Header Ads

Responsive Ads Here

POLISI TANGA YAWATAHADHARISHA WANANCHI KUELEKEA SIKUKUU


Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga,Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Edward Bukombe akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na matukio yaliyotokea kwa kipindi cha mwaka mzima ambapo alisema Jumla ya Silaha 14 za moto zilikamatwa kulia ni RCO wa mkoa wa Tanga,Justine Masejo 

JESHI la polisi mkoani Tanga, limewahadharisha wananchi kuelekea katika msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani kama ulipuaji baruti na fataki ikiwemo kuchoma moto matairi barabarani, kwa yeyote atakayefanya hivyo atachukulia hatua za kisheri. 

Kamanda mpya wa mkoa huo, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Edward Bukombe, alisema kwamba jeshi hilo linapiga marufuku kwa mtu yeyote kulipua au kusababisha milipuko ikiwemo baruti, fataki na Eksozi za magari, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria namba 13 ya sheria ya milipuko. 

“Hivyo wakazi wa mkoa wa Tanga, ni marufuku kuchoma matairi hovyo na kulipua baruti bila kibali, kufanya hivyo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakae kiuka agizo hili,” alisema RPC Bukombe. 

Alisema uzoefu unaonesha kuwa siku za sikukuu watu wengi hujisahau kujiwekea ulinzi ikiwemo kuwaangalia watoto hivyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wazazi kuhakikisha wanachukua hatua za kuwalinda watoto pamoja na nyumba zao ili wahalifu wasitumie mwanya huyo kufanya uhalifu wa kuvunja au watoto kupotea mitaani. 

Kamanda Bukombe alisema kwamba jeshi hilo limejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanasherehekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu bali aliwakumbusha kuzingatia taratibu za kumbi za burudani kufungwa nyakati za saa 6:00 usiku na hata ibada za mkesha wa Krismasi na Mwaka mpya zimalizike muda huo. 

Katika hatua nyingine Kamanda huyo wa polisi alisema mwenendo wa uhalifu mkoani humo, katika kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka 2017,  umeendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu ma hakuna matukio yanayotishia usalama kwa wananchi baada ya kuyadhibiti kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola. 

Hata hivyo, alisema kwamba katika kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka huu, katika misako waliyoiendesha na operesheni mbalimbali waliweza kukamata wahalifu waliofanya matukio mbalimbali ambapo kesi za bangi zilikuwa 237 kwa bangi yenye uzito wa kilogramu 76.1 na mirungi kesi zilikuwa 37 na uzito wa mirungi ilikuwa kilogramu 5,396.740. 

Kwa upande wa wahamiaji haramu jeshi hilo walikamata wahamiaji haramu wapatao 224 kati ya hao Wasomali walikuwa 55 na Waethiopia walikuwa 149 na Wakenya walikuwa 20 ambao wote walifikishwa katika vyombo vya sheria. 

Kamanda huyo pia alisema kuwa katika kudhibiti ujambazi na unyang’anyi wa kutumia silaha, jeshi hilo katika kipindi hicho lilifanikiwa kukamata jumla ya silaha 14 za moto ambapo bastola zilikuwa 2, shortgun 3 na magobore yaliyotengenezwa kienyeji yalikuwa 9.
Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga,Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Edward Bukombe akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na matukio yaliyotokea kwa kipindi cha mwaka mzima ambapo alisema Jumla ya Silaha 14 za moto zilikamatwa, kushoto ni Afisa Mnadhimu wa Jeshi hilo Mkoani Tanga,Leonce na kulia ni RCO wa mkoa wa Tanga,Justine Masejo(Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha)
Sehemu ya waandishi wa habari wakichukua taarifa 

No comments