Header Ads

Responsive Ads Here

MWANSANSU MWENYEKITI MPYA CHAMA CHA MAPINDUZI -NAMTUMBO


NA YEREMIAS NGERANGERA -NAMTUMBO

Wanachama wa chama cha mapinduzi wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wamemchagua Aggrey Mwansasu kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho kwa kumbwaga aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Benjamini Nindi .

Uchaguzi wa kumpata mwenyekiti huyo ulifanyika katika Bwalo la shule ya sekondari Namtumbo shule ambayo inamilikiwa na jumuiya ya wazazi wa chama cha mapinduzi kilomita tatu kutoka mjini Namtumbo.

Aidha katika uchaguzi huo awali uliingia dosari baada ya msimamamizi wa uchaguzi huo Zena Rashidi Mijinga kujisahau kwa kutosoma kanuni ya kushinda uchaguzi ni sharti mgombea apate asiliomia hamsini ya kura zitakazopigwa.

Dosari ya kanuni hiyo kutosomwa awali ilijionesha baada ya wagombea wa nafasi ya uenyekiti kutofikia asilimia hamsini ya kura zilizopigwa na kuwataka wajumbe wa mkutano huo kurudia kupiga kura kwa nafasi ya uenyekiti hali iliyoibua hasira kutoka kwa wajumbe kwa madai ya kutaka kumbeba mgombea mmojawapo katika uchaguzi huo na kuongeza kuwa kanuni hizo kwa nini hazikusomwa kabla ya uchaguzi na badala yake zisomwe wakati uchaguzi umefanyika.

Mwenyekiti wa muda wa mkutano huo bwana Fadhili Kitete alionekana kuokoa jahazi kutoka kwa wajumbe waliotaka kukataa kurudia uchaguzi huo kwa kuwaomba wajumbe hao radhi kwa kutosoma kanuni hizo kabla ya uchaguzi na kusema kuwa ni kosa la kibinadamu na kuwataka wajumbe waridhie kurudia kupiga kura kwa nafasi hiyo ya uenyekiti kwa kuzingatia kanuni hiyo ya asilimia Hasini ili uchaguzi huo uwe wa haki na uliofuata kanuni za uchaguzi.

Bwana kitete aliongeza kuwa kanuni ndizo zinazoongoza uchaguzi na kurudia uchaguzi hautazuia wajumbe kumchagua mgombea wanayempenda alisema mwenyekiti huyo wa muda wa uchaguzi huo.

Wajumbe kwa pamoja walikubaliana na hoja ya Mwenyekiti huyo wa muda kurudia kupiga kura katika nafasi hiyo ya mwenyekiti wa chama wa wilaya.
Waliogombea nafasi ya uenyekiti wa chama wilaya ya Namtumbo walikuwa wanne ambao ni Legani Luambano ,Yordani Fusi,Benjamini Nindi na Aggrey Mwansasu ambapo katika uchaguzi wa awali Legani Luambano alipata kura 20, Yordani Fusi alipata kura 25, Benjamini Nindi aliyekuwa akitetea kiti hicho alipata ura 290 na Aggrey Mwansasu alipata kura 304 kati ya kura 645 zilizopigwa.

Uchaguzi wa marudio uliwashindanisha wagombea wawili Benjamini Nindi na Aggrey Mwansasu ambao walionesha kuwa na ushindani mkubwa kwa wajumbe lakini mpaka mwisho wa uchaguzi huo msimamizi wa uchaguzi huo  Zena Rashidi alimtangaza Aggrey Mwansasu kuwa mshindi kwa nafasi ya uenyekiti kwa kumbwaga mpinzani wake Benjamini Nindi aliyekuwa anatetea nafasi hiyo kwa awamu nyingine tena.

Zena Rashidi alimtangaza Aggrey Mwansansu ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura 369 dhidi ya kura 228 alizopata mpinzani wake kati ya kura 610 zilizopigwa ambapo kura 13 ziliharibika katika uchaguzi huo .Mkutano huo pia uliwachagua wajumbe wawakilishi wa mkutano mkuu wa Taifa,mkutano mkuu wa mkoa na viongozi wa jumuiya ya wanawake, vijana na wazazi.

No comments