Header Ads

Responsive Ads Here

MIILI YA ASKARI 14 WA JWTZ YAAGWA

Serikali imetaka Umoja wa Mataifa (UN) kufanya uchunguzi wa kina na kwa haraka kubaini waliohusika katika shambulizi kwa askari wa Tanzania waliokuwa wakilinda amani Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).


Akizungumza wakati wa kuaga miili ya askari 14 waliofariki katika mapigano na waasi wa kikundi cha ADF nchini DRC, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inataka baada ya uchunguzi huo hatua zichukuliwe ili kutenda haki.


Miili ya askari hao imeagwa leo Alhamisi, Desemba 14,2017 katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa jijini Dar es Salaam.


“Serikali ya Tanzania inataka Umoja wa Mataifa ufanye uchunguzi wa kina, ulio wazi na wa ukweli kwa damu hizi za Watanzania zilizomwagika ili tujue na haki iweze kutendeka. Ni matumaini yetu kuwa Umoja wa Mataifa watafanya hivyo kwa haraka,” amesema.


Majaliwa ameishukuru Serikali ya DRC na UN kwa ushirikiano baada ya kutokea shambulizi hilo. Amewataka Watanzania waungane kuwaombea mashujaa hao na kuenzi mchango wao kwa Taifa.


Amesema Tanzania imekuwa ikishiriki ulinzi wa amani sehemu nyingi kama vile Lebanon, Darfur na DRC na maeneo yote wanapokuwepo askari wa Tanzania wanasifiwa kwa ufanisi wa kazi.


“Msiba huu ni wa Taifa lote na watu wote wenye kupenda amani, daima tutawakumbuka mashujaa wetu na kuendelea kuenzi na kujivunia kazi zao na mchango wao mkubwa kwa nchi yetu na duniani kwa jumla,” amesema.


Waziri Mkuu Majaliwa ameliambia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwamba, yaliyotokea DRC yasiwakatishe tamaa katika kutimiza wajibu wao nchini humo na kwingineko ambako wanatekeleza majukumu yao ya ulinzi wa amani.


Awali, akizungumza wakati wa kuaga miili ya askari hao, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo alisema askari hao waliuawa kwenye mapigano yaliyodumu kwa saa 13.


Amesema majeruhi wa shambulio hilo linalodaiwa kufanya na waasi wa ADF wanaendelea vizuri na wanapatiwa matibabu katika hospitali zilizopo Goma, Kinshasa na wengine wamepelekwa Uganda.


Shughuli ya kuaga miili ya mashujaa hao imehudhuriwa na viongozi kadhaa wakiwemo, Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mkewe Salma; wakuu wa majeshi wastaafu Robert Mboma, Mirisho Sarakikya na Davis Mwamunyange; Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda; mawaziri, wabunge na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa.


Miili ya askari hao ilirejeshwa nchini kwa ndege ya Umoja wa Mataifa Desemba 11,2017.


Jumapili Desemba 10, 2017 Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James Mwakibolwa alisema askari hao walivamiwa kambini na waasi wa ADF na mapigano yalidumu kwa takriban saa 13. Alisema askari 14 wa JWTZ waliuawa, 44 walijeruhiwa na wengine wawili hawajulikani walipo.


Taarifa iliyotolewa baadaye na jeshi ilisema askari mmoja amepatikana.


Mwakibolwa alisema tukio hilo lililotokea Desemba 7,2017 katika kambi ndogo iliyopo katika daraja la Mto Simulike, kaskazini mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu nchini DRC.


Chanzo- Mwananch

No comments