Header Ads

Responsive Ads Here

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba awataka watafiti kufanya utafiti wenye majibu ya changamoto kwa wafugaji


mif
Na Masanja Mabula –Pemba
MKUU  wa Mkoa wa Kaskazini Pemba  Omar Khamis Othman ameitaka Taasisi ya Wakala wa Utafiti wa Mifugo Zanzibar kufanya tafiti ambazo zitatoa majibu ya changamoto zinawakabili wafugaji .

Amesema wafugaji katika Mkoa wa Kaskazini Pemba wamekuwa wakiendesha shughuli zao za ufugaji kwa mazoea jambo ambalo linakwamisha harakati zao za kujikwamuwa kimaisha.
Akizungumza na ujumbe wa Taasisi hiyo  Ofisini kwake Wete , ukiongozwa na Mkurugenzi wake Dr  Kassim Gharib Juma , Mkuu wa Mkoa amesema changamoto ambayo zinahitaji  utafiti wa kina ni maradhi pamoja na malisho ya mifugo.
Aidha amesema iwapo changamoto hizo zitapatiwa ufumbuzi hali ya uchumi wa wananchi itaimarika  na mafanikio yatapatikana .
“Taasisi hii inapaswa kufanya utafiti ambao utatoa jibu la changamoto zinazowakabili wafugaji ambao wengi wao wanaendesha shughuli zao hizo kwa mazoea , jambo ambalo linakwamisha harakati zao kimaisha ”alisema .
Aliongeza kuwa “Bado mifugo inakabiliwa na changamoto ya maradhi pamoja na malisho , hivyo kuwepo na taasisi hii itakuwa ni mwarubaini wa hayo naomba sana mfanye kazi kwa uwadilifu na uwaminifu mkiitumikia serikali yenu ”alisisitiza
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kaskazini Pemba Ahmed Khalid Abdalla ameishauri taasisi hiyo kujikita zaidi kufanya tafiti za Kuku na Ng’ombe mifugo  ambayo inafugwa kwa wingi katika Mkoa huo.
“Wafugaji wengi wa Kuku na Ngombe wameanza kuvunjika moyo kutokana na mifugo yao kufa kutokana na maradhi , hivyo uwepo wa taasisi hii itawashawishi wananchi kuekeza katika sekta ya mifugo ”alieleza.
Katika maelezo yake Mkurungezi wa Taasisi ya Wakala wa Utafiti wa Mifugo Zanzibar Dk Kassim Gharib Juma amesema taasisi yake imekusudia kuliimarisha shamba la Chamanangwe ili liwe shamba darasa kwa wafugaji .
Amesema moja ya majukumu ya taasisi hiyo ni kufanya utafiti wa maradhi , malisho pamoja na masoko  na kuwataka wafungaji kuwa tayari kushirikiana na watendaji wa taasisi wakati wa ziara ya kufanya utafiti .
Dr Kassim amesema sehemu kubwa ya utafiti utakaofanyika Kisiwani Pemba utafanyika Mkoa wa Kaskazini Pemba kutokana na Mkoa huo na idadi kubwa ya mifugo kuliko Mkoa wa Kusini Pemba .

No comments