Header Ads

Responsive Ads Here

EMAT, Muhimbili Wapongezwa Kwa Kutekeleza Mikakati ya Serikali


001
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza katika mkutano wa Chama cha Watoa Huduma za Magonjwa ya Dharura Tanzania (EMAT) ambao umefanyika jijini Dar es Salaam leo.

002
Baadhi ya washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi wakiwa kwenye mkutano huo leo.
003
Rais wa EMAT, Dkt. Hendry Sawe akieleza juhudi zilizofanywa na chama hicho katika kutoa mafunzo kwa wataalamu wa magonjwa ya dharura na ajali nchini.
004
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Rais wa EMAT leo jijini Dar es Salaam.
005
Mkurugenzi wa Mpango Endelevu wa Abbot Foundation, Dkt. Feato Kayandabila akiueleza mkutano huo jinsi mfuko huo unavyoshirikiana na EMAT katika kutoa mafunzo kwa wataalamu wa magonjwa ya dharura na ajali nchini.
006
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki.
Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
………….
Serikali imekipongeza Chama cha Watoa Huduma za Magonjwa ya Dharura Tanzania (EMAT) kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kuendelea kutekeleza mpango wa Serikali wa kutoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi nchini.
Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo madaktari na wauguzi kutoka hospitali za mikoani na wilayani ili  kutoa huduma bora kwa wagonjwa mahututi na ajali.
EMAT, MNH, MUHAS pamoja na wadau mbalimbali ilianza kutoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa kuhakikisha inaokoa maisha ya wagonjwa wa dharura na ajali kupitia wataalamu wa Afya  waliopo mikoani na wilayani.
Akifungua Mkutano wa EMAT, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kwa kuwa dharura hutokea mahali popote na kwa kila mtu ni muhimu sababu mpango huo umekuwa ukiokoa maisha ya wagonjwa kwa  zaidi asilimia 45.
“Najivunia kuona kazi kubwa inayofanywa na EMAT ambayo inasaidia kutekeleza mpango wa Serikali wa kusambaza huduma za dharura hapa nchini. Serikali inatambua juhudi zenu na tunawahakikishia tutaendelea kuwaunga mkono ili muendelee kuboresha huduma za dharura nchini,” alisema Dkt. Mpoki.
Katibu Mkuu amesema ili kuhakikisha wagonjwa mahututi wanaendelea kuokolewa, Serikali imewasomesha wataalamu bingwa wa magonjwa ya dharura na ajali 27 ambao wanafanya kazi katika hospitali mbalimbali nchini.
Amesema Serikali itaendelea kuwasomesha wataalamu zaidi wa huduma ya dharura na ajali ili kuhakikisha kila mkoa unakuwa wataalamu bingwa wa huma hiyo.
“Sasa hivi tutafungua idara ya magonjwa ya dharura na ajali katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Mkoa ya Maount Meru Arusha na baadaye kwenda katika hospitali za mikoa na wilaya nchini,” amesema.
Rais wa EMAT, Dkt. Hendry Sawe amesema chama hicho kimejiwekea malengo  kwa kushirikiana Wizara ya Afya na wadau wengine ili kutimiza lengo la kuwa na huduma bora za tiba ya dharura kwa Watanzania wote.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Dkt. Upendo George amesema EMAT ikishirikiana na MNH, MUHAS, Abbot Fund Tanzania Stanbic Bank, MSD, Dkt. Ntuyabaliwe Foundation, Aga Khan na MOKAS imetoa mafunzo ya siku mbili kwa washiriki zaidi ya 150 kutoka hospitali mbalimbali nchini ili kuwawezesha kutumia vifaa vichache vilivyopo wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dkt. Irene Kulola amesema  washiriki wote  kutoka sehemu mbalimbali nchini wamepatiwa  mafunzo stahiki ili waweze kuwafundisha wenzao jinsi ya  kuokoa maisha kwa wagonjwa wa dharura na ajali.
Naye Katibu wa EMAT ambaye ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali Muhimbili, Dkt. Juma Mfinanga amesema kuwapo kwa wataalamu waliobobea katika kutoa huduma za dharura na ajali katika hospitali hiyo kumesaidia kuboresha huduma na kupunguza vifo.

No comments