Header Ads

Responsive Ads Here

MPINA AKAMATA MAROBOTA 1152 YA NYAVU HARAMU MWANZA NA SINGIDA ZENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 894.Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina(mwenye kofia) akiwa na Kiongozi wa Operesheni ya maalum ya kudhibiti uvuvi haramu katika ukanda wa Ziwa Victoria, Shafii Ramadhani Kiteri wakikagua shehena ya marobota 600 ya nyavu haramu zenye thamani ya shilingi milioni mia tano inayomilikiwa na Meshaki Chacha jijini Mwanza leo. Nyavu hizo zimetaifishwa na nyingine kuteketezwa na mmliki akitakiwa kulipa faini ya shilingi milioni hamsini ndani ya masaa 24.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (mwenye miwani na kofia )akisikiliza jambo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ukerewe, Frank Bahati (kushoto) wakiwa kwenye boti ya doria kutoka katika kijiji Kakukuru wakielekea kwenye kambi ya uvuvi ya Kisiwa cha Galinzila ambapo Mhe.Waziri alifanya mkutano na wavuvi . Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Estomiah Chang’a. (Na John Mapepele)
Mmliki wa ghala lenye shehena ya marobota 600 ya nyavu haramu za kuvulia samaki zisizoruhusiwa kisheria zenye thamani ya shilingi milioni mia tano, Meshaki Chacha akihojiwa na Mwandishi wa Habari wa ITV baada kikosi kazi kilichoundwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina(mwenye kofia) kuvamia ghala lake lililopo jijini Mwanza leo. Ametakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 50 ndani ya masaa 24 leo. 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (mwenye miwani)akikagua nyavu haramu za kuvulia samaki katika kijiji cha Kakukuru wilayani Ukerewe ambapo alichoma moto nyavu haramu za zenye thamani ya shilingi bilioni mbili. Kulia ni Lameki Mongo, Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kushoto ni Abbakary Murshidi, Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Ukerewe (Na John Mapepele) Aapa kutokomeza uvuvi haramu nchini
Asema imebaki 3% tu ya Sangara wanaokubalika kuvuliwa katika ziwa Victoria

Na John Mapepele

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Joelson Mpina amekamata marobota 1152 ya aina mbalimbali za nyavu haramu zisizoruhusiwa kisheria kutumika kuvulia samaki zenye thamani ya shilingi milioni 894 jijini Mwanza na Singida ambapo baadhi ya nyavu hizo zimetaifishwa na nyingine kuteketezwa na wamiliki wakitakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 120 ndani ya masaa 24 kwa makosa ya kufanya biashara ya nyavu hizo kinyume cha sheria.

Akiongea na Vyombo vya Habari jijini Mwanza katika ghala la nyavu la Meshack Chacha mara baada ya kukamata shehena ya marobota 600 ya nyavu haramu kwenye ghala lake, Mhe. Mpina alisema nyavu haramu 294 kati ya 894 zilikamatwa na kikosi kazi maalum cha kudhibiti uvuvi haramu katika kanda ya Ziwa Victoria alichokiunda hivi karibuni wakati mmoja wa wafanyabiashara hao Masagati Majani alijaribu kutorosha vyavu hizo kwa kutumia gari aina ya Scania lenye namba za usajili T.452 BBS kutoka Mwanza kuelekea Dar es Salaam.

Gari hilo lipo katika kituo cha polisi cha Singida kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria ambapo kulingana na sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003, imetoa mamlaka kwa watendaji wa Serikali kutaifisha mali zote zilitumika katika uvuvi haramu kupitia kifungu cha 37(a) (ii) na (iii)

Aliwataja wamiliki wengine ambao walikamatwa kutokana na kujihusisha na biashara haramu ya uagizaji na uuzaji wa vyavu zisizoruhusiwa kisheria kuwa ni Josia Jonam Obielo, Jeremiah Asam na Dastun Venant ambapo alisema Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wote wanao agiza na kuuza zana haramu za uvuvi wanakamatwa na sheria kali zinachukuliwa ili kudhibiti uvuvi haramu nchini.

“Niliapa kusimamia ulinzi wa raslimali za uvuvi nchini hivyo nitahakikisha operesheni hii inakuwa ya kudumu katika kupambana na uvuvi haramu hadi uvuvi haramu utakapokwisha” alisisitiza Mpina

Katika hatua nyingine Waziri Mpina amelaani kitendo Kiwanda cha Sunflag cha mkoani Arusha kwa kuendelea kufadhili uvuvi haramu nchini kutengeneza na kuuza vyavu za kuvulia samaki zisizoruhusiwa kisheria wakati Serikali imekuwa ikisisitiza viwanda vyote nchini kuacha tabia ya kufadhili uvuvi haramu kwa kutengeneza zana haramu za uvuvi.

Waziri Mpina ameagiza watalam kwenda mara moja katika kiwanda hicho kuchunguza ukweli wa jambo hilo ili sheria zichukue mkondo wake.Hivi karibuni Waziri Mpina aliunda Kikosi maalum cha kupambana na uvuvi haramu ambapo katika kipindi kisichozidi siku kumi na nne zaidi ya zana haramu za uvuvi ikiwa ni pamoja na nyavu zenye jumla ya bilioni tatu zimeteketezwa katika kanda ya ziwa Victoria peke yake huku viwanda vitano vya kusindika samaki vilivyopo jijini Mwanza vikitakiwa kulipa jumla ya shilingi milioni 180 ndani ya masaa 24.

Viwanda hivyo vilitozwa faini hiyo kutokana na kuendelea kuwa wafadhili wakuu wa uvuvi haramu kwa kununua na kuchakata samaki aina Sangara wachanga na wazazi kinyume cha Sheria ya Uvuvi.

Waziri Mpina alisema Sheria ya Uvuvi namba 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 kifungu cha 90(1) inataka samaki wanaovuliwa waandaliwe katika mazingira yanayokidhi vigezo vya usalama kwa mlaji na kwamba ni kosa kisheria kuwavua au kuchakata samaki aina ya Sangara walio chini ya sentimeta 50 kwa kuwa ni wachanga na sentimita 25kwa Samaki aina ya Sato. Pia sentimita 85 kwa Sangara kwa kuwa ni wazazi wanaotakiwa kundelea kuzaa.

Waziri Mpina alisema samaki aina ya Sangara kwenye Ziwa Victoria wapo katika hatari ya kutoweka kabisa katika kipindi cha miaka miwili endapo hali ya uvuvi haramu ukiachwa uendelee bila kuchukua hatua za haraka na madhubuti kudhibiti janga hili.

Alisema kulingana na utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Samaki Tanzania (TAFIRI) 2017 unaonesha kuwa samaki wachanga waliochini ya sentimita 50 wasioruhusiwa kuvuliwa ni asilimia 96.6 , samaki wazazi walio zaidi ya sentimita 85 ambao pia hawarusiwi kuvuliwa ni asilimia 0.4 na samaki wa sentimita 50 mpaka 85 ambao ndio wanafaa kuvuliwa ni asilimia 3 tu hivyo juhudi za pamoja za wadau wote wa sekta ya uvuvi zinahitajika ili kurejesha raslimali ya uvuvi katika Ziwa Victoria kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.

No comments