Header Ads

Responsive Ads Here

HALMSHAURI YA WILAYA YA MUFINDI NA PELUM TANZANIA YAPITISHA MPANGO WA MATUMIZI YA ARDHI KWA VIJIJI VINNE


1.Mkuu wa Idara ya ardhi na makazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa, Jeswald Ubisimbali akifafanua jambo kuhusu utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Halmashauri hiyo kupitia mradi wa ushiriki wa wananchi katika kilimo (CEGO) unaosimamiwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).Na Mwandishi Wetu,
Mufindi
10.10.2017

HALMASHAURI ya Mufindi Mkoani Iringa kwa kushirikiana na Shirika la PELUM Tanzania kupitia mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika sekta ya kilimo (CEGO) limepitisha Mpango wa Matumizi ya Ardhi kwa vijiji vinne  vya Halmashauri hiyo, hatua inayolenga kuongeza wigo wa ushirikishaji wa jamii katika usimamizi wa rasilimali za ardhi.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwandishi wa Habari hii,  Mkuu wa Idara ya Ardhi na Makazi Wilaya ya Mufindi, Jeswald Ubisimbali alivitaja vijiji vilivyopitisha Mpango huo kuwa ni Magunguli, Isaula, Usokami na Ugesa.
Ubisimali alisema zoezi hilo limesaidia kwa kiasi kikubwa juhudi za Serikali katika kumaliza migogoro ya ardhi katika maeneo hayo sambamba na kuongeza idadi ya vijiji vilivyofanyiwa mpango wa matumizi ya Ardhi Wilayani humo.
“Kumekuwa na migogoro ya ardhi katika wilaya ya Mufindi baina ya wakulima, wafugaji, na wawekezaji wakubwa jambo ambalo limechangia kuzorotesha shughuli za maendeleo hivyo kupita kwa Mipango ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji vinne hemu ya mafanikio makubwa kwa Serikali” alisema Ubisimbali.
Alisema kuwa kupitia Mpango huo, Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na Shirika la PELUM Tanzania limefanikiwa kupima zaidi ya vipande 500 katika kila kijiji kilichoanishwa katika Mpango huo  ikijumuisha makazi, mashamba na Taasisi.
Aidha alisema mara baada ya ya mipango hiyo kupita, Halmashauri ya Wilaya kwa kushrikiana na Shirika la PELUM Tanzania linatarajia kuandaa hati miliki za kimila kwa kwa taasisi na wananchi wote waliopimiwa maeneo yao kukabidhiwa hati zao kuonyesha umiliki halali wa maeneo yao.
Ubisimbali alisema kuwa Wilaya ya Mufindi ina jumla ya vijiji 121 ambapo ni vijiji 43 pekee ndivyo vimefanyiwa Mpango wa matumizi ya Ardhi na hivyo kulitaka Shirika la PELUM Tanzania kuendelea kutafuta miradi mingine ili kuweza kusaidia vijiji vingine vilivyobaki katika mpango huo.
Alisema kutokufanyika kwa Mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vilivyobaki inasababishwa na Halmashauri kuwa na bajeti finyu ikiwemo ukusanyaji wa mapato kutokufikia malengo jambo linalochangia kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi kwenye baadhi ya vijiji wilayani humo.
Ubisimbali alisema vijiji 13 katika Wilaya hiyo ndiyo vyenze vilivyopo kwenye migogoro mikubwa ya ardhi baina  ya wananchi na wawekezaji zikiwemo Kampuni za Mufindi Paper Mills, Green Resource Limited na SAO HILL FOREST na hata hivyo jitihada mbalimbali zinafanywa na Halmashauri hiyo ili kutatua changamoto hiyo.
Wilaya ya Mufindi ni moja kati ya Wilaya sita zinazonufaika na mradi wa CEGO unaotekelezwa katika Halmashauri sita nchini ikiwemo Morogoro Vijijini, Mvomero, Kongwa, Bahi, Kilolo na Mufindi kupitia mashirika wanachama ya TAGRODE-Iringa, UMADEP-Morogoro na INADES-Dodoma.

No comments