Header Ads

Responsive Ads Here

RC TABORA MKANDARASI ALIYESABABISHA HASARA YA MILIONI 50 KATIKA UJENZI WA CHOO CHA MILAMBO ATAFUTWE POPOTE ALIPO.


RC TBRR
Na Tiganya Vincent.-RS-Tabora
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeagizwa kutafuta na kuletwa Mkandarasi na Mshauri wa Mkandarasi aliyehusika na ujenzi wa Choo katika Shule ya Sekondari ya Milambo na kusababisha hasara ya shilingi milioni 50.

Agizo hilo limetolewa jana mjini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mradi wa Miombo ikiwemo ujenzi wa majiko ya kisasa yanayotumia kuni kidogo  na mengine gesi ya chooni.
Alisema kuwa haiwezekani Serikali itumie fedha nyingi hizo kisha choo kititie kwa muda mfupi toka kilipojengwa mwaka 2013.
“Mkandarasi huyo aliyejenga hata kama mnavyosema kuwa ameshastaafu ,nataka ndani ya wiki moja aje na maelezo ofisini kwangu juu ya nani anabeba hii hasara ya jengo kutitia muda mfupi baada ya kukamilika” alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Mwanri alisema kuwa Mshauri huyo ambaye ametajwa kwa jina moja la Kuya na aliyekuwa Mkuu wa Shule hiyo ambaye hivi sasa yuko Urambo na Mkandarasi ni lazima wapeleke maelezo juu ya utaratibu mzima ulitumika katika ujenzi huo.
Alisema kuwa kitendo cha jengo hilo kutitia kimezalisha hasara nyingine ya milioni 18 ambazo Mradi wa Miombo ulikuwa umejenga mtandao wa gesi kwa ajili ya kusafirisha hadi katika jiko la shule hiyo ili liweze kupunguza gharama ya matumizi ya kuni.
Mwanri alisema mradi huo umeshindwa kufanyakazi kwa sababu ya ukosefu wa malighafi ya uzalishalishaji wa gesi kwa matumizi ya jikoni.
Alimwaagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora kuhakikisha anamtafuta popopte alipo aliyekuwa Mkandarasi na Mshauri wake na kumleta ili aweze kueleza kuwa hiyo hasara nani anaibeba.
Mwanri alisema asipokuja kwa hiari yake atalazimika kutumia Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kumsaka na kumleta ili ajibu hoja ya kusababishia hasara Serikali.
Aidha Mkuu wa Mkoa huyo alimwagiza Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Milambo kuhakikisha anasimamisha mara moja matumizi ya Choo hicho kilichotitia ili kisije kinasababisha maafa kwa wanafunzi.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora amewaagiza viongozi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora na Mkurugenzi Mteandaji wa Manispaa ya Tabora kuhakikisha wanakarabati choo cha wasichana ambayo kimesababisha kuzagaa kwa maji taka na kutishia afya za wanafunzi.
Alisema kuwa ndani ya wiki moja kama atakuta kazi hiyo haijatekelezwa atalamizika kuwachukulia hatua Mwalimu Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora kwa kushindwa kujali afya za wanafunzi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora yuko katika kutembelea shughuli mbalimbali zinazofadhiliwa na Mradi wa Miombo ambayo ni pamoja na ujenzi wa majiko ya kisasa yanatumia kuni kidogo, ufugaji nyuki, ufugaji kuku, matumizi ya gesi ya kinyesi kwa ajili ya kupika na mingine mingi.

No comments