Header Ads

Responsive Ads Here

OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU IMEPOKEA TABLETS 500 ZENYE THAMANI YA SH. MILIONI 400 KWA AJILI YA UTAFITI WA MAPATO NA MATUMIZI YA KAYA BINAFSI TANZANIA BARA 2017/18


PICHA NAMBA 1
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa (kushoto) akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhiwa tablets kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kufanyia Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18. Kulia ni Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini Nadia Belhaj Hassine Belghith

PICHA NAMBA 2
Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini Nadia Belhaj Hassine Belghith (kulia) akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhi tablets katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa ajili ya kufanyia Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18. Kulia ni Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mayasa M. Mwinyi.
PICHA NAMBA 3
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa (kushoto) akipokea tablet kutoka kwa Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini Nadia Belhaj Hassine Belghith (kulia) wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekabidhiwa tablets hizo kwa ajili ya kufanyia Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18.
PICHA NAMBA 4
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia hafla ya kukabidhiwa tablets Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutoka Benki ya Dunia leo jijini Dar es Salaam. Ofisi ya Taifa ya Takwimu imepokea tablets hizo kwa ajili ya kufanyia Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18.
PICHA ZOTE NA EMMANUEL GHULA
…………………
Na Emmanuel Ghula
26/09/2017
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imepokea Tablets 500 zenye thamani ya Shillingi milioni 400 kutoka Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya tablets hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amesema kupatikana kwa tablets hizo kutasaidia kurahisisha zoezi la ukusanyaji wa taarifa muhimu za Mapato na Matumizi ya Kaya pamoja na kupunguza gharama ambazo zingetumika kuchapisha madodoso ya karatasi.
“Ofisi ya Taifa ya Takwimu leo tumepokea tablets 500 kutoka Benki ya Dunia ikiwa ni maandalizi ya kuanza kwa Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18. Tablets hizi zitasaidia kurahisisha kazi na kupunguza gharama ambazo tungetumia kuchapisha madodoso ya karatasi,” amesema Dkt. Chuwa.
Dkt. Chuwa amesema utafiti huu utahusisha maeneo wakilishi 796 na kaya wakilishi 9,552 zilizochaguliwa kitaalamu kuweza kutoa matokeo ya viashiria vya umaskini na viashiria vingine.
Amesema utafiti huu utatoa takwimu za msingi kwa viashiria vya kiuchumi na kijamii ambavyo vitasaidia kusimamia na kutathmini mwelekeo wa serikali katika harakati zake za kupunguza umasikini. Taarifa za utafiti huu pia zitasaidia kupima utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Awamu ya Pili (FYDP-II) 2016/17 – 20/21 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs 2030), pamoja na kuwezesha kufanyika kwa tafiti mbalimbali zinazohusu mwenendo wa hali ya umaskini katika ngazi ya Mikoa na Wilaya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia nchini, Bella Bird amesema Benki ya Dunia imetoa tablets hizo kwa NBS ili kurahisisha ukusanyaji wa taarifa kwa kutumia teknolojia ya kisasa badala ya kutumia njia ya madodoso ya karatasi ambayo ni gharama kubwa.
Amesema Benki hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikishirikiana na NBS katika tafiti mbalimbali na hivyo vifaa hivi ni mwendelezo wa ushirikiano huo katika upatikanaji wa takwimu rasmi nchini ambazo pia hutumika kimataifa katika kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Kukamilika kwa utafiti huu kutasaidia kupatikana kwa takwimu rasmi zinazohusu Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi zitakazotumika kwa ajili ya kusimamia na kutathmini program mbalimbali za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.
Utafiti huu unafanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na idara mbalimbali pamoja na Wadau wa Maendeleo.

No comments