Header Ads

Responsive Ads Here

TUWASA YAJA NA DAWA KUWABANA WADAIWA SUGU

Na Tiganya Vincent
RS –TABORA
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imesema kuwa mfumo mpya wa  malipo kabla ya kupata huduma ya maji ulioanzishwa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka ya Mjini Tabora (TUWASA) utasaidia kuiondolea usumbufu wa kudai fedha zake kutoka kwa wateja ambao wamekuwa hawataki kulipia maji kwa wakati.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati uzinduzi wa mfumo mpya wa ulipiaji maji kabla ya matumizi katika Manispaa ya Tabora ambao mteja wa TUWASA atapata maji baada ya kulipa kupitia  simu yake ya mkononi au  Benki ya NMB.
Alisema kuwa mfumo wa zamani ulikuwa unatoa mwanya kwa baadhi ya wateja kuendelea kunufaika na huduma upatikanaji wa maji kwa kulipia wakati mwingine fedha kidogo kinyume cha maji aliyotumia.
Mwanri aliongeza kuwa mfumo utasaidia pia kulta nidhamu katika matumizi ya maji na uwajibikaji katika malipo ili ndio upate huduma la sivyo mteja atakosa huduma hiyo.
“Kwa kweli hivi sasa mumekuja na dawa ya wateja sugu waliokuwa hawataki kulipa sasa wamepatikana …na hakutakuwepo na madeni mapya yanayotokana na wateja kuchelewa kulipa bila kwani mambo yatakuwa papo kwa papo ndio upate huduma” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alizitaka taasisi za umma zinazodaiwa kuhakikisha zinalipa ili Mamlaka hiyo izitumie fedha hizo katika kuboresha zaidi huduma kwa wananchi wengine ambao hawajafikiwa na maji ya bomba.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA  Mkama Bwire alisema kuwa Mamlaka hiyo inawadai wateja wake zaidi bilioni 3.3 na kufanya Mamlaka hiyo kuwa na wakati mgumu wa kutoa huduma kwa wateja wake wanapohitaji fedha ambazo haziko mkononi mwao.
Alitaja makundi ya wanadaiwa hao kuwa ni taasisi za umma shilingi bilioni 2.8, wateja wengine milioni 427 na wafanyabiashara milioni 88.
Bwire alisema kuwa deni hilo limesababisha kukwama kwa mipango mingi ya kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji ikiwemo kusababisha nao wadaiwe na Shirika la Ugavi wa Umeme la Taifa (TANESCO ) .
Alisema kuwa uzinduzi wa mita hizo za kulipa kabla ya kupata huduma zitawasaidia kukabiliana na wadaiwa sugu na kuondokana na usumbufu wa kufuatilia madeni  na hvyo  kuokoa muda kwa wateja wake na nauli ambazo wateja wamekuwa wakitumia kwenda kulipia bili zao.
Akizungumzia hali ya uzalishaji maji kwa Mamlaka hiyo Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TUWASA alisema kuwa uhaba wa mvua zilizonyesha msimu uliopita na uharibifu wa vyanzo vya maji vinavyoingiza maji katika Bwawa la Kazima na lile la Igombe limesababisha kuwepo na mgao wa Maji katika Manispaa ya Tabora.
Bwire alisema  kuwa kina cha maji kimeshuka na kufanya kuwepo na tope jingi katika maji na hivyo kulazimika kutumia dawa za gharama kubwa kwa ajili ya usafishaji tope na uuaji wa wadudu katika maji.
Alisema kuwa hivi sasa wanatumia milioni 140 kwa mwezi kutoka milioni 60 walizokuwa wakitumia hapo awali katika kipindi kama hicho  wakati wa maji mengi katika mabwawa hayo.
Naye Meneja Biashara wa TUWASA Bernard Biswalo alisema kuwa kupitia mfumo mpya wa malipo ya kabla ya matumizi ya maji mteja atalazimika kulipia kupitia mitandao Tigo Pesa , M-PESA na Benki ya NMB ili ndio aanze kupata huduma hiyo.

No comments