Header Ads

Responsive Ads Here

MSHAMA-WAMILIKI WA VIWANJA 943 KUFUTIWA HATI ZAO BAADA YA KUKAIDI AGIZO


SAM_5568
Mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama ,akizungumza jambo na waandishi wa habari ofisini kwake .

Picha na Mwamvua Mwinyi
………………….
Na Mwamvua Mwinyi ,Kibaha
SERIKALI wilayani Kibaha ,mkoani Pwani inatarajia kufuta umiliki wa viwanja vya watu binafsi pamoja na taasisi 943 baada ya kushindwa kutekeleza agizo la kwenda kujisalimisha ndani ya mwezi mmoja wilayani humo ili kueleza mpango kazi kwa kila mmiliki .
Aidha inawaomba wawekezaji kujitokeza kwenda kuwekeza wilayani hapo kwani bado kuna maeneo ya kutosha yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda .
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha ,mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama alisema ,hatua inayofuata sasa ni kupeleka majina yao kwa waziri wa ardhi na maendeleo ya makazi kwa ajili ya kuwafutia umiliki.
Assumpter alisema kuwa tayari ameshaandaa orodha ya wamiliki hao , na wiki hii anaipeleka ili kufanyiwa kazi.
“Wapo baadhi yao wameshindwa kuendeleza kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano na wengine miaka 15 wakati sheria inataka mmiliki kuendeleza eneo ndani ya miaka mitatu na endapo atashindwa kuendeleza unaweza kunyanganywa eneo husika,” alisema Assumpter .
Alieleza viwanja ambavyo havikuendelezwa kabla ya agizo hilo vilikuwa 1,000 ambapo waliojitokeza ni 246 kuelezea mipango yao .
Viwanja vya taasisi ni 189 ambavyo wahusika nao hawajajitokeza.
“Hatuwezi kuwavumilia,mji wetu wa Kibaha ndiyo makao makuu ya mkoa wa Pwani kwa kushindwa kuendeleza maeneo yao hawa tunawafutia umiliki ili wapewe watu wengine,” alisema .
Hata hivyo ,Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wilaya hiyo imedhamiria kuendeleza mji huo hivyo hataki kuona vichaka ambavyo vimekuwa ni moja ya sehemu ambazo watu wanafanyiwa uhalifu.
“Watu wamekuwa wakifanyiwa vitendo mbalimbali ikiwemo wanawake kubakwa, madereva bodaboda kuporwa pikipiki na kuuwawa kutokana na mashamba na viwanja kushindwa kuendelezwa,” alifafanua Assumpter .
Akizungumzia kuhusiana na taasisi za serikali na umma ambazo zilipewa maeneo na kushindwa kuyaendeleza na kuwa hatarini kunyanganywa maeneo hayo alisema yote yamefika na kueleza jinsi gani watakavyoendeleza maeneo hayo.
Agost 10 mwaka huu ,Assumpter alitoa mwezi mmoja kwa kwa taasisi ,makampuni mbalimbali na wananchi waliokumbatia viwanja vyenye hati zaidi ya 1,000 pasipo kuviendeleza kuhakikisha wanafanya hivyo ndani ya muda huo .

No comments