Header Ads

Responsive Ads Here

USAJILI VITAMBULISHO VYA TAIFA KARATU WATIA FORA, ZAIDI YA WANANCHI 1200 KUSAJILIWA KWA SIKU


DSC04559
Umati  wa Watu uliofurika kupata huduma ya Usajili Vitambulisho vya Taifa wakati zoezi hilo likiendelea katika Kata ya Rhotia. Hawa ni akinamama wajawazito na wenye watoto wachanga wakipatiwa huduma maalumu kwa utaratibu maalumu uliowekwa wa kusaidia wazee, wajawazito na wamama wenye watoto wachanga.

DSC04563
Afisa Usajili Wilaya ya Karatu Bwana STEVE MBALA akiendelea na taratibu za kuthibitisha uraia wa waombaji na kugonga muhuri wakati zoezi hili likiendelea. utaratibu huu umekuwa ukifanyika kabla ya mwananchi kuruhusiwa kupiga picha, kuchukuliwa alama za vidole na saini ya kielektroniki.
DSC04568
Foleni hii ni ya Watendaji Kata na Wenyeviti katika Vijiji vya Kata ya Rhotia wakithibitisha makazi ya kila mwananchi anayeishi katika Kata na Kijiji chake kabla ya kutoa idhini ya kuthibitishwa uraia.
…….
Si kwa idadi hii ya watu iliyofurika katika Wilaya ya Karatu Kata ya Rhotia ambako Usajili wa Wananchi Vitambulisho vya Taifa unaendelea.
Kwa mujibu wa Afisa Usajili Wilaya ya Karatu Bi. Rehema Ngomuo takribani wananchi 1200 wamekuwa wakisajiliwa kwa siku na wengine kushindwa kuwasajili na kulazimika kurejea makwao tayari kwa siku inayofuata bila manung’uniko wala ulalamishi; kutokana na umati mkubwa wa wananchi kufurika kwenye vituo vya Usajili kupata huduma hiyo.
Diwani wa Kata hiyo Bwana Marseli Roli (CCM) ambaye muda wote amekuwepo kituoni hapo kuhakikisha wananchi wake wote wanasajiliwa kwa kuzingatia utaratibu uliopangwa amesema imekuwa ni kawaida ya wananchi katika Kata yake kuitikia wito haraka haswa katika masuala ambayo yana manufaa ya moja kwa moja na maisha yao ya kila siku.
“ Hili suala la Vitambulisho ni suala muhimu na kila mmoja anatambua umuhimu wake na ndiyo maana hatukupata shida ya kuwahamasisha wananchi kufika kusajiliwa kwa kuwa kila mmoja anatambua thamani ya kuwa nacho. Wengine hapa kama unavyowaona wamefika tangu saa 11 alfajiri” alisema
Kwa Wilaya ya Karatu Kata ambazo zinashiriki zoezi hili kwa sasa ni Kata ya Rhotia ambayo baada ya siku saba itafuatiwa na Kata za Janakona na Karatu. Wilaya zingine za mkoa wa Arusha zinaendelea na Usajili zikiwemo Arusha, Arumeru, Longido na Loliondo huku Ngorongoro wakiwa tayari kuanza Jumamosi hii.

No comments