Header Ads

Responsive Ads Here

MIAKA 18 YA KIFO CHA NYERERE NA ELIMU BURE

Neema Mathias na Thobias Robert-Maelezo
25, sept 2017
“Maandiko ya Dini zetu yanasema kuwa; “Kila nafsi itaonja umauti katika dunia hii, mwanadamu ni mavumbi na mavumbini atarejea, hii ndiyo hali halisi ilivyo hatuna budi kuwaombea mema wale wote waliotangulia mbele ya haki kwani, ‘mbele yao nyuma yetu”.

Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anatimiza miaka 18 tangu atangulie mbele ya haki, mnamo tarehe 14, Oktoba 1999. Watanzania na wapenda haki amani uzalendo na mshikamano kote duniani wanatambua kumbukumbu hii ilivyo muhimu katika mustakabali wa Taifa la Tanzania na kuenzi Umoja Barani Afrika.
Aidha, kuna mengi ya kujifunza na kukumbuka tunapoadhimisha kumbukumbu hii, hususan katika suala zima la kuwaridhisha wale vijana wa Tanzania ambao hawakupata kuishi enzi za utawala wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Baba wa Taifa alifanya mambo mengi katika kuijenga Tanganyika na baadaye Tanzania huru, katika nyanja mbalimbali ikiwemo siasa, ambapo alihimiza umoja, uzalendo na utumishi uliotukuka kwa viongozi, kupiga vita rushwa, ubadhilifu, uonevu na kuwaletea maendeleo wananchi hususan wanyonge.
Aidha, Mwalimu alipiga vita ubaguzi, kuwa na matabaka, udini, ukanda, ukabila na kuwaunganisha Watanzania wote kwa kutumia lugha ya Kiswahili, ambayo imebaki kama alama ya ushindi ya umoja kwa watanzania.
Upande wa uchumi alihimiza kufanya kazi kwa bidii, kujituma, kuwa mbunifu, mpinga rushwa,  kuwa na matumizi sahihi kwa fedha za umma, kupiga vita uzembe kazini, kuwa wazalendo na kuipenda nchi yako,  kuimarisha viwanda ili kukuza uchumi ambao ulimilikiwa na umma wa Tanzania, pia  viwanda vilitoa ajira nyingi kwa wananchi.
Mwandishi wa Makala hii amelenga kuangazia juu ya sera ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ya “Elimu Bure” mara baada ya uhuru, ambayo ililenga kuondoa maadui wakuu watatu yaani ujinga, umasikini na maradhi.
Mara baada ya uhuru wa Tanganyika Mwalimu alitambua kuwa kuna idadi ndogo sana ya wasomi, pia wananchi waliowengi walikuwa hawajui kusoma wala kuandika. Elimu ni jambo muhimu katika Taifa lolote ili kuweka msingi imara ya wasomi wenye weledi wa kutosha wanaoweza kutumia mazingira yao, katika kujiletea maendeleo na kutatua changamoto zinazowazunguka.
Mwalimu alitambua Elimu iliyotolewa na wakoloni ilikuwa na kasoro kama vile ubaguzi wa rangi, kujenga matabaka ya wazungu, wahindi, waarabu na watoto wa kiafrika wa machifu wenye uwezo na wasiokuwa nacho, ubaguzi wa dini, kabila nk. Kutokana na ubaguzi huo kulikuwa na shule za wazungu, wahindi, waafika lakini watoto wa mchifu na viongozi wa kiafrika ambao ni sawa asilimia 40 tu.
Mwalimu kwa juhudi na weledi wake alianza kutafuta Elimu kwa watoto wote wa Tanganyika hata kabla ya uhuru.  Mathalani, Mwalimu Nyerere alipopata fursa ya kuzungumza mbele ya Umoja wa Mataifa (UN) Desemba, 20 mwaka 1956 miongoni mwa mambo aliyozungumzia ilikuwa ni suala la ubaguzi katika kupata fursa ya elimu kati ya watoto wa  Tanganyika  na wale wa kikoloni.
Kutokana na changamoto za kutopata elimu na uwiano mdogo wa watu wanaojua kusoma na kuandika, mwaka 1967, Mwalimu Nyerere alitangaza Azimio la Arusha lililolenga utoaji wa ‘Elimu Bure” kwa Watanzania wote waliofikisha umri wa miaka saba kwa lengo la kuondoa ujinga, umasikini na maradhi.  
Mfumo wa Elimu Bure Tanzania ulioanzishwa na Mwalimu Nyerere ulilenga kusisitiza   juhudi za pamoja katika kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Pia, ulihimiza misingi ya usawa na wajibu wa kutoa huduma ambazo zinaendana na kipaji maalum katika kuhimiza elimu ya kujitegemea.
“Elimu yetu lazima ipingane na mawazo ya kiburi cha usomi kwani hii inapelekea waliosoma kuwadharau wale ambao vipaji vyao sio vya kisomi au wasio na uwezo wowote lakini ni binadamu wa kawaida, dharau kama hii haina nafsi katika jamii ya raia walio sawa,”. Alisema Mwalimu Nyerere.
Juhudi za Mwalimu Nyerere katika kuhakikisha kuwa wimbi kubwa la ukosefu wa elimu kwa Watanzania linapungua ama kumalizika kabisa zilizaa matunda kwa kiasi kikubwa kwani idadi ya wanafunzi shuleni iliongezeka ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo awali.
Mathalani, takwimu zinaonesha kuwa, Uandikishaji wa wanafunzi katika shule ya msingi ulipanda kutoka asilimia 25 ambapo asilimia 16 kwa watoto wa kike kwa mwaka 1960 hadi asilimia 72 ambapo asilimia 85 kwa watoto wa kike.
