Header Ads

Responsive Ads Here

"BENKI YA AZANIA YAAZIMIA KUBORESHA SEKTA YA UMMA ILI KUKUZA UCHUMI"


Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

UONGOZI wa Benki ya Azania Limited umeridhika na namna serikali ilivyopokea mawazo ya wadau wa sekta binafsi katika mkutano walioshiriki kuuandaa mkoani Dodoma kwa lengo la kutoa fursa kwa wafanyabiashara kuishauri serikali katika masuala mbalimbali yahusuyo kodi.

Katika mkutano huo ulioongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango wafanyabiashara kutoka kampuni mbalimbali za binafsi walieleza changamoto wanazokumbana nazo na kushauri njia muafaka za kuondokana na changamoto hizo ili kuweka mazingira mazuri ya biashara nchini.

“Lengo letu la msingi kuwepo katika mkutano huu ni kutaka kuhakikisha sekta binafsi zinakuwa karibu na serikali ili kupatikane nafasi ya kuelezana yale yanayoonekana ni kikwazo katika uwekezaji, kama inavyofahamika kazi ya benki ni kutoa mikopo na kuwezesha kampuni kutimiza malengo yake na kumudu kulipa kodi,” alisema Bw Godwin Seiya.

Akizungumzia hali halisi ya kiuchumi nchini Bw Seiya alisema kodi ndiyo inayoendesha nchi hivyo hakuna namna ambayo serikali itaruhusu ukwepaji kodi lakini mbali ya hayo serikali imefungua milango ya majadiliano na kuwasikiliza wafanyabiashara mambo yanayowakwaza.

“Hii ni heshima kubwa tumepewa wafanyabiashara, katika mkutano huu kama alivyoeleza Waziri Mpango, ndipo ambapo sehemu ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha itatengenezwa kupitia mawazo yaliyotolewa na wajumbe,” alisema mhudhuriaji mmoja.

Akihutubia wajumbe katika mkutano huo wa siku moja, Waziri Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi na mwenyekiti alisema serikali haina tatizo na kubadili mfumo wa kodi kwa sababu kila siku wanatafuta namna nzuri ya kukusanya kodi bila kuwakwaza wafanyabiashara.

“Naomba niwaeleze kuwa hata serikali inafurahi kuwa na mikutano ya namna hii, kwa sababu tunatarajia tutapata mapendekezo yanayotekelezeka. Katika mazingira haya niliyoeleza ningependa kuona tunapata mfumo wa kodi utakaofungulia nguvu ya sekta binfsi,” alisema Dkt. Mpango.

Alisisitiza kuwa kwa sasa Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayoendelea ambayo yanajipanga kuwa na uchumi wa kati kwa kutegemea mapato ya ndani kwa sababu wahisani wamepunguza kutoa misaada na mikopo.

“Tukiamua kufanya kazi pamoja na kuweka nguvu zetu kwa kusikilizana changamoto na kupata majibu mazuri; hakuna kitakachotushinda. Katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/18 tuliingiza mambo mengi kutokana na ushauri wa sekta binafsi. Tutaendelea kufanya hivyo na hii ni ahadi ya serikali,” alisema Dkt. Mpango.

Kwa upande wake mwakilishi wa jumuiya ya wenye viwanda nchini (CTI) Dk. Samwel Nyantahe pamoja na mambo mengine, amesisitiza umuhimu wa serikali pamoja na jumuiya ya wafanyabiashara kuendelea kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta binafsi.

“Sekta binafsi ina changamoto nyingi tunazokabiliana nazo, tutumie vizuri fursa kama hizi za kukutana na serikali kueleza mambo yanayotukwaza ili yapatiwe majibu, lakini pia kama tuna ya kushauri huu ndio wakati wake,” alisema Dkt. Nyantahe.

Azania Bank Limited imeweka wazi kuwa ushiriki wake katika maandalizi ya mkutano huo muhimu kwa sekta binafsi na sekta ya umma ni kutaka kuwezesha uchumi wa viwanda kwa kuongeza fursa kwa sekta binafsi ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia ukuzaji uchumi kupitia ulipaji kodi.

No comments