Header Ads

Responsive Ads Here

CCM ZANZIBAR YATAKA PEMBEJEO WANAZOPEWA WAKULIMA ZIWE NA VIWANGO.


1
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma
Mabodi akiwahutubia wakulima na wananchi katika uzinduzi wa kilimo cha
mpunga bonde la mahekani huko Kizimbani Unguja.

2 (1)
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Mabodi
akizindua kilimo cha mpunga kwa kuendesha Tirekta akiashiria kuanza
kwa shughuli za kilimo hicho uko katika bonde hilo.
3
Mbunge wa Jimbo la Bububu Mh. Mwantakaje Haji Juma
akizungumza na wakulima hao katika hafla ya uzinduzi wa kilimo cha
mpunga.
4
Ni Baadhi ya wakulima na wananchi walioudhuria katika
hafla hiyo ya uzinduzi wa kilimo cha mpunga katika mabonde ya mpunga
yaliyomokatika jimbo la Bububu.
Na Is-haka Omar, Zanzibar.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi ameishauri
serikali kuhakikisha Pembejeo za kilimo wanazouziwa wakulima zinakuwa
na viwango vinavyoendana na mazingira ya kilimo yaliyopo nchini.
Ushauri huo ameutoa jana wakati akizindua msimu wa kilimo cha Mpunga
katika mabonde yaliyopo katika Jimbo la Bububu na vitongozi vyake uko
katika bonde la Mahakani lililopo katika kijiji cha Kizimbani Wilaya
ya magharibi “A” .

Alisema wananchi wengi wanafanya shughuli za kilimo katika mazingira
magumu hivyo ni lazima taasisi za umma zinazohusika na kuuza pembejeo
za kilimo ambazo ni mbolea, dawa na mbegu kuwa makini kwa kuhakikisha
bidhaa hizo zinakidhi vigezo vya kilimo ili kuepusha hasara kwa
wakulima.
Dkt. Mabodi alitoa ufafanuzi huo baada ya Mwakilishi wa jimbo la
Bububu, Mh. Masoud Abrahman Masoud kueleza kuwa katika msimu wa kilimo
ulipita baadhi ya wakulima wanaolima mpunga katika mabonde ya mpunga
ya jimbo hilo walipata walikosa mavuno kutokana na mpunga kukauka kwa
sababu ya kutumia pembejeo mbovu zisizokuwa na viwango.

“Nitakaa na viongozi wa Wizara husika kwa lengo la kuwaeleza
changamoto hiyo nao waweze kuifanyia kazi ili isiweze kujitokeza
katika misimu ijayo.”, alifafanua Dk. Mabodi na kuwasihi wakulima
wasivunjike moyo kwani serikali yao ni makini na ina dhamira ya
kuhakikisha ardhi ndogo iliyopo inatumika kwa kilimo cha kisasa.

Alieleza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 imeahidi
kuisimamia serikali kuhakikisha inaweka miondombinu endelevu ya kilimo
itakayosaidia Zanzibar kulima mazao ya aina mbali mbali hasa mpunga
kwa lengo la kupunguza uagizishiaji wa chakula kutoka nje ya nchi.
Alisisitiza wakulima hao kuhakikisha wanaendelea kufanya maandalizi
mapema ya msimu wa kilimo cha mpunga na mazao mengine ili kwenda
sambamba na msimu wa mvua kwa lengo la kupata mavuno mengi.
Hata hivyo aliwasihi kuwatumia wataalamu wa kilimo ili waweze kutoa
ushauri wao juu ya mbegu zinazostahili kupandwa kwa mujibu wa maeneo
husika ya kilimo.

Aliwapongeza viongozi wa Jimbo la Bububu ambao ni Mbunge, Mwakilishi
na Madiwani kwa ushirikiano wao unaozaa matunda ya kutekeleza ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020  kwa vitendo kwa kuanzisha mradi wa
kilimo cha mpunga unaowanufaisha wakulima wengi wa jimbo hilo.

Akizungumzia uchaguzi unaondelea ndani ya CCM Dk.Mabodi alisema
msimamo wa chama hicho ni kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa wanakuwa
ni viongozi safi kimatendo, kimaadili na wanaokubalika katika jamii na
wenye uwezo wa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa dola wa  mwaka 2020.

” Ajenda ya wapinzani ni kuzungumzia uchaguzi uliopita na kuzua na
kuaminishana mambo ambayo hayawezekani kutekelezeka lakini CCM kazi
yetu kubwa ni kuwapelekea maendeleo wanachama wetu popote walipo nasi
tunawafikia”, alisema Dk. Mabodi.
Sambamba na hayo Dk.Mabodi aliahidi kuchangia nusu ya fedha za kununua
tirekta ndogo aina ya powertiller ili iweze kuwasaidia wakulima hao
katika shughuli za kilimo.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Mh. Mwantakaje Haji Juma alisema mradi huo
wa kilimo cha mpunga umeendeshwa kwa awamu tatu na kuwapatia wananchi
mafanikio makubwa ya chakula na awamu ya sasa jumla ya shilingi
milioni 16 zinatarajia kutumika fedha zitakazotolewa na mbunge na
mwakilishi wa jimbo hilo.

Akisoma risala kwa niaba ya wakulima wa jimbo hilo, Bw. Saleh Said
Njonjo alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na
kupunguziwa bei ya pembejeo za kilimo pamoja na kupunguziwa bei ya
kulimiwa na matrekita ya serikali katika mabonde yao.

Hata hivyo alisema kuwa jumla ya wakulima 723 wa jimbo hilo na maeneo
jirani watanufaika na mradi huo wa kilimo cha mpunga katika mabonde ya
Mahekani, Tomokani, Mkanyageni, Mkuruwinda, Ndagoni, Mbuyuni Dole,
Kichakani Bumbwisudi, Shamba ndogo, chemchem, kipanga na saraya.

Kwa upande wake mkulima wa bonde la mahekani, Bw. Abdalla Haji Abdalla
amesifu juhudi za viongozi wa jimbo la Bububu kwa kuwajali wakulima wa
jimbo hilo na kuelezea kuwa yeye ni mmoja kati ya watu walionufaika na
mradi wa kilimo cha mbunga kwa awamu mbili zilizopita.

No comments