Header Ads

Responsive Ads Here

TAMKO LA MHE. UMMY MWALIMU (MB), WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, KUHUSU UNAWAJI WA MIKONO NCHINI TAREHE 15 OKTOBA, 2017 KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA UNAWAJI MKONO DUNIANIWaziri wa Afya Ummy MwalimuNdugu Wananchi,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta zinazohusika na Usafi na Afya Mazingira inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Unawaji Mikono (Global Hand Washing Day). Siku hii huadhimishwa tarehe 15 Oktoba ya kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha jamii kuongeza uelewa na ufahamu zaidi wa umuhimu wa unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni kama njia madhubuti na rahisi katika kudhibiti magonjwa yanayoweza kuenezwa na mikono iliyochafuliwa na vimelea mbalimbali vya magonjwa. Nchi yetu imekuwa ikiadhimisha siku hii tangu mwaka 2011 ambapo shughuli mbalimbali zenye kulenga kuhamasisha jamii zimekuwa zikifanyika.


Ndugu Wananchi,
Tunapokumbushia kila mwaka juu ya umuhimu wa unawaji wa mikono katika siku hii, ni kwa ajili ya kutia chachu katika jamii yetu juu ya manufaa yapatikanayo kutokana na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni. Umuhimu huu unakwenda sanjari na ukweli kwamba kutozingatia kanuni za tabia binafsi za usafi hupelekea kuenea kwa magonjwa. Ni dhahiri kuwa mikono michafu huchangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa magonjwa kama vile kuhara, kuhara damu, magonjwa ya macho na ngozi pamoja  na maambukizi ya mfumo wa hewa kama vile mafua na homa ya mapafu (pneumonia) ambayo kwa kiwango kikubwa, yanaweza kuepukika ikiwa tabia ya unawaji wa mikono ikizingatiwa ipasavyo.

Ndugu Wananchi,
Tafiti mbalimbali za hivi karibuni zinaonesha kuwa vyanzo vikuu viwili vya vifo vya watoto katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ni magonjwa ya kuhara na maambukizi ya mfumo wa upumuaji. Kitendo rahisi cha kunawa mikono kwa sabuni kinaweza kuondoa takribani nusu ya hatari ya uambukizwaji wa magonjwa ya kuhara na takribani theluthi ya maambukizi ya mfumo wa upumuaji. Hali hii inabainisha kunawa mikono kuwa ni chaguo bora zaidi na rahisi katika kuzuia maambukizi ya magonjwa.

Ndugu Wananchi,
Kunawa mikono na kuzingatia kanuni nyingine za usafi ikiwemo matumizi ya vyoo bora na maji safi na salama ya kunywa kwa ujumla wake vimebainika kuwa afua muhimu katika jamii yetu hasa kwenye makuzi ya watoto. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 30% ya udumavu wa mwili kwa watoto katika nchi yetu unasababishwa na kutokuzingatia kanuni za usafi. Hali hii inaweka changamoto zinazogusa nyanja za uchumi, maendeleo ya nchi na ustawi wa jamii kwa ujumla. Jamii inapokuwa na afya njema kunakuwa na manufaa ya kuongeza tija ya uzalishaji mali. Licha ya kuwa zoezi hili linaweza kuonekana dogo lakini kwa upande wa afya ni kubwa hasa katika kuzuia maambukizi ya magonjwa kwenye vituo vyetu vya afya. Takwimu zinaonyesha kuwa kunawa mikono kwa maji na sabuni kunaweza kupunguza magonjwa yanayoweza kutokea kwenye vituo vya afya (Hospital Acquired Infections) kwa asilimia 50%.

Ndugu Wananchi
Wahenga walisema Samaki mkunje angali mbichi, methali hii inatukumbusha jukumu tulilonalo la kuwafundisha watoto na vijana wetu umuhimu wa usafi binafsi hususani unawaji wa mikono kwa sabuni. Tafiti za kisayansi zinathibitisha kuwepo kwa uhusiano wa ongezeko la mahudhurio ya wanafunzi shuleni na uboreshaji wa miundobmbinu ya maji na usafi wa mazingira katika shule husika. Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia ndogo tu ya shule za msingi ndizo zina vifaa vya kunawia mikono. Hii ina maana kuwa tunahitaji kuboresha hali ya usafi wa mazingira katika shule ili matokeo makubwa sasa yaweze kufikiwa katika sekta ya Elimu. Hivyo, ninapenda kutoa wito kwa jamii kushirikiana na serikali kuhakikisha kuwa kila shule nchini inakuwa na huduma ya vyoo bora na pia sehemu maalum za kunawa mikono ili kuwakinga wanafunzi dhidi ya maradhi yanayoenezwa kwa njia ya uchafu.

