Header Ads

Responsive Ads Here

SERIKALI KUENDELEA KUTOA FEDHA ZA BAJETI KWA MIRADI YA MAENDELEO

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
Serikali itaendelea kutoa fedha zaidi za Bajeti kwa miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya kipaumbele kwa kadri inavyoendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati akiahirisha Mkutano wa Nane wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Mjini Dodoma.
“Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2017/2018, aidha mwenendo wa utekelezaji unaridhisha. Serikali imeweka jitihada kubwa za kuimarisha ukusanyaji mapato ya ndani kwa kutumia mifumo ya kielektroniki” amefafanua Waziri Mkuu.
Katika hatua hiyo Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Agosti, 2017 Serikali imetoa jumla ya Shilingi Trilion 3.944 zinazotokana na mapato ya ndani na fedha za nje kwa matumizi ya Serikali ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ulipaji wa mishahara ya watumishi wa umma na Deni Taifa.
Aidha, Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa Serikali itahakikisha kila kituo cha kutolea huduma za afya nchini kinakuwa na vifaa vya kutosha ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini imeendelea kuimarika” ameongeza Mhe. Majaliwa.
Akizungumzia suala la elimu, Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea na mpango wa Elimu bila malipo kwa kupeleka fedha moja kwa moja katika shule za Umma za Msingi na Sekondari nchi nzima.
Kwa upande wa Kilimo Waziri Mkuu amesema kuwa, Serikali imeamua kuanza kwa kuweka mkazo wa kuyaendeleza kwa kasi mazao makuu matano ya biashara yakiwemo Pamba, Tumbaku, Korosho, Chai na Kahawa.
Waziri Mkuu ameahirisha rasmi Bunge la Jamburi ya Muungano wa Tanzania mpaka Novemba 7, 2017.

No comments