Header Ads

Responsive Ads Here

WATAHINIWA ZAIDI YA ELFU SABA WAONGEZEKA MTIHANI WA DARASA LA SABA MKOA WA SINGIDA


1
Mmoja kati ya Wanafunzi wa shule ya Msingi Mahembe Manispaa ya Singida akifanya mitihani ya kumaliza elimu ya Msingi.


Idadi ya Watahiniwa wa mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi Mkoa wa Singida inayoanza leo imeongezeka hadi kufikia wanafunzi 28,947 kutoka wanafunzi 21, 417 waliofanya mitihani hiyo hiyo mwaka jana.
Ongezeko hilo la wanafunzi 7,530 ni kiashiria cha kuboreshwa kwa elimu na usimamizi wa sekta ya elimu msingi kwa Mkoa wa Singida pamoja na jitihada za wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria masomo yao ipasavyo.
Hayo yamebainishwa leo na Afisa Elimu Mkoa wa Singida Florian Kimolo ambaye amefafanua kuwa jumla ya wasichana 15,964 na wavulana 12,984 wameanza mitihani ya darasa la saba mkoa wa Singida kwa kufanya mtihani wa Kiingereza ukifuatiwa na mtihani wa Hisabati.
Kimolo ameeleza kuwa ongezo la wanafunzi wanaofanya mitihani inaweza kusababishwa na idadi kubwa ya udahili kwa mwaka walioanza darasa la kwanza wanafunzi hao, lakini pia sababu nyingine kubwa ni usimamizi mzuri katika sekta hiyo ili kupunguza utoro na wanafunzi wanaoacha shule.
Amefafanua kuwa wanafunzi wanaweza kudahiliwa wengi lakini wakamaliza wachache kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro, kuacha shule, uhamisho, na vifo hivyo idadi ikiongezeka ya watahiniwa ni ishara kuwa walimu, wazazi/walezi na idara za elimu ngazi zote zimefanya kazi nzuri ya kusimamia sekta hiyo.
Kimolo amesema mitihani imeanza kufanyika kwa amani na utulivu kutokana kuwa ofisi yake imefanya maadalizi mapema kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na halmashauri zote za Mkoa wa Singida.
Aidha amewataka wasimamizi kuzingatia maadili, kanuni na sheria walizoelekezwa wakati wa semina za usimamizi ili mitihani ifanyike kwa haki bila ya matatizo yoyote.
Kimolo ameongeza kuwa jumla ya vituo vya kufanyia mitihani hiyo kwa mkoa wa Singida ni 518 huku mikondo ikiwa 1313 huku akiwasisitiza wanafunzi hao kufanya mitihani kwa amani na nidhamu.

No comments