Header Ads

Responsive Ads Here

JUMIA TRAVEL YAZINDUA AWAMU YA PILI YA TUNZO ZA USAFIRI AFRIKA

 Kampuni inayojihusisha na huduma za malazi na usafiri kwa njia ya mtandao barani Afrika, Jumia Travel, inatarajia kufanya tunzo za usafiri kwa awamu ya pili Januari 25. Sherehe hizo za awamu ya mwaka huu wa 2018, zitafanyika sambamba kwenye nchi nyingine 8 Afrika ambazo ni: Algeria, Cameroon, Ivory Coast, Ghana, Nigeria, Uganda, Senegal na Tanzania. Kwa nchini Tanzania zitafanyika tarehe 25 Januari, 2018. 

Akizungumzia juu ya umuhimu wa tunzo hizi kwenye sekta ya utalii nchini, Meneja Mkazi wa Jumia Travel Tanzania, Xavier Gerniers amebainisha kuwa, “Tunzo hizi zinalenga katika kukuza sekta ya utalii Tanzania, lakini pia kuona haja ya kuwahimiza wadau kwenye biashara ya hoteli kuboresha huduma zao pamoja na kutangaza vivutio vilivyopo kwenye maeneo yao.” 

“Kutakuwa na vipengele saba ambavyo vitatolewa tunzo vikiwemo: Hoteli Bora iliyopendekezwa na wateja mwaka 2017, Shirika Bora la Ndege lililopendekezwa na wateja mwaka 2017, Tovuti Bora iliyotangaza vivutio vya kitalii mwaka 2017, Hoteli iliyofanya huduma zake kupitia Jumia Travel mwaka 2017, Hoteli Bora iliyopendekezwa zaidi na wasafiri mwaka 2017, Hoteli Bora ya Kustarehe mwaka 2017, na Hoteli Bora kwa shughuli za kibiashara mwaka 2017,” aliongezea. 

Jopo la majaji, likiwa limeundwa na wataalamu wa hali ya juu kwenye sekta ya utalii nchini, limechaguliwa ili kutathmini hoteli zilizochaguliwa na kisha kuamua washindi. Maamuzi ya majaji yatachangia 50% ya matokeo, huku 50% iliyobakia itatoka kwa hadhira kupitia mchakato wa upigaji kura unaoendelea. 

“Tumeona itakuwa ni vema kuwashirikisha moja kwa moja wadau na wateja kwenye sekta ya utalii nchini kwenye tunzo za awamu hii. Hivyo basi, tumewapa fursa sawa kutoa maoni yao juu ya waliochaguliwa na wanaostahili kuzawadiwa kwenye vipengele tofauti vilivyoainishwa,” alifafanua na kumalizia Meneja Mkazi huyo wa Jumia Travel nchini, “Tunaamini kwamba zoezi hili litaongeza tija kwenye mchakato mzima wa utoaji wa tunzo hizi na kulifanya zoezi kuwa shirikishi zaidi. Wakati zikiwa zimebakia siku chache kabla ya kilele cha sherehe hizi, watanzania wanaweza kuendelea kuzipigia kura hoteli na shirika la ndege kwa kufuatilia kurasa zetu za mitandao ya kijamii, ambapo pia watajipatia fursa ya kujishindia muda wa kulala bure kwenye hoteli ya kifahari.” 

Washindi wa tunzo hizi watazawadiwa kwenye hafla fupi itakayofanyika tarehe 25 ya mwezi Januari, 2018, kwenye hoteli ya Harbour View Suites jijini Dar es Salaam, sambamba na miji ya Lagos, Algiers, Dakar, Abidjan, Accra, Douala, na Kampala. 

Akielezea jitihada za kukuza sekta ya utalii Afrika, kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Jumia Travel barani Afrika, Bw. Joe Falter aliongezea kwa kusema kuwa, “kwa kuandaa tunzo za usafiri Afrika, dhumuni letu kuu sio tu kuwatambua na kuwazawadia wadau wa sekta ya utalii wa ndani kwa kuonyesha weledi mkubwa, lakini pia tunataka kuweka viwango ambavyo vitakubalika kwenye sekta ya utalii barani Afrika.” 

Unaweza kufuatilia mijadala mbalimbali kuhusu tunzo hizi kwenye mitandao ya kijamii kupitia: #JumiaTravelAwards2018

No comments