Header Ads

Responsive Ads Here

RC TABORA: HALMASHAURI TOENI USHIRIKIANO KWA POLISI ILI KUKOMESHA MAUAJI

Na Tiganya Vincent
RS-Tabora
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeziagiza Halmashauri zote mkoani hapa kuongeza ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika hatua yake ya kukabiliana na vitendo vya kihalifu ikiwemo mauaji yanayotokana na imani za kishirikina.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa mkutano uliwahusisha Wakuu wa Wilaya , Wakurugenzi Watendaji  , Wakuu wa Idara na Seketarieti ya Mkoa wa Tabora.
Alisema kuwa haiwezekani watu wakaendelea kufa katika maeneo yao kwa sababu ya kushindwa kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa ambazo zinaweza kuzuia na kukomesha vitendo vya kihalifu.
Mwanri alisema kuwa watendaji wengi ambao ni waajiriwa wa Halmashauri ndio wako karibu na wananchi na kwao ni rahisi kupata taarifa za mipango yote inayopangwa na wahalifu kwa urahisi kupitia raia wema na hivyo kusaidia Polisi kuzuia uhalifu unaokuwa umepangwa kufanyika.
Alisema kuwa ni vema viongozi hao wakasimama katika nafasi zao kama viongozi wa Kamati za Ulinzi za maeneo yao kuanzia kijiji hadi Kata ili kukomesha mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu kwa kuwakata watu wanaokusudia kutekeleza vitendo hivyo na kuwafikisha Polisi ili hatua zaidi za kisheria.
Mwanri alisema kiongozi yoyote anayekaa na kusubiri Jeshi la Polisi ndio lije kuzuia uovu katika eneo lake hafai na anapaswa ajitathmini kama anafaa kuendelea na nafasi alinayo.
“Haiwezekani mkaa kama viongozi mnaangalia watu wanauwawa, huku hatumchukui hatua ya kusaidiana na Jeshi la Polisi…..Mkuu wa Jeshi la Polisi mimi na wakuu wa Wilaya na viongozi wote tunakuahidi tutakupa ushirikiano utakaohitaji ili kukomesha tabia hiyo ya mauaji” alisisitiza Mkuu huyo Mkoa.
Alisema kuwa haiwezekani watu wanakuja katika Kijiji , halafu Mwenyekiti wa Kijiji na viongozi wa Kijiji wanakaa kimya na kuona jambo hilo ni kitu cha kawaida.
Mwanri alisisitiza kuwa ikitokea mauaji katika Kijiji watu wa kwanza watakaosaidia ni viongozi ili waeleze kuwa walishindwaje kupata taarifa juu ya mauaji ambayo yameandaliwa na kundi kubwa kama yale yaliyotokea hivi karibuni kata ya Uchama wilayani Nzega.
Aidha Mkuu wa Mkoa amezitaka Halmashauri kushirikiana na Jeshi hilo katika ujenzi na uboreshaji wa Vituo vya Polisi katika maeneo ambayo yanahitaji lakini havipo.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Wilbroad Mtafungwa alisema kuwa Jeshi hilo limejitahidi kupita katika Wilaya zote kuelimisha jamii juu ya kupiga vita vitendo vya ushirikina na ramli chonganisha ambazo zimekuwa chanzo kikubwa cha mauaji ya wazee na walemavu wa ngozi.
Alitoa wito kwa taasisi nyingine nao kuendelea kuungana mkono juhudi za Polisi za kuwaelimisha na kuwakamata watu wote wanaendesha vitendo vya ramli hizo chonganishi ambao baadhi yao wameshafikishwa Mahakamani.

No comments