Header Ads

Responsive Ads Here

Ugeni wa Mfalme wa Oman Kuneemesha Uwekezaji Viwanda na Miundombinu

T2
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage akiteta jambo na Balozi wa Oman hapa nchini Mhe. Ali A. Al Mahruqi walipokutana katika hafla ya mapokezi ya meli iliyobeba ujumbe kutoka kwa mfalme wa Oman uliowasili katika bandari ya Dar es Salaam leo. Katikati ni Mfanyabiashara wa Tanzania Seif A. Seif.


Na.Paschal Dotto-MAELEZO
Serikali ya Oman imeonyesha nia ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi, kijamii, na kiutamaduni kwa manufaa ya maendeleo ya kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya ugeni huo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Hussein Mwinyi alishukuru ujio wa ujumbe huo na kusema kuwa watapata fursa ya kujionea sehemu ambazo wanaweza kuwekeza hapa nchini.
“Tunashukuru kwa ujio huu kwani ujumbe wa Serikali ya Oman umekuja kututembelea na kujifunza katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo lakini pia wanaweza wakawekeza na kuiwezesha Tanzania ya viwanda kufanikiwa ikiwa ni pamoja na kudumisha udugu, ushirkiano na mshikamano uliokuwepo tangu awali”,alisema Waziri Mwinyi.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage alisema ujio huo ni wa manufaa kwetu kwani Oman ni nchi ambayo imeendelea na ina uzoefu katika matumizi ya gesi inayotumika kuzalisha nishati kwenye ujenzi na viwanda hivyo watatupatia uzoefu katika maeneo ya uwekezaji na kushirikiana nao katika biashara mbalimbali.
“Oman ni wabia wakubwa ambao tunashirikiana  katika maeneo mengi ya uwekezaji, kwa sasa tutashirikiana katika bandari mpya ya Bagamoyo, na wao ndiyo watahusika kuchonga bandari hiyo na kuandaa maeneo ambapo  tunataka tuanze na viwanda 190 . alisema Waziri Mwijage
Akiendelea kusema kuwa Serikali ya Oman inatarajia kuwekeza katika viwanda vya kuzalisha sukari pamoja na kufanya biashara ya kahawa na chai moja kwa moja kutoka Tanzania kwenda Oman, pia kutafuta soko kubwa la zao la mbaazi nchini humo.
“Tunatafuta kufanya biashara na Oman hasa  soko la mbaazi ili kutoka kwenye soko la ndani mpaka kwenye soko la kimataifa tukianza na Oman,ingawa ni wateja wetu wa kihistoria haya ni maeneo ambayo mimi nayaangalia sana”, alisisitiza Waziri Mwijage .
Pamoja na faida tutakazopata kutokana na ugeni huu, Waziri Mwijage alibainisha kuwa,  watanzania wataweza kunufaika na elimu ya uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi watakayoipata kutoka kwao kwa kuwa nchi ya Oman ina uzoefu wa kutosha katika sekta hiyo.
 “Mbali na mafuta wao wana meli ya kubeba gesi iliyogandishwa (LNG Vessel) ambayo sisi tunaiona  kama ndoto kwa hiyo wana ujuzi mkubwa nitaongea na Waziri wa nishati ili tuone namna ya kushirikiana nao, hivyo ugeni huu utaleta neema kwa nchi yetu”, alisisitiza Waziri Mwijage.
Kwa upande wake Waziri wa Mafuta na Gesi kutoka Oman Dkt.Mohammed Hamed Al-Rumhi alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kudumisha upendo na ushirikiano katika masuala ya uchumi na udugu kama hapo zamani na kuweza kuinuana kuichumi.
“Tuko tayari kukuonyesheni nini tumefanya na makosa gani tulifanya kwenye masuala ya biashara za mafuta na gesi ili ninyi katika kuvuna mafuta na gesi msije mkafanya makosa kama yetu na vilevile kuona faida gani sisi tumepata ili nanyi muweze kupata huo ujumbe na kuweza kuitumia rasilimali yenu ya mafuata na gesi vizuri kabisa”, alisema Dkt. Hamed Al-Rumhi
Dkt. Hamed Al-Rumhi alisema kuwa wako tayari kutoa msaada wa mafunzo kwa Tanzania endapo Tanzania itakuwa tayari kutoa watu wake kujifunza masuala ya uvunaji wa gesi na mafuta.
Ujumbe kutoka kwa mfalme Shekh Sultan Qabous Bin Said wa Oman uko nchini kwa ziara ya siku sita ambapo umekuja na meli ya kifahari ikiwa na watu 350, na unaongozwa na Waziri wa mafuta na gesi  kutoka nchini humo, Dkt. Mohamed Hamed Al-Rumhi.

No comments