Sayansi ya Uhai kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Profesa Mohammed Sheikh, akipanda mbegu ya mahindi aina ya Wema katika uzinduzi wa shamba darasa uliofanyika leo katika Kijiji cha Kilombero Kata ya Muhurunga, Mtwara vijijini.

 Wananchi wa Kijiji cha Kilombero wakishiriki kupanda mbegu hiyo katika shamba darasa

Shughuli za upandaji zikiendelea
 Mtafiti kutoka COSTECH, Dk.Beatrice Lyimo akizungumza katika uzinduzi wa upandaji wa mbegu hizo katika Kijiji cha Mnawene. Kulia ni Mkurugenzi wa Sayansi ya Uhai kutoka COSTECH, Profesa Mohammed Sheikh.
 Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara mjini ambaye ni Kaimu Katibu Tawala Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Francis Mkuti akizindua upandaji wa mbegu hizo katika Kijiji cha Mnawene.
 Mkurugenzi wa Sayansi ya Uhai kutoka COSTECH, Profesa Mohammed Sheikh, akimkabidhi mbegu hizo,  Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara mjini ambaye ni Kaimu Katibu Tawala Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Francis Mkuti
 Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Ali Linjenje, akizungumzia ubora wa mbegu hizo.
Mkulima wa Kijiji cha Kilombero katika Kata ya Muhurunga, Fakhi Kipangulo, akizungumzia changamoto waliyo kuwa nayo kuhusu kilimo kisichokuwa na tija.

Na Dotto Mwaibale, Mtwara

MKOA wa  Mtwara umeipongeza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) kwa kuwapelekea mbegu bora ya mahindi aina ya wema WE2109 ambayo itapandwa katika mashamba darasa na kusambazwa kwa wakulima wengine katika mkoa huo.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara mjini ambaye ni Kaimu Katibu Tawala Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Francis Mkuti wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mbegu hiyo ya mahindi yanayostahimili ukame uliofanyika katika, vijiji vya Kilombero na Mnawene kilichopo Kata ya Ziwani wilaya ya Mtwara Vijijini.

"Kwa niaba ya mkuu wa wilaya napenda kuishukuru COSTECH kwa kutuletea mbegu hizi katika wilaya yetu hasa baada ya kuona changamoto tunayokabiliwana nayo ya kilimo za zao moja la korosho " alisema Mkuti.

Mkuti alisema msaada huo hautapotea bure kwani watahakikisha wanayahudumia vizuri mashamba darasa hayo kupitia maofisa ugani na wao watafanya ziara za mara kwa mara ya kutembelea yalipo mashamba hayo kuona maendeleo yake.

Mkulima wa Kijiji cha Kilombero katika Kata ya Muhurunga, Fakhi Kipangulo alisema mbegu hiyo waliyoletewa itakuwa mkombozi wao kwani kwa muda mrefu wamekuwa na changamoto ya kupata mazao kiduchu kutokana na kilimo walichokuwa wakikifanya kutokuwa cha tija.

"Tumefarijika sana kuletewa mbegu hii kwani sasa tutainuka kiuchumi na kupata chakula cha kutosha kwani hapo awali tulikuwa tukilima ekari mbili hadi tatu lakini tulikuwa tukipata mahindi viroba viwili au vitatu na hiyo ilitokana na kuchanganganya mazao zaidi ya matatu katika shamba la mahindi.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH, Mkurugenzi wa Sayansi ya Uhai kutoka COSTECH, Profesa Mohammed Sheikh alisema COSTECH kupitia OFAB wanaendesha mradi huo ili kuhakikisha matokeo mazuri ya kazi za tafiti yanawafikia wakulima.

Alisema COSTECH ndio mshauri mkubwa wa serikali katika masuala ya kilimo cha kitafiti hivyo wanakila sababu ya kuhakikisha tafiti zinazofanyika nchini zikiwafikia walengwa ili waweze kufanya vizuri katika kilimo.

Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,Ali Linjenje alisema mkoa huo umepata bahati kubwa kwa kupelekewa mbegu hizo ambapo kwa mkoa mzima wamepata kilo 500 na kwa wilaya ya Mtwara vijijini wamepata kilo 150.

Alisema mkulima akitumia mbegu hizo na kufuata kanuni za kilimo zinazoelekezwa katika ekari moja atapata magunia ya mahindi yasiyo pungua 30 na hata kama kutakuwa na changamoto zozote kama ukame na wadudu atapata magunia sio kuanzia 10 hadi 15.

"Tuna bahati kubwa kuletewa mradi huu katika mkoa wetu hivyo tusiwaangushe hawa wenzetu tuwe wa mfano tuyatunze haya mashamba ili tupate matokeo mazuri" alisema Linjenje.

Mashamba darasa ya mbegu bora ya mahindi aina ya Wema yameanzishwa katika mkoa huo baada ya COSTECH na OFAB kutoa mafunzo kwa wataalamu wa kilimo mwaka jana yakiwa na lengo la kuwasaidia wakulima kuzalisha mazao ya chakula kama mahindi badala ya kutegemea zao la korosho pekee na kuachana na kilimo kisicho na tija.


No comments