Header Ads

Responsive Ads Here

TANZANIA YAELEZA SABABU ZA KUJITOA MPANGO WA UWAZI SERIKALINI


SeeBait
Wakati Tanzania imejitoa katika Mpango wa Uendeshaji Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP), sababu za kufanya hivyo zimebainika.


Barua ya Tanzania kujitoa katika mpango huo iliyoandikwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga ya Juni 29 iliyowekwa kwenye tovuti ya OGP imeeleza sababu ni kutokana na kuwepo kwa Sheria ya Upatikanaji wa Habari ya mwaka 2016.


Amesema sheria hiyo inalenga kuongeza haki ya upataji wa taarifa na uwazi wa shughuli za Serikali.


Sababu nyingine amesema ni Serikali kuanzisha Tovuti Kuu ya Takwimu Huria (www.opendata.go.tz) kuchapisha data ili zitumiwe na mtu yeyote na hasa kutoka sekta za kipaumbele za elimu, maji na afya.


Pia, amesema Tanzania ni mwanachama wa Mpango wa Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) wenye malengo sawa na OGP.


Kutokana na hilo, amesema Tanzania inaamini uanachama katika mpango mwingine wenye malengo sawa unaweza kuathiri ushiriki wake.


Tanzania ilikuwa mwanachama wa OGP tangu Septemba 2011. Dhamira ya Serikali kujiunga na OGP ilikuwa kufanya shughuli zake kuwa wazi zaidi kwa wananchi kwa manufaa ya uboreshaji wa utoaji wa huduma kwa umma katika kupambana na rushwa na kujenga uaminifu zaidi.


Kupitia mpango kazi wa nchi wa OGP wa 2012-2013 na wa pili wa 2014-2016, Serikali ilitoa ahadi ya kuendeleza ufikiwaji wa taarifa kuhusu utekelezaji wa Serikali na kuchapisha takwimu huria kwenye sekta za kipaumbele za afya, elimu na maji.

No comments