Header Ads

Responsive Ads Here

CHUPA ZA DAMU 400 ZAKUSANYWA MWANZA


DSC03876 .Meneja wa Kituo cha Nitetee
Meneja wa Kituo cha kulea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha Nitetee Foundation, Johansen Emmanuel akipima shinikizo la dmu kabla ya kutolewa damu katika uchangiaji damu wa hiari wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ashura jijini Mwanza 

DSC03881 Uchangiaji damu
Mkurugenzi wa Chuo cha Urembo cha NIFO Beauty College cha jijini Mwanza Flora Lauwo katikakati akichangia damu katika maadhimisho ya Siku ya Ashura.Kulia ni Zawadi Mihayo na kushoto ni Hadija Hussein ambao ni wanafunzi wa chuo hicho.Jumla ya chupa 445 zilikusanywa jana.
DSC03884. Wanafunzi wa chuo cha Urembo wakichangia damu
Wanafunzi wa Chuo cha Urembo cha NIFO Beauty College cha jijini Mwanza Happyness Corneli kulia na Hadija Hussein wakitoa damu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ashura yaliyofanyika jana ikiwa ni kumbukumbu ya kifo cha Imamu Hussein (A.S) na mwanzo wa mwaka wa Kiislamu.
DSC03894 .Maualana Sheikh Bakriy akichangia damu
Maulana Sheikh Seyyid Abass Bakriy (kulia) akitolewa damu katika maadhimisho ya Siku ya Ashura yaliyofanyika jijini Mwanza jana kwa jamii na waumini wa dini ya Kiislamu kuchangia damu kwa hiari.Kushoto ni Sulemani Mpuhu.

 
Na Baltazar Mashaka, Mwanza
 
Taasisi za The Desk & Chair Foundation Tawi la Tanzania na The Bilal Muslim Mission of Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Damu Salama Kanda ya Ziwa zimekusanya chupa 445 za damu.

Zoezi hilo la kuchagia damu kwa hiari ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Ashura kuashiria kuanza kwa mwaka wa Kiislamu lakini pia ni kumbukumbu ya kuuawa kwa Imam aliyeuawa huko katika Jangwa la Karbala nchini Iraq.

Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation Alhaji Sibtain Meghjee ambaye pia ni mwenyeiti wa Bilal Muslim alisema jamii inatakiwa kubadili mitizamo hasi na kuona umuhimu wa kujitolea kwa hiari kuchangia damu kuwa ni jambo la kheri ili kuokoa maisha ya watu wengine na itumie sikukuu kubwa za Pasaka, Krismasi na nyingine, zikiwemo sherehe za arusi kuchangia damu.

“Kuchangia damu kutasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na ukosefu wa damu.Watu wajitolee iwe ni wakati wa huzuni na furaha,wazitumie siku kuu kubwa kuchangia damu na kufanya hivyo watakuwa wamefanya jambo jema na urithi wa kukumbukwa na jamii,”alisema.

Alhaji Meghjee alieleza kushangazwa na baadhi ya watu kuhoji kuwa wanapochangia damu wananufaika na nini ilhali wakifahamu damu haina kiwanda, haizalishwi popote zaidi ya binadamu mwenyewe na hivyo wanaunga mkono agizo la Wazitri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee  na Watoto la kuchangia damu kwa hiari.

Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Chuo cha Urembo cha NIFO Beauty College Flora Lauwo alisema kuwa amefanya kazi nyingi za jamii na kubaini watu wengi hawataki kuchangia damu kutokana na hofu ya afya zao  kutokana na kukosa elimu ya kustosha.

Alishauri kutokana na watu wengi kupoteza maisha sababu ya ukosefu wa damu serikali kutunga sheria ili kila mtu mwenye afya njema achangie damu licha ya kuwepo kwa tatizo la ukosefu wa elimu kwenye jamii yenyewe kutokuona jambo hilo ni muhimu .

Katika zoezi hilo Lauwo alikuwa miongoni mwa wachangiaji wa damu, wakiwemo wanafunzi 50 wa chuo hicho cha urembo cha NIFO Beauty na kwamba wameguswa na zoezi hilo kutokana na mtoto mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Musa anayesumbuliwa na tatizo la saratani ya damu na hivyo kuhitaji kuongezewa kila mara.

Aidha, Kiongozi wa Shia Khoja Ithna Asheri Mwanza Maulana Sheikh Seyyid Amiri Abass Bakriy alishauri Watanzania bila kujali imani zao za dini wala makabila yao kujitoa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watoto, wajawazito na watu maradhi mengine kwa sababu ukichangia damu ili kuokoa mtu mmoja utakuwa umeokoa maisha ya watu wengi.

“Ukijitolea kwa Siku hii ya kumbukumbu ya Imam Hussein utapata thawabu zaidi na unavyodhani.Hivyo Watanzania msiogope kuchangia damu kwa kuwa ni muda mfupi tu wa kujitolea damu hiyo na inarudi kwa kasi,”alisema.

Maulana Bakriy aliongeza kuwa katika maadhimisho hayo ya Siku ya Ashura ni mfano wa kuigwa na wapenda haki, ukweli, heshima, uadilifu na usawa kwenye jamii zetu katika kuondoa dhuluma, unafiki na ujinga kwa kuwatia moyo waumini na wanyonge wanaokandamizwa.

No comments