Header Ads

Responsive Ads Here

Tanzania kunufaika na mafunzo ya KAIZEN kutoka Japan


PICHA 1
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Mradi wa KAIZEN ya siku tano wakifuatilia somo kutoka kwa mmoja ya wakufunzi  kutoka Japan mapema leo Jijini Dar es Salaam.

PICHA 2
Mkufunzi mkuu wa Mradi wa KAIZEN kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bi. Jane Lyatuu akieleza umuhimu wa Mradi huu kwa ukuaji wa viwanda nchini wakati wa kufunga mafunzo ya darasani yaliyofanyika katika ofisi za Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) Jijini Dar es Salaam.
PICHA 3
Mratibu wa mradi wa KAIZEN kutoka Tooku Garment(EPZA) Bw.Ibrahim Gamba akieleza faida alizozipata kutoka katika mafunzo ya siku tano ya  Mradi huo katika ukuaji wa viwanda nchini katika kufunga mafunzo hayo yaliyodumu kwa siku tano Jijini Dar es Salaam.
PICHA 4
Kiongozi mkuu wa Mradi wa KAIZEN kutoka Japan Takao Kikuchi akieleza jinsi ya uendeshaji wa Mradi huu kwa vitendo utakaonza hivi karibuni na kudumu kwa miezi sita baada ya kufunga mafunzo ya darasani yaliyofanyika (EPZA) jijini Daraes Salaam.
PICHA 5
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Mradi wa KAIZEN kutoka Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufungwa kwa mafunzo hayo leo (EPZA) Jijini Dar es Salaam.
PICHA 6
Meneja Uhamasishaji Uwekezaji kutoka (EPZA) Bi.Grace Lemunge akiwa katika picha na Washiriki pamoja na Wakufunzi wa mafunzo ya Mradi wa KAIZEN katika kufunga mafunzo hayo leo (EPZA) Jijini Dar es Salaam.
Picha na Paschal Dotto-MAELEZO
…………..
Thobias Robert-MAELEZO
07.10.2017
Tanzania itaendelea kunufaika na mafunzo aina ya KAIZEN kutoka kwa wataalamu wa Japan ili kuleta mabadiliko na kuongeza tija viwandani katika kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Hayo yalielezwa na Kiongozi wa Mafunzo hayo hapa nchini Bw. Takao Kikuchi kutoka Japani alipokuwa akifunga mafunzo hayo kwa njia ya kusoma darasani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) jana jijini Dar es Salaam.
“Tumeleta mafunzo ya KAIZEN nchini Tanzania kwa sababu, Tanzania ipo katika mchakato wa kuelekea kwenye uchumi wa viwanda, hivyo tumekuja kutoa mafunzo haya ili kubadili dhana zilizojengeka kwa wafanyakazi na wazalishaji ili wazingatie ubora na ufanisi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea,” alisema Bw. Kikuchi.
Katika mafunzo hayo  ambayo yamefanyika kwa siku tano yalilenga kuleta ubora, tija na uwajibikaji kwa wafanyakazi na wamiliki wa viwanda hapa nchini ili kuendeleza viwanda, kuongeza uzalishaji wa bidhaa bora kwa wateja, kuongeza ushindani wa viwanda hapa nchini pamoja na kupunguza gharama zisizo za lazima katika uzalishaji.
“Tatizo la uzalishaji viwandani halipo kwa viongozi bali kwa wafanyakazi kwani wakati mwingine wanakaa tu ofisi kupiga soga wakati wa kufanya kazi hivyo tunatoa mafunzo haya ili kueleza umuhimu wa kutumia muda vizuri na kutekeleza majukumu kwa wakati muafaka.” alisisitiza Bw. Kikuchi.
Kwa upande wake Mkufunzi Mkuu wa Mafunzo hayo kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bi. Jane Lyatuu alieleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa Viwanda vya hapa nchini kubadili mtazamo na uzalishaji usio na tija hivyo vitajikita katika kuzalisha bidhaa zenye ubora na manufaa kwa watumiaji.
“Dhana ya KAIZEN italeta tija, ubora na ufanisi ili kuendeleza viwanda vilivyopo na ambavyo tunatarajia kujenga hapa nchini, huduma pamoja na bidhaa zitakazokuwa zinazalishwa zitaweza kuhimili ushindani kwa soko la ndani na la kimataifa,” alifafanua Bi. Lyatuu.
Ametoa wito kwa Serikali kupeleka dhana ya KAIZEN katika shule na vyuo ili kujenga msingi ulio imara tangu utotoni pamoja na sekta, idara na wizara nyingine kwani itarahisisha utendaji kazi wenye tija usio na mazoea kama utamaduni uliojengeka kwa baadhi ya wafanyakazi hapa nchini.
Naye Mratibu wa KAIZEN kutoka katika Kiwanda cha Tanzania Tooku Garment Factory ambacho kipo chini ya EPZA Bw. Ibrahim Gamba alisema kuwa mafunzo yaliyotolewa na Wakufunzi kutoka Japan yatasaidia uzalishaji wa viwandani hapa nchini na kubadili kwa kiasi kikubwa uelewa na mazoea yaliyojengeka kwa baadhi ya watu na wamiliki wa viwanda.
“Mafunzo ya KAIZEN yanaelezea umuhimu wa hatua zote za uzalishaji kuanzia kwenye mchakato wa uzalishaji, menejimenti na namna ya kudhibiti uzalishaji na usamabazaji wa bidhaa kuanzia viwandani hadi kwa mlaji (Mteja), hivyo mafunzo haya ni muhimu kwa kila mwenye kiwanda hapa nchini,” alifafanua Bw, Gamba.
Aidha kwa upande wake Meneja uendelezaji uwekezaji kutoka EPZA  Bi. Grace Lemunge alieleza kuwa, mada zilizofundishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na umuhimu wa kutopoteza muda katika maeneo ya uzalishaji (viwandani), kuzalisha bidhaa kulingana na uhitaji wa soko, kuondoa urasimu katika shughuli za uzalishaji viwandani, mpangilio wa vitu viwandani na ofisini pamoja na kuhifadhi takwimu na taarifa kwa usahihi.
Mafunzo hayo yalifanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 2, Oktoba mwaka huu, ikiwa ni awamu ya pili ambapo yataendelea kwa muda wa miezi sita kwa vitendo katika mikoa nane yenye viwanda vingi hapa nchini ambayo ni Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Singida, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro na Mbeya.
Vilevile mafunzo hayo yalihudhuriwa na wawakilishi 25 kutoka katika viwanda vilivyopo chini ya EPZA ambavyo ni Tanzania Tooku Garment Factory, Kamal Steel Ltd, Quality Pulse, Hyses EPZ Company, Soman Agro Limited, wanafunzi kutoka chuo cha Uchumi na Biashara (CBE), SIDO pamoja na wakufunzi kutoka Japan kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA)
Awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ilianza mwaka 2013-2016 ambapo yalihusisha mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma na yalifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Mafunzo haya yatendelea kufanyika hapa nchini hadi 2020.

No comments