Header Ads

Responsive Ads Here

EMAT Yaanza Mafunzo ya Kuokoa Maisha ya Wagonjwa Mahututi Nchini


001
Dkt. Kilalo Mjema wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akitoa mafunzo jinsi ya kuokoa maisha ya mtoto mdogo kwa washiriki mbalimbali.

002
Washiriki mbalimbali wakimsikiliza Dkt. Ramadhani Juma wa hospitali hiyo wakati akitoa mafunzo ya vifaa gani vinapaswa kutumika kwa mgonjwa mwenye tatizo la kupumua.
003
Muuguzi Songoma John wa Muhimbili akiwaeleza washiriki jinsi kumpatia huduma mtoto mwenye tatizo katika mfumo wa njia ya hewa (choking)
004
Baadhi ya washiriki wakijifunza mafunzo ya uongozi katika kutoa huduma ya dharura kwa wagonjwa.
005
Dkt. George Dilunga akitoa mafunzo kwa washiriki jinsi ya kumuhudumia mgonjwa mwenye tatizo la kupumua (respiratory failure). 
Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili.
…………
Chama cha Watoa Huduma za Magonjwa ya Dharura Tanzania (EMAT) kwa kushirikiana na   Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Chuo kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) leo wameanza kutoa mafunzo kwa vitendo jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura kwa wataalamu mbalimbali wa afya.
Lengo la mafunzo hayo ni kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya dharura na ajali nchini kwani utoaji bora wa huduma ya magonjwa ya dharura na ajali imesaidia kupunguza vifo kwa zaidi ya asilimia 45 duniani.
Kwa mujibu wa Rais wa EMAT, Dkt. Hendry Sawe, mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika katika kampasi za Muhimbili, MUHAS na Hospitali ya Aga Khan na kwamba yanahusisha watoa huduma zaidi ya 150 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.
Dkt. Sawe amesema lengo la kuu la mafunzo kwa njia ya vitendo ambayo yameanza kutolewa leo hadi kesho ni kuwawezesha watoa huduma nchini kuwa tayari kutoa huduma za kuokoa maisha kwa kutumia mbinu  mbalimbali za kitaalamu kwenye hospitali zao.
“EMAT kwa kushirikiana Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wadau wengine, tunatimiza lengo la kuwa na huduma bora za tiba ya dharura kwa Watanzania wote, hivyo mafunzo haya ni hatua muhimu sana ya kutimiza malengo hayo,” amesema Dkt. Sawe.
Rais huyo amesema mafunzo hayo pamoja na mkutano yanaratibiwa na EMAT kwa kushirikiana na MHN, MUHAS, Aga Khan, MSD, Abbot Fund Tanzania,  Stanbic Bank, MOKAS na Dkt. Ntuyabaliwe Foundation.
Naye Katibu wa EMAT ambaye ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Juma Mfinanga amesema kuwapo kwa wataalamu waliobobea katika kutoa huduma za dharura na ajali, kumesaidia kuboresha huduma katika hospitali hiyo na kupunguza vifo kwa zaidi ya asilimia tano. 
Katika hatua nyingine, Dkt. Pendo George ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mkutano huo amesema washiriki wanafundishwa jinsi ya kutumia vifaa vichache vilivyopo wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura.
“Kama unataka kumpima mgonjwa mapigo ya moyo na kukuna mashine, daktari au muuguzi anapaswa kutumia njia mbadala ili kuokoa maisha ya mgonjwa,”amesema Dkt. Pendo.
Mratibu wa mafunzo hayo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dkt. Irene Kulola amesema washiriki wote watapata mafunzo stahiki ili kuokoa maisha ya kila mtanzania nchini. Amesema washiriki kutoka mikoa mbalimbali na  nchi za jirani wamehudhuria mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuhitimishwa na kongamano kuu la kisayasi ‘Tanzanian Conference on Emergency Medicine’ ambalo litafanyika Ijumaa wiki hii tarehe 13/10/2017 kwenye ukumbi wa mikutano wa LAPF, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam. Mgeni Rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya.

No comments