Header Ads

Responsive Ads Here

UJENZI WA BANDARI KAVU HUKO KWALA WAFIKIA ASILIMIA 85 /WAKARIBIA KUKAMILIKA


SAM_5957
Mkuu wa Mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo ,alipotembelea eneo inapojengwa bandari kavu huko Kwala wilayani Kibaha.

Picha na Mwamvua Mwinyi
…………..
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
HALMASHAURI ya wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani,imetakiwa kupanga mpango mji katika kijiji cha Kwala ambapo inajengwa bandari kavu ili kuepukana na ujenzi holela.
Aidha kukamilika kwa ujenzi wa bandari kavu hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa malori Jijini Dar es Salaam kwani makontena yatakayoingia nchini hayatashushwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam badala yake yatashushwa kwenye bandari mpya ya Kwala.
Mkuu wa mkoa huo,mhandisi Evarist Ndikilo aliyasema hayo alipotembelea mradi huo ambao ulianza mwezi machi mwaka huu ukiwa na thamani ya sh.bilioni 7.2 ukijengwa na kampuni ya kizalendo ya Suma JKT chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

“Halmashauri ihakikishe inaweka mipango miji kwenye eneo hilo ili kusiwe na ujenzi holela “
“Pamoja na hilo kuwe na huduma zote kuanzia mahoteli sehemu ya magari kusubiria siyo zije kujengwa na watu binafsi, polisi, mabenki na huduma nyingine muhimu,” alisema mhandisi Ndikilo.

Alieleza halmashauri isisubiri mradi umalizike ndipo ianze kuweka mipango miji ,kinachotakiwa sasa ni kwenda sambamba na ujenzi wa mradi .

“Hapa patakuwa kitovu cha biashara na kutakuwa na shughuli nyingi hivyo lazima kuwe na mpangilio mzuri wa ujenzi “
“Hata miundombinu ya barabara ya kuja huku ni mbaya lazima mamlaka zinazohusika zianze kuboresha mazingira na mara kazi zitakapoanza mwakani serikali ijipatie mapato,” alisema mhandisi Ndikilo.

Meneja wa mradi huo ,Mhandisi Raymond Kweka alisema kwamba wanatarajia kukamilisha novemba 30 mwaka huu kwa awamu ya kwanza.
Alieleza ujenzi unaendelea vizuri ukiwa umefikia asilimia 85 kwenye eneo la mradi lenye ukubwa wa hekta zaidi ya 150.
Kweka alisema ,baadhi ya changamoto kubwa ni mvua baada ya barabara ya Vigwaza Kwala kukatika na maji kujaa kwenye eneo la mradi.
Pili maji yanatoka mbali ambapo mwanzo walitegemea bwawa jirani na mradi ambao limeendelea kukauka hivyo kusababisha kukosa maji.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha ,Beda Mbaga alisema wanatarajia kuanza kupitia maeneo yanayozunguka mradi huo ili kuweka mipango miji .

No comments