Header Ads

Responsive Ads Here

WATUMISHI WANAOTOA HUDUMA WAMETAKIWA KUTOA TAARIFA ZA MAPATO NA MATUMIZI KWA WAKATI


PMO_9572
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
Serikali imewataka watumishi wa Mikoa, Halmashauri na vituo vya kutolea huduma na kutoa taarifa za mapato na matumizi kwa wakati kwa wananchi katika maeneo yao.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa wakati akizindua Mfumo wa Kielektroniki wa Kuandaa Mipango, Bajeti na Ripoti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (PlanRep) iliyoboreshwa na Mfumo Mpya wa Uhasibu na Utoaji Taarifa (FFARS) leo mjini Dodoma.
“Ukamilishaji wa mifumo hii utasaidia kuongeza uwazi, uwajibikaji kwa watumshi hasa katika eneo la mapokezi na matumzi ya fedha za umma kuanzia katika vituo vya kutolea huduma mpaka ngazi ya Halmashauri”.
 “Kuanzia sasa sitegemei kuona kituo chochote cha kutolea huduma kilichopo chini ya Halmashauri kinakuwa na matumizi yasiozingatia taratibu na kanuni za fedha au kubadilisha matumizi ya fedha bila kuwasiliana na Mamlaka husika” amesisitiza Waziri Mkuu.
Aidha, alisema kuwa lengo la matumizi ya mifumo ya TEHAMA ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali na zisitumike kukwamisha shughuli na utaratibu wa kazi za Serikali.
Vilevile, Waziri Mkuu alisema kuwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kipindi kirefu imekuwa ikitumia gharama kubwa, muda mwingi katika kukamilisha zoezi zima la uandaaji wa Mipango, Bajeti. Hivyo kupitia mfumo changamoto hizo zimetatuliwa.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI George Simbachawene amesema kuwa kupitia mfumo huo umeweza kuokoa zaidi ya Shilingi Bilioni nne gharama ya Serikali zilizokuwa zikitumika kila mwaka kwa ajili ya kufanya maandalizi ya kuandaa bajeti.
“Mifumo hii itasaidia kutaleta ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa huduma kwa wananchi, utasaidia kupunguza muda na kuleta maendeleo kwa kasi na pia utasaidia kutunza taarifa ya mapato yote katika ngazi ya Halmashauri” ameongeza George Simbachawene.
Naye Kaimu Balozi wa Marekani nchini Imni Patterson amesema kuwa pamoja mifumo hiyo itaongeza ufanisi na kuboresha usimamizi wa fedha na kuwezesha Serikali ya Tanzania kutoa fedha kwa malengo yaliyokusudiwa na mahitaji ya wananchi kwa ufasaha.
“Marekani inajivunia kushirikiana na Tanzania, mnapofanya kazi kwa malengo ya kuwa na Serikali yenye uwazi, maendeleo endelevu na ustawi wa pamoja” amesema Kaimu Balozi wa Marekani nchini.
Akitoa salamu, Mkurugenzi wa Mradi wa PS3 Dkt. Emmanuel Malangalila amesmea kuwa mifumo hiyo imeundwa na kutengenezwa na vijana wa Kitanzania kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI wakishirikiana na watumishi wa mradi wa uimarishaji wa mifumo ya sekta ya umma (PS3).
“Mifumo hii miwili itaimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa matumizi ya fedha katika Halmshauri na ngazi za vituo vya kutolea huduma na hivyo utoaji wa huduma kwa wananchi kuboreka zaidi” amesema Dkt. Malangalila.
Mradi wa uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) ni mradi wa miaka mitano ulioanza Julai 2015 na kumalizika 2020 na unafanya kazi katika Halmashauri 93 katika mikoa 13 Tanzania Bara ikiwa na lengo la kutoa msaada wa kitaalamu kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya Serikali katika ngazi ya Taifa na Halmashauri ili kuboresha utoaji wa huduma za jamii.

No comments