Header Ads

Responsive Ads Here

WAZIRI JAFO ATOA SIKU SABA KWA MTENDAJI MKUU WA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA KUANZA KUTEKELEZA UJENZI WA MRADI WA ULIOKUWA UMEKWAMA


1
Naibu Waziri wa Tamisemi Seleman Jafo akisalimiana kwa kumpa mkono  mmoja wa wagonjwa mara alipofanya ziara yake ya  kushtukiza katika hospitali ya tumbi kwaa ajili ya kuweza kufanya ukaguzi katika  mradi wa upanuzi wa  hospitali hiyo.

PICHA NA VICTOR MASANGU
NA VICTOR MASANGU, KIBAHA 
NAIBU Waziri wa Tamisemi Seleman Jafo amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa Tumbi  na kutoa muda wa wiki moja kwa mtendaji mkuu wa Shirika la elimu Kibaha kuanza mara moja  ujenzi kwa ajili ya mradi wa  upanuzi wa majengo  baada ya kubaini umekwama kwa kipindi cha  miaka  saba bila ya kuendelezwa kitu chochote hali ambayo imesababisha kwa sasa eneo hilo  kuota nyasi na kugeuka  kuwa vichaka.
Jafo akizungumza kwa masikitiko makubwa  na baadhi ya watumishi wa hospitali ya Tumbi,pamoja na viongozi waandamizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani amechukizwa kuona  mradi huo kutelekezwa na kusababisha miundombinu yake ya  majengo  kuchakaa kabla hata ya kuanza kutumika kitendo ambacho amekilaani vikali na kusema suala hilo hawezi kulifumbia macho  hata kidogo.
Jafo alibainisha kuwa serikali tayari  imeshatoa kiasi cha shilingi milioni 600 na fedha hiyo imeshaingizwa katika Ofisi ya Ras Pwani tangu mwaka jana  kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo lakini anashangazwa kuona mradi huo kusimama, hivyo amewaagiza watendaji wa  mamlaka zinazohusika kukutana na kuliweka sawa jambo hilo kwa lengo la kuweza kuboresha sekta ya afya.
“Kwa kweli natoa wiki moja kwa mtendaji mkuu kufanya haraka iwezeknavyo mradi huu wa upanuzi ambao ulikuwa umesimama kwa kipindi kirefu kukaa chini na watendaji wenzake wakubaliane na kuweza kuanza mara moja ujenzi huo maana fedha zipo tu na kwamba tayari tumeshazitoa shilingi milioni 600 sasa sijui nini tatizo kwa hiyo wiki ijayao nataka kuona ujenzi huo unaanza kuendelea,”alisema Jafo.
Aidha Jafo alisema kwamba lengo kubwa la serikali ya awamu ya  tano ni kuhakikisha kwamba inaboresha huduma ya matibabu kwa wananchi wote hivyo asingependa  kuona baadhi ya watu wanarudisha nyuma juhudi za serikali  katika kuboresha sekta ya afya katika maeneo mbali mbali ya Tanzania.
Kutokana na agizo hilo la Naibu Waziri  mwandishi wa habari hizi  aliweza  kubisha hodi na kuweza  kuzungumza  na Kaimu Mkurugenzi mkuu   wa shirika la elimu Kibaha  Robert Shilingi  amebainisha kuwa  vikwazo na  changamoto  kubwa zinazopelekea kukwama  kwa mradi wa ujenzi wa upanuzi wa hospitali ya Mkoa ya Tumbi ni ukata wa fedha ambao ulikuwa unawakabili hivyo kupelekea ujenzi kutokamilika kwa wakati.
Naye Kaimu afisa miliki wa shirika la elimu Kibaha Injinia  Zacharia Mwinuka ambaye pia ndiye alikuwa anasimamia ujenzi  amesema kwamba mradi huo wa upanuzi ulianza tangu mwaka 2009 na kufafanua zaidi sababu nyingine ni kuwepo kwa ufinyu wa bajeti pamoja  na ucheleweshwaji wa fedha kutoka serikalini.
MRADI huo wa ujenzi kwa ajili ya upanuzi wa  hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa Tumbi ulianza utekelezaji wake tangu  mnamo mwaka 2009 na ulitarajiwa kukamilika kwa kipindi cha miaka mitatu lakini hadi kufikia mwaka   huu wa 2017  bado haujamalizika na miundombinu yake ya  majengo  tayari imeshaanza kuchakaa licha ya serikali ya awamu ya tano kutoa kiasi cha shilingi 600 kwa ajili ya ujenzi huo.

No comments