Header Ads

Responsive Ads Here

SMZ KUONDOSHA MICHANGO KWA WANAFUNZI WA SEKONDARI KUANZIA MWKA WA FEDHA UJAO

Na Ramadhani Ali – Maelezo             
RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Muhamed Shein  ametangaza kuondoshwa michango ya wanafunzi wa Skuli za Sekondari kuanzia mwaka ujao wa Fedha 2017/2018.

Akizungumza na walimu, wanafunzi na wananchi katika tamasha la 53 la Elimu bila Malipo katika kiwanja cha Gombani Pemba, Rais Shein alisema uamuzi huo ni kutekeleza azma ya muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume ya Elimu bila malipo kwa wananchi wote wa Zanzibar.
Alisema azma hiyo ilitekelezwa kikamilifu kwa miaka mingi lakini kutokana na changamoto zililzojitokeza wazee walitakiwa kuchangia kiwango kidogo cha fedha na kitaondoshwa kuanzia mwezi Julai mwakani.
Aliziagiza Wizara ya Elimu na Wizara ya Fedha kushirikiana katika kuandaa bajeti ambayo itakidhi matakwa ya kuondolewa michango ya wanafunzi wa skuli za Sekondari.
“Azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuondosha michango ya wazazi katika elimu ya maandalizi, msingi na sekondari na fedha za kutimiza lengo hilo tunazo, ”Dkt. Shein alisisitiza.
Hata hivyo alisema elimu ya vyuo vikuu Serikali
itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wote wenye sifa bila ya riba ili kuhakikisha hakuna kijana atakaeshindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu kutokana na kukosa fedha.
Dkt. Shein aliwahimiza walimu kutekeleza wajibu wao wa kusomesha kwa mujibu wa sheria na kufuata maadili ya kazi hiyo na kutumia fursa ya kuwepo vyuo vingi vinavyotoa elimu ya juu kujiendeleza kielimu.
Alisema serikali imekusudia kuongeza ubora wa elimu kwa kujenga majengo mapya ya kisasa, kuyafanyia matengeneza ya zamani pamoja na kuongeza vifaa vya kufundishia na vifaa vya maabara kwa skuli za sekondari.
Kwa upande wa wanafunzi Dkt. Shein aliwataka kutekeleza wajibu wao wa kusoma kwa bidii na kuwa waangalifu katika kutumia Teknolojia ya habari kwani inaweza kuwaongoza ama kuwapotosha watakapoitumia vibaya.
Akizungumzia kurejeshwa vuguvugu la michezo katika Tamasha la Elimu bila Malipo, alisema ni kuibua na kuiviendeleza vipaji vya vijana  na kujenga maelewano na urafiki kati ya wanafunzi wa skuli mbali mbali za Unguja na Pemba.
Akimkaribisha Rais kuhutubia wanafunzi na walimu katika Tamasha hilo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alisema Wizara itasimamia kikamilifu uwajibika ndani ya taasisi zilizomo ndani ya Wizara na itahakiisha mwalimu atakaeshindwa kutekeleza wajibu wake sheria zitamuandamana.
Tamasha la 53 la Elimu bila malipo linalofanyika kwa zamu kati ya  Unguja na Pemba mwaka huu ilikuwa zamu ya Pemba na liliwakutanisha zaidi ya wanafunzi  2,000 na walimu wao kutoka skuli mbali mbali.              
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO

No comments