Ndugu Wananchi,
Kauli mbiu ya Siku ya Kunawa Mikono kwa mwaka huu ni “Mikono Safi kwa Manufaa ya sasa na ya Baadaye! ambayo kwa kiingereza ni“Our Hands, Our Future!”, Kauli mbiu hii imejikita katika kusisitiza jamii yetu kwa ujumla wake kujenga tabia ya kunawa mikono nyakati zote muhimu hali inayoweza kuokoa maisha na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi . Unawaji wa mikono ninaufananisha na chanjo ambayo mtu anajichanja mwenyewe. Hii inatokana na ukweli usiopingika wa manufaa katika kuzuia magonjwa ambayo nimekwisha yataja hapo mwanzo. Vilevile, kauli mbiu hii inatupa fundisho zaidi za kulinda afya zetu na vivyo hivyo kutuwezesha kuimarisha afya yetu, familia na jamii kwa sasa na baadaye ili kujiweka tayari kwenye uzalishaji viwandani, mashambani na maofisini.  

Ndugu Wananchi,
Afya bora kupitia usafi wa mikono ni moja ya misingi  ya kuitambua jamii kuwa ni wastaarabu. Hatuwezi kuwa na afya bora kama hatujawekeza kwenye masuala muhimu ya kulinda afya zetu. Hali ya unawaji mikono katika Bara letu la Afrika si wa kuridhisha kwani imebainika kuwa nchi nyingi zina wastani wa chini ya asilimia 50%. Kwa upande wa nchi yetu ni asilimia 12% tu ya kaya zina vifaa vya kunawia mikono vinavyofanya kazi. Takwimu hizi zinadhihirisha kuwa kati ya watu 100 ni kumi 12 hunawa mikono. Mtakubaliana nami kuwa kupitia utamaduni tuliojijengea wa kusalimiana kwa kushikana mikono unaweza ukapima namna ambavyo tunaweza kuambukizana magonjwa kwa njia hii. Wito wangu kwenu wananchi ni kila mmoja wetu azingatie tabia ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kwa manufaa yetu sote.

Ndugu Wananchi,
Neno ustaarabu lina maana pana hasa katika kipimo cha maandeleo kwani ustaarabu unajumuisha usafi katika nyanja zote. Kwa muktadha huu, ni matumaini yangu unapoitwa mstaarabu katika jamii yetu tambua kwamba wewe ni miongoni mwa watu wasafi wanaozingatia kanuni zote za afya. Ni matumaini yangu sote kwa pamoja tutabadilika katika kuhakikisha kaya zetu zinakuwa na vifaa vya kunawia mikono nyakati zote muhimu ambazo ni KABLA YA KULA, KABLA YA KUANDAA CHAKULA, BAADA YA KUTOKA CHOONI, BAADA YA KUMSAFISHA MTOTO ALIYEJISAIDIA NA KABLA YA KUMLISHA MTOTO.

Mwisho
Kutokana na hali hii niliyoieleza, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wadau imejipanga kutumia njia mbalimbali ambazo zitasaidia kupunguza tatizo la uchafu katika mazingira yetu ikiwemo unawaji wa mikono. Ili kukabiliana na tatizo la uchafu wa Mazingira nchini, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inatekeleza Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira. Kupitia Kampeni hii tunatarajia kuongeza idadi ya kaya zitakazo kuwa na vifaa vya kunawia mikono angalau kwa zaidi ya asilimia 50% toka asilimia 12% ilivyo sasa hadi asilimia 50% ifikapo 2021. Kupitia kauli mbiu ya NIPO TAYARI ya Kampeni hii ninamtaka kila mmoja wetu awe tayari kubadilika na kuzingatia usafi kwa ujumla wake. Aidha, nitoe rai kwa wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika kutekeleza Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira, kwani ni kwa manufaa yetu wenyewe na vizazi vijavyo. 

Itakuwa faraja kubwa kwangu na Serikali kwa ujumla endapo kila Mji/Kata/Mtaa/Kijiji na Kitongoji kitashirikisha wananchi wake katika shughuli za usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uwekaji wa vifaa vya kunawia mikono. Hali kadhalika, Viongozi na Wataalam Afya Mazingira waendelee kuwa mstari wa mbele kuhimiza suala hili kwenye jamii. Nimatumaini yangu kwamba tutakapoadhimisha Siku ya Matumizi ya Choo Duniani na Wiki ya Usafi tarehe 19 Novemba, 2017 elimu na hamasa kuhusu kunawa mikono kwa maji na sabuni kutakuwa kumezoeleka.Ahsanteni kwa kunisikiliza

No comments