Header Ads

Responsive Ads Here

TABORA YAMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA MIRADI YA MAENDELEO INAYOENDELEA KUTEKELEZWA

 

NA TIGANYA VINCENT.

 TABORA.

VIONGOZI mkoani Tabora wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Johni Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kuwajengea  miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani huo , hatua ambayo imeufanya uanze kufunguka kwa kasi na kuwa na mazingira mazuri kwa wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali.

Tamko hilo limesomwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri kwa niaba ya viongozi wenzake kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Wilaya wakati wa kufanga kikao kazi cha siku tatu kilichofanyika mjini hapa.
Alisema kuwa uamuzi  wa Rais Magufuli kupeleka mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao umeanza kujengwa tangu Agosti 24 mwaka huu , maandalizi ya  ujenzi wa reli ya kisasa, upanuzi wa uwanja wa ndege, maandalizi ya ujenzi wa bomba la mafuta na ujenzi wa barabara za lami umesaidia kuufungua mkoa huo na kuwafanya watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kuanza kuonyesha nia ya kutaka kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali.
Mwanri alizitaja  jitihada Rais Magufuli kuwa ni pamoja na  kupambana dhidi ya ubadhirifu wa mali za umma, rushwa , ukwepaji kodi na kuongozeka ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na  uwajibikaji katika maeneo ya kazi.
Aliongeza kuwa jitihada nyingine ni kuzuia shughuli zisizo na tija na kuongeza bajeti katika huduma za jamii kama vile maji na afya  zimesaidia kuleta  matumaini makubwa wakazi wa Tabora.
Mwanri alisema kuwa viongozi wa Tabora kwa pamoja wanaunga mkono juhudi hizo za Rais Magufuli ambazo zinaendeleza kazi kubwa ya Mwasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kuwatumikia wananchi na kushughulikia shida za wananchi.
Alisema kuwa kwa pamoja wanaahidi kuendelea kushirikiana naye katika mapambano dhidi ya maovu yote ikiwa ni pamoja na kudhibiti utoroshaji madini na makinikia nje ya nchi na kuhakikisha rasilimali ambazo Mungu amewajali Watanzania zinawanufaisha wananchi wengi na sio watu wachache.
Mwanri alisema kuwa Mkoa wa Tabora utaendelea kutekeleza kwa nguvu zote maagizo yote yatakayokuwa yanatolewa na Rais na viongozi wote ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa mkoa huu.
Kikao kazi hicho cha siku tatu kiliwashirikisha Wakuu wa Wilaya zote, Wakurugenzi Watendaji, Wakuu wa Idara na Seketarieti ya Mkoa wa Tabora kwa lengo la kuwajengea uwezo na kukumbusha majukumu yao katika kuhakikisha wanawatumia wananchi kwa ufanisi zaidi.

No comments