Header Ads

Responsive Ads Here

MAWAZIRI WA UVUVI ZANZIBAR,TANZANIA WAKAGUA MELI ZINAZOOMBA LESENI


Na Kijakazi Abdalla            Maelezo   
UTARATIBU wa kusajiliwa kwa meli za kigeni hapa Tanzania kwa ajili ya kuendesha shughuli za uvuvi, ni miongoni mwa njia zitakazotoa fursa za ajira kwa Watanzania.

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mhe. Hamad Rashid Mohammed, amesema pia kwamba utaratibu huo utasaidia kuimarisha uchumi kwa kukuza pato la taifa.
Akiwa katika ziara ya kuitembelea meli ya uvuvi ya kampuni ya XINSIJI No. 83 kutoka Jamhuri ya Watu wa China iliyofika bandarini Zanzibar, Waziri huyo alisema, Tanzania itapata mabalozi wazuri ikiwa vijana wake wataajiriwa katika meli za aina hiyo.
Meli hiyo ipo kisiwani Unguja kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi ikiwa ni utaratibu wa kawaida na kisheria kabla kupewa leseni ya kuendesha shughuli za uvuvi hapa nchini.
Aidha alisema, kuongezeka kwa meli hizo zinazovua katika bahari kuu samaki wenye viwango, kutawanufaisha wananchi wa Zanzibar pamoja na wageni wanaofika nchini kwa ziara za kitalii ambao hoteli wanazofikia zina mahitaji makubwa ya samaki.
“Meli kama hizi ni muhimu kwa visiwa vyetu pamoja na Tanzania, kwani kuna uhakika wa kupatikana samaki wenye sifa na viwango vinavyokubalika kiafya kwa usalama wa mlaji,” alisema Waziri huyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Abdallah Hamis Olega, amesema kuwepo kwa meli za uvuvi kutahakikisha rasilimali za nchi hazipotei.
Alisema katika wakati huu ambapo Tanzania iko safarini kuelekea kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati, kupatikana samaki kwa wingi na wenye kiwango kizuri, kutahamaisha uwekezaji katika viwanda vya  kusindika samaki.
Olega, alisema pia kwamba hatua hiyo inaleta matumaini makubwa kwa vijana wa Kitanzania kufaidika na fursa za ajira, na kuondoa mazoea ya kutokuajiriwa kwa wazalendo katika meli zilizojikita katika uvuvi wa bahari kuu.
Ziara ya viongozi hao kutembelea meli zilizomo katika hatua ya kuomba leseni za uvuvi wa bahari kuu ni ya kwanza, ambapo kwa sasa meli 17 zimeomba leseni ili kuanza kuvua samaki.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
………..
ONE
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI WA TANZANIA ABDALLAH HAMIS OLEGA AKIKAGUA MELI YA KAMPUNI YA XINSHIJI NO 83 ILIYOFIKA ZANZIBAR KWA AJILI YA KUOMBA LESENI YA UVUVI WA BAHARI, KUU NCHINI TANZANIA.
TWO
WAZIRI WA KILIMO, MALIASILI, MIFUGO NA UVUVI WA ZANZIBAR HAMAD RASHID MOHAMMED, AKIZUNGUMZA NA MWAKILISHI WA KAMPUNI YA INTRECHICK ZANZIBAR HUKO BANDARINI UNGUJA.
THREE
WAZIRI WA KILIMO, MALIASILI, MIFUGO NA UVUVI ZANZIBAR HAMAD RASHID MOHAMMED NA NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI TANZANIA ABDALLAH HAMIS OLEGA WAKIPAKIA SAMAKI KATIKA GARI BANDARINI MJINI ZANZIBAR.
PICHA ZOTE NA KIJAKAZI ABDALLA    MAELEZO ZANZIBAR

No comments