Header Ads

Responsive Ads Here

MKUU WA WILAYA YA CHEMBA APIGA MARUFUKU VIONGOZI WA VIJIJI KUKARIBISHA WAFUGAJI NA MAKUNDI YA MIFUGO


odunga
Na Mwandishi wetu Chemba
Serikali wilayani Chemba mkoa wa Dodoma imewagiza viongozi wa serikali za vijiji, kata na tarafa katika wilaya hiyo kuacha mara moja tabia ya kuwakaribisha wageni kutoka mikoa ya jirani wanaoingia na makundi ya mifugo na kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Chemba mkoani Dodoma Simon Odunga wakati akiongea na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini na akaeleza kuwa mifugo inayoingia kwenye wilaya hiyo pia imekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira katika pori la akiba la Swagaswaga.
Bwana Odunga alisema hivi karibuni zaidi ya ng’ombe 250 walikamatwa wakichunga katika pori la akiba la Swagaswaga kinyume cha sheria za uhifadhi na kwamba serikali itachukua hatua kali dhidi ya wote wanaoingiza mifugo kwenye pori hilo kinyume cha sheria.
Kuhusu wananchi waliowavamia askari wa wanyamapori wakiwa na silaha za jadi ikiwemo mishale ya sumu wakitaka kupora mifugo iliyokamatwa hifadhini, mkuu wa wilaya alisema kitendo hicho hakikubaliki na amewaonya wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani askari hao wako kwa mujibu wa sheria na wanatimiza wajibu wao.
Alisema pori hilo lina rasilimali muhimu ikiwemo wanyamapori adimu na misitu ya vyanzo vya maji kwahiyo lazima lihifadhiwe kwaajili ya matumzi ya vizazi vya sasa na vijavyo na kwamba tayari kuna operesheni inayoendelea kukabiliana na uhalifu unaofanywa na baadhi ya wananchi kwenye pori hilo.
“Kuna baadhi ya wananchi wanaishi ndani ya pori na kuchangia uharibifu wa mazingira, kwa bahari nzuri wenzetu wa Mamlaka ya wanyamapori Tanzania TAWA, wameshafanya tathimini ya hali hiyo na taratibu za kuwaondoa zikikamilika wataondoka” alisema Bwana Odunga.
Aidha Bwana Odunga amekitaka chama cha wafugaji kusaidia kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa kufuga kisasa na kuvuna mifugo yao waiuze na kujiendeleza kimaisha kwani jamii nyingi za wafugaji zinaishi maisha duni licha ya mifugo mingi waliyo nayo.
“Inashangaza kuona baadhi ya wafugaji wana ngombe zaidi ya elfu tano lakini wanaishi maisha duni, hawana makazi bora, usafiri na hata wanashindwa kupeleka watoto wao shule jambo ambalo halikubaliki” alisema mkuu wa wilaya.
Alisema wilaya imeanza zoezi la upigaji chapa wa mifugo kama njia muhimu ya utambuzi wa mifugo iliyoko katika wilaya hiyo zoezi linalotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa kumi ambapo zaidi ya ng’ombe laki wanatarajiwa kuwekewa alama za utambuzi.
Kwa upande wake Meneja wa pori la akiba la Sawagaswaga Alex Choyachoya alisema kuanzia sasa uongozi wa pori hilo umejipanga kukabiliana na vitendo vya uhalifu ikiwemo uingizaji wa mifugo na ujangili wa aina mbalimbali.
Aidha Bwana Choyachoya aliishukuru serikali kwa ushirikiano katika kushirikiana na askari wa mamlaka ya wanyamapori katika pori la akiba la Swagaswaga kwa kuimaimarisha doria zinazlenga kuimarisha vitendo vya uhalifu katika pori hilo.
Kuhusu wananchi waliowavamia askari wa wanyamapori wakiwa na sialaha za jadi ikiwemo mishale yenye sumu wakitaka kupora mifugo iliyokamatwa katika pori hilo alisema watu hao walikamatwa na wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya uhalifu wa kuingia ndani ya pori kinume cha sheria.

No comments