Header Ads

Responsive Ads Here

Tanzania Kushiriki Tamasha la 19 la Dunia la Vijana na Wanafunzi


Pix 01
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Erick Shitindi akizungumza na baadhi ya vijana watakaoshiriki tamasha la 19 la Dunia la Vijana na Wanafunzi jijini Sochi nchini Urusi kabla ya kuwakabidhi bendera mapema hii leo jijini Dar es Salaam.

Pix 02
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Erick Shitindi (katikati) akimkabidhi bendera mmoja wa vijana watakaoshiriki tamasha la 19 la Dunia la vijana na wanafunzi jijini Sochi nchini Urusi, kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Bi. Venerose Mtenga.
Pix 03
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Bi. Venerose Mtenga toka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Bw. Erick Shitindi juu ya vijana watakaoshiriki tamasha la 19 la Dunia la Vijana na Wanafunzi jijini Sochi nchini Urusi.
Pix 04
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Erick Shitindi (aliyevaa tai) akiwa katika picha ya pamoja na vijana watakaoshiriki tamasha la 19 la Dunia la vijana na wanafunzi jijini Sochi nchini Urusi mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Picha na Eliphace Marwa – Maelezo
……………
Na. Eliphace Marwa
MAELEZO
DAR ES SALAAM
JUMLA ya Vijana 31 wanatarajia kuiwakilisha Tanzania katika tamasha la dunia la vijana linalotarajia kufanyika Jijini Sochi nchini Urusi  kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 22 Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na ujumbe wa Vijana hao leo Jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhiwa bendera ya Taifa,  Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Erick Shitindi alisema tamasha hilo litakuwa na zaidi ya washiriki ishirini elfu kutoka nchi 150 Duniani kote.
 Shitindi aliwapongeza vijana hao kwa fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika tamasha hilo na kuwaomba kuitumia vyema fursa hiyo kwa ajili ya kuiwakilisha vema na kutangaza uzuri wa nchi viongozi kwa mataifa mbalimbali.
“Tamasha hili litatoa fursa kwenu vijana wa Tanzania na mtakapokuwa huko kuzungumzia mambo mazuri ya Tanzania na hasa kutangaza uzuri wa nchi yetu kwa vijana wa mataifa mengine” alisema Shitindi.
Aidha Shitindi aliwaasa vijana hao kwa kutambua kuwa wanakwenda nchi ya ugenini na hivyo kuwa makini kwa kuwa  watakutana na watu mbalimbali wenye tabia, maadili na itikadi za mlengo tofauti tofauti za kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kiuchumi.
“ Kama mnavyofahamu Tanzania inasifika Duniani kote kuwa ni kisiwa cha amani na utulivu na ni nchi yenye maadili safi, hivyo tunategemea nanyi mtaenda kuonyesha nidhamu ya hali ya juu huko ugenini” aliongeza Katibu Mkuu Shitindi.
Shitindi aliwataka vijana hao kueleza uzuri na mandhari ya vivutio vya utalii vilivyopo nchini ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Mbuga za Serengeti na bonde la Ngorongoro ambalo ni moja kati ya maajabu saba ya dunia kuwa vipo na ni mali ya Tanzania na si vinginevyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Vijana Bi. Venerose Mtenga kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – ambaye ndiye mkuu wa msafara huo, alimuahidi Shitindi kuwa vijana hao watakuwa mabalozi wazuri kwa Tanzania.
“Lengo la tamasha hilo ni kuwakutanisha vijana kutoka nchi mbalimbali duniani ili kujenga mshikamano, kubadilishana uzoefu kidiplomasia, na uzoefu katika mbinu mbali mbali za maendeleo katika utandawazi”, alisema Venerose Mtenga .

No comments