Mwaka 1985 (ingawa idadi ya wananchi ilikuwa inaongezeka kwa kasi); asilimia ya watu wazima waliojua kusoma na kuandika ilipanda kutoka asilimia 17 mwaka 1960 hadi 63 mwaka 1975 hii iliongezeka kuliko nchi nyingine za Afrika na iliendeelea kupanda.
Waswahili husema; “Kusifiwa siyo shani, shani ni kushuhudia”, ikiwa na maana kuwa habari ya kusimuliwa si halisi uhakika wake utaupata ukijionea mwenyewe, methali hii inajidhihiriha kwa baadhi ya Walionufaika na Sere ya Elimu Bure ya Mwalimu Nyerere, ambao mpaka sasa wapo katika uongozi wa serikali, Bunge au Mahakama. Aidha, wengine elimu waliyoipata wamekuwa wafanyabiashara wakubwa wenye mafanikio.
Wanufaika hao walipata elimu kati ya miaka 1967 mpaka mwaka 1985 kutoka darasa la kwanza mpaka Chuo Kikuu, kupitia sera ya “Elimu Bure”. Hakika Mwalimu Nyerere sio rahisi Watanzania kukusahau kwa mema na maarifa waliyoyapata ili kujenga Taifa hili.
Mfano Tanzania sasa ina wataalamu wa madini wanaoweza kumsaidia na kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuwa zoezi hili tunaibiwa, na hapa tunadanganywa, kwa sasa kama nchi tunaweza kufanya smelting ya madini ujuzi huo tunao nk. Haya yote ni kazi ya Mwalimu Nyerere pumzika kwa Amani Baba.
Sera ya Elimu Bure ya mwaka 1976 ilifutwa na kuanzishwa Sera ya uchangiaji Elimu ya mwaka 1986, ambayo ilileta changamoto kubwa kwa wazazi na walezi wa watoto nchini Tanzania. Changamoto kubwa  ikiwa ni kupungua kwa idadi ya watoto waliojiandikisha kuingia darasa la kwanza na utoro uliokidhiri mwaka hadi mwaka kuwa na kupelekea idadi ndogo ya watoto waliohitimu kidato cha nne.
Takribani miaka 30 imepita (1985-2015) ya sera ya uchangiaji elimu na kuonekana kwa changamoto lukuki, ambazo hazijengi Taifa lenye umoja na Usawa. Ndipo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe magufuli, ikawafuta machozi Watanzania wanyonge ambao hawakuwa na uwezo wa kuwasomesha watoto wao.
Elimu Bure na Magufuli ya mwaka 2016, ni mkombozi iliyofanya ndoto za wanyonge kuwa kweli, ambapo inatolewa kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne. Mwaka 2016 idadi ya watoto walioandikishwa kuanza darasa la kwanza ilivuka lengo hadi asilimia 120, dhahiri imeonyesha ni jinsi gani sera hii imepokelewa kwa mafanikio makubwa.  Sera ya Elimu Bure inaendeana na jukumu la Malengo ya Melenia ya Dunia inayosema “Elimu ni haki ya kila mtoto na raia kuhakikisha anapewa na Taifa lake” 
Ikumbukwe, wazazi bado wanawajibu wa kuhakikisha mtoto anaandaliwa vema kabla ya kwenda shule, yaani apewe mahitaji muhimu. Mahitaji hayo ni pamoja na mavazi, malazi na chakula, hivyo bado mzazi au mlezi ana wajibu wa kumhudumia mwanaye ipasavyo.
Huko Afrika Kusini, Baba wa Taifa hilo Hayati Nelson Mandela, ambaye alipiania uhuru na kuwakomboa waafrika kusini kutoka kwenye minyororo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kutoka kwa makaburu na Rais wa Kwanza wa Taifa lisilo la Ubaguzi, aliyefariki mwaka 2013 akiwa na umri wa miaka 95, hukumbukwa kila ifikapo tarehe 5, Disemba kila mwaka.
Wahega husema ‘usilipe baya kwa baya’, Mandela alikuwa kiongozi maarufu na mwenye nguvu duniani kutokana na kutolipiza kisasi kwa makaburu baada ya kutoka gerezani kwani wengi walifikiri angefanya hivyo. Baada ya kutoka katika gereza la Robben island ambako alifungwa kwa miaka 27, Mandela aliweka mazingira mazuri ya upatanisho kati ya makaburu ambao waliwatesa watu weusi wakati wa kupigania uhuru wa Afrika Kusini.
Katika kudhihirisha utu, hekima na busara alizokuwa nazo, Mandela aliwahi kusema, “Utafanikiwa vingi katika dunia hii kupitia matendo ya rehema kuliko kwa matendo ya kuadhibu watu” akiwa na maana kuwa kiongozi anapaswa kufanya matendo mema kwaajili ya maendeleo ya taifa lake na siyo kulipa kisasi kwa waliokutendea mabaya.
Ni wazi kuwa mataifa na mashujaa wapo wengi duniani, lakini sina budi kuyataja kwa uchache kwani ninaweza nikaandika hadi nikamaliza kurasa kwa kurasa juu ya kumbukumbuku ambazo hufanywa na mataifa mbalimbali kwa waasisi wao.
Mbali na kuadhimisha kumbukumbu za waasisi hao mataifa mengi yamekuwa yakiendeleza na kuyapa kipaumbele yale mazuri yaliyoachwa na waanzilishi wa nchi hizo kwa lengo la kukuza mataifa yao katika Nyanja mbalimbali kama vile za kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa.
Tanzania bado tunahitaji mapambano ya dhati katika kukabiliana na maadui watatu wa maendeleo aliowaoanisha Hayati Mwalimu Nyerere ambao ni maradhi, umasikini na ujinga. Pumzika kwa Amani Mwalimu.

No comments