Header Ads

Responsive Ads Here

AGAPE YAKUTANA NA WANAFUNZI NA WALIMU KATA YA DIDIA KUZUIA MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI SHINYANGA

Shirika lisilo la kiserikali la Agape AIDS Control Programme (AACP) la Mjini Shinyanga limekutana na wanafunzi na walimu wa shule za msingi Didia,Mwanono,Bugisi,Mwamalulu ,Bukumbi na shule ya Sekondari Didia zilizopo katika kata ya Didia halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kupanga mikakati ya kuzuia ndoa na mimba za utotoni.


Kikao hicho kimefanyika leo Ijumaa Januari 19,2018 katika shule ya msingi Didia na kuhudhuriwa na baadhi ya wanafunzi walioambatana na walimu wao kutoka shule hizo.

Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda alisema lengo la kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Didia Felister Meli,Kaimu Mtendaji wa kata William Nkuya ni kupanga mikakati ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni ili wanafunzi waweze kumaliza masomo yao vizuri.

Alisema wanafunzi waliohudhuria kikao hicho watakuwa viongozi wa wanafunzi wengine katika kupambana na ndoa na mimba za utotoni ambapo wataunda klabu kwa ajili ya masuala hayo zitakazopewa jina la “Tuseme Klabu”.

“Hatutaki kuona mwanafunzi anakatiza masomo kwa sababu ya kupewa mimba ama kuolewa, ni wajibu wetu wanafunzi,walimu,serikali na wadau wote tushirikiane kupaza sauti ili watoto wetu watimize ndoto zao”,alieleza Isabuda.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE John Myola alisema bado jitihada kubwa zinatakiwa kufanyika ili kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika jamii kwani baadhi ya matukio yamekuwa yakifanywa na ndugu wa karibu huku kesi za watoto zikifanywa dili na baadhi ya watendaji wasio waaminifu.

Kwa upande wake Secilia Kiza kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga aliwataka wanafunzi kutofumbia macho vitendo vya ukatili na watoe taarifa katika vyombo vinavyotakiwa.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE,John Myola akizungumza katika kikao chao na wanafunzi na walimu kutoka shule za msingi Didia,Mwanono,Bugisi,Mwamalulu ,Bukumbi na shule ya Sekondari Didia zilizopo katika kata ya Didia halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kilichofanyika katika shule ya msingi Didia leo Ijumaa Januari 19,2018 - Picha zote na Kadama Malunde
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGAPE John Myola akizungumza katika kikao hicho ambapo aliwataka wanafunzi kufichua vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na walimu kuwa wadadisi wa mambo mbalimbali wanayoambiwa na wanafunzi wao.
Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda akielezea lengo la kukutana na wanafunzi na walimu kwa ajili ya kujadili namna ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni
Meneja Mradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka shirika la AGAPE,Mustapha Isabuda akionesha picha ya watoto waliosaidiwa na shirika la AGAPE baada ya watoto hao kukatishwa masomo kwa kupewa ujauzito na wengine kuolewa wakiwa na umri mdogo
Secilia Kiza kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga akizungumza katika kikao hicho ambapo aliwasisitiza wanafunzi,walimu na jamii kwa ujumla kutoa taarifa pale wanapoona kuna matukio ya ukatili dhidi ya watoto.
Mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Didia,Hellena Mussa akizungumza katika kikao hicho ambapo alisema wataenda kutoa elimu ya namna ya kuzuia mimba na ndoa za utotoni
Picha ya pamoja washiriki wa kikao hicho.